Prof. Janabi: Wanaume ombeni nafasi za kushiriki mafunzo mbalimbali
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Prof. Mohamed Janabi akizundua mpango mkakati wa mwaka 2022/23 -2025/2026 wa
taasisi hiyo wakati wa hafla fupi ya kuzindua mpango huo iliyofanyika leo
katika ukumbi wa mikutano wa JKCI jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) CPA Agnes Kuhenga akielezea mpango mkakati wa mwaka 2022/23
-2025/2026 wa JKCI jinsi utakavyofanya kazi kwa viongozi wa Taasisi hiyo wakati
wa hafla fupi ya kuzindua mpango huo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam
Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakimsikiliza Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) CPA Agnes Kuhenga wakati akiwaelezea kuhusu mkakati wa taasisi hiyo
mwaka 2022/23 -2025/2026.
Mwenyekiti wa kamati iliyoandaa mpango mkakati wa mwaka
2022/23 -2025/2026 wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
akielezea namna ambavyo mpango mkakati huo umelenga kuboresha huduma
zinazotolewa na Taasisi hiyo kwa wananchi wakati wa hafla fupi ya kuzindua
mpango mkakati huo iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa JKCI pamoja
na wajumbe wa kamati iliyoandaa mpango
mkakati wa Taasisi hiyo wa mwaka 2022/23 -2025/2026 mara baada ya kuuzindua leo
jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa kiume wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wametakiwa kuomba nafasi za mafunzo mbalimbali ili kuongeza ujuzi wa kazi
tofauti na ilivyo sasa ambapo wanawake ndio wanaoomba zaidi nafasi za kushiriki
mafunzo hayo.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akizundua mpango mkakati
wa JKCI wa mwaka 2022/23 -2025/2026.
Prof. Janabi alisema katika kutekeleza mpango mkakati wa kwanza
wa mwaka 2017-2022 JKCI imewekeza katika vifaa tiba vya kisasa hivyo basi kama
wafanyakazi hawataongeza taaluma zao kwa kusoma kozi za muda mrefu na mfupi
vifaa hivyo vitazidi taaluma walizonazo sasa na hivyo kushindwa kuvitumia.
“Taasisi yetu imekuwa ikiwawezesha wafanyakazi wa kada zote
wanaotaka kusoma kuongeza elimu ili waweze kuendana na maendeleo ya sayansi na
teknolojia changamoto iliyopo wanaume wanaojitokeza ni wachache ukilinganisha
na wanawake ninawaomba nanyi wanaume mjitokeze kwa wingi kuomba nafasi za
kusoma”,.
“Takwimu nilizonazo
zinaonesha wafanyakazi wengi wa jinsia ya kike wa JKCI wapo mstari wa mbele
kushiriki mafunzo ya kuongeza ujuzi, nawahimiza sasa wafanyakazi wa jinsia ya
kiume nanyi mjitokeze fursa hii ni yetu sote”, alisema Prof. Janabi.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mpango mkakati wa mwaka
2017-2022 Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa JKCI CPA Agnes Kuhenga alisema
mpango mkakati wa kwanza umeleta
mafanikio makubwa ikiwemo uboreshaji wa miundombinu na uwekezaji wa vifaa tiba
vya kisasa.
“Mpango Mkakati wa mwaka 2017-2022 umeiwezesha JKCI kufunga
mtambo mpya wa Cath lab, ujenzi wa duka la dawa za magonjwa mbalimbali,
uanzishwaji wa maabara ya kutengeneza dawa za maji kwa ajili ya watoto wenye
magonjwa ya moyo, ujenzi wa wodi ya watoto na ukarabati wa wodi za watu
maarufu”,.
“Pia mpango mkakati huo uliwezesha ununuliwaji wa vifaa vya
kisasa vya matibabu zaidi ya 500, uboreshwaji wa sehemu wanazokaa wauguzi,
pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha kwa asilimia
100”, alisema CPA Agnes.
CPA Agnes alisema mpango mkakati wa pili ulioanza kufanya
kazi mwaka huu wa fedha wa 2022/23 umeandaliwa na wataalamu kutoka JKCI tofauti
na ule wa kwanza ambao ulihusisha wadau kutoka nje ya taasisi kuuandaa.
“Nawapongeza wajumbe wa kamati ya kuandaa mpango mkakati wa
mwaka 2022/23 -2025/2026 kwa kufanya kazi nzuri na kubwa kwani hii ni mara yetu
ya kwanza kuwahusisha wataalam wetu kuandaa mpango huu tofauti na ule wa kwanza
ambao uliwahusisha wadau kutoka nje ya Taasisi”, alisema CPA Agnes.
Akielezea mpango mkakati wa mwaka 2022/23 -2025/2026
Mwenyekiti wa uandaaji wa mpango mkakati huo Dkt. Peter Kisenge alisema kazi ya
uandaaji wa mpango huo imekamilika sasa ni wakati kwa wafanyakazi wote kuusoma,
kuuelewa na kutimiza majukumu yao kama mpango huo unavyowataka kufanya.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema kwa kuwahusisha wataalam wa JKCI kuandaa mpango mkakati huo kumeongeza
wigo mpana kwa wanakamati ambao kupitia wao wafanyakazi wote wapewe uelewa wa
namna wanapaswa kutimiza majukumu yao kwa kufuata mpango mkakati wa mwaka
2022/23 -2025/2026.
“Nawashukuru wajumbe wa kamati ya kuandaa mpango mkakati wa
mwaka 2022/23 -2025/2026, ushirikiano na utayari mliouonesha wakati tunaandaa
muendelee kuuonyesha kwa wafanyakazi wengine pindi watakapohitaji kupata
ufafanuzi ili malengo tuliyoyaweka yaweze kufikiwa ifikapo mwaka 2026”, alisema
Dkt. Kisenge.
Comments
Post a Comment