Wataalam wa afya nchini wapatiwa mafunzo ya kimataifa ya jinsi ya kufanya kipimo cha kuangalia moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO)
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) yanayoendelea katika Taasisi hiyo Jijini Dar Es Salaam. Mafunzo hayo yaliyoudhuriwa na wataalam wa afya zaidi ya 100 yamefanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na
utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge akielezea namna mafunzo ya Echo yatakavyofanyika kwa washiriki wa
mafunzo ya upimaji wa jinsi moyo
unavyofanya kazi kwakutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) yanayoendelea
katika Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam
Mbunge wa viti Maalum Mhe. Dkt.
Alice Kaijage akielezea ujuzi atakaoupata katika mafunzo ya upimaji wa jinsi moyo unavyofanya kazi kwakutumia
mashine ya Echocardiogram (ECHO) yatakavyomsaidia katika taaluma yake wakati wa
mafunzo hayo ya siku mbili yanayoendelea katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
iliyopo Jijini Dar Es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo
kutoka Taasisi ya Piedmont Health iliyopo
Atlanta Georgia nchini Marekali Dkt. Mani Vannan akiwafundisha watalaam wa afya kutoka
hospitali mbalimbali nchini namna ya kupima kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) wakati wa mafunzo
hayo yanayoendelea katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar Es
Salaam.
Wataalam wa afya kutoka
hospitali mbalimbali nchini wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na
mkufunzi kutoka Taasisi ya Piedmont
Health iliyopo Atlanta Georgia nchini Marekali Dkt. Mani Vannan ya namna ya kupima
kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya
Echocardiogram (ECHO) wakati wa mafunzo hayo yanayoendelea katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete Jijini Dar Es Salaam.
Wataalam wa afya zaidi ya 100 kutoka hospitali
binafsi na hospitali za umma wameshiriki mafunzo yakimataifa ya siku mbili ya upimaji
wa jinsi moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) ambayo
yamefanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
Akizungumza na waandhishi wa Habari wakati
wa uzinduzi wa mafunzo hayo leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema kuwa mafunzo hayo yanatolewa
na wakufunzi na wabobezi wakuu wa magonjwa ya moyo kutoka nchini Marekani.
Prof. Janabi alisema kuwa lengo la
mafunzo hayo nikuongeza ujuzi kwa wataalam wa afya ili kusaidia na kupunguza wagonjwa
ambao wanaingia gharama kutoka mikoani kwenda JKCI kwa ajili ya kufanyiwa kipimo
cha Echo kwani wakiweza kuwagundua katika maeneo yao ya kazi wataweza kuchagua wagonjwa
wanaohitaji kufanyiwa matibabu zaidi na kuwatuma JKCI.
“Tumekua tukifanya mafunzo kama hayo huko
nyuma lakini kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani ndio maana leo tunasema haya ni
mafunzo yetu ya kwanza yakimataifa kwasababu tuna wabobezi na wataalam zaidi katika
uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) kutoka nchini Marekani”,
“Kwetu sisi wataalam wakutoa huduma za
matibabu ya moyo, hatuwezi kufanya upasuaji wa aina yoyote bila kufanya kipimo
cha Echo hivyo ujuzi tutakaoupata hapa utasaidia zaidi kuboresha huduma zetu na kuchagua wagonjwa wapi waende kwenye upasuaji
na wangapi wanaweza kutumia dawa bila ya kufanyiwa upasuaji”, aliseama Prof.
Janabi
Prof. Janabi alisema kuwa mafunzo ya upimaji
wa jinsi moyo unavyofanyakazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) yataendelea
kutolewa kila mwaka kwa wataalam wote wa afya bila kubagua waliopo katika hospitali
za umma na zile za binafsi ili kujifundisha mbinu mpya za kugundua matatizo ya moyo
awali kabla ya tatizo kuwa kubwa.
Mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mbunge
wa viti maalum Mhe. Dkt. Alice Kaijage alisema kuwa ameshiriki mafunzo ya upimaji
wa jinsi moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) ili
aweze kupata mbinu mpya na zakisasa katika kutoa huduma za matibabu ya moyo.
“Nikiwa bungeni tuna kituo cha afya hivyo
kwanjia moja ama nyingine naweza kusaidiana na wenzangu kama mtaalamu kupima moyo
unavyofanya kazi kwa wagonjwa wanaofika katika kituo hicho lakini pia kupitia taaluma
yangu natakiwa kuongeza ujuzi ili niweze kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia”
Kwa upande wake Mkufunzi kutoka Taasisi
ya Piedmont Health iliyopo Atlanta Georgia nchini Marekali Dkt. Mani Vannan alisema
kuwa anaamini katika mafunzo ya mara kwa mara katika taaluma ya afya na nimoja ya
matamanio yake kuona wataalam wa afya wanashiriki mafunzo ya kuongeza taaluma zao
kila wanapopata fursa.
“Naamini Taasisi hii inamisingi mizuri
katika taaluma ya upimaji wa jinsi moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya
Echocardiogram (ECHO), madhumuni ya mafunzo haya nikuifanya nchi hii kuwa kituo
cha ubora katika utoaji wa huduma za kibingwa za vipimo na matibabu ya moyo”,
alisema Dkt. Mani
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tiba Shirikishi
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delila Kimambo alisema kuwa kipimo
cha kuangalia jinsi moyo unavyofanyakazi ni moja ya huduma za tiba shirikishi ambayo
nimuhimu kwa mtaalam wa afya kujua matatizo aliyonayo mgonjwa na kumpa mwelekeo
wa huduma gani mgonjwa anastahili kupewa.
“Mgonjwa yeyote wa moyo nilazima afanyiwe
kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO), ni kipimo muhimu ambacho
wataalam waliopo hapa leo wanapaswa kukifahamu kwa undani zaidi ndio maana tumeandaa
mafunzo haya ili tuwakumbushe na kuwafundisha waweze kutoa huduma hiyo katika ubora
zaidi”,
“Unapofanya kipimo cha Echo vyema zaidi
unamsaidia mgonjwa kupata huduma bora zaidi, kumpa taarifa sahihi itakayomsaidia
katika matibabu yake pamoja na kujua tatizo lake kama linahitaji dawa ama upasuaji”,
alisema Dkt. Delila
Comments
Post a Comment