Kwa mara ya kwanza JKCI yafanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa kufungua tundu dogo kwenye kifua (Minimal Invasive Surgery)
Madaktari bingwa wa upasuaji mkubwa wa moyo na mishipa ya
damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Hospitali
ya King Faisal Specialist iliyopo nchini Saud Arabia kumfanyia upasuaji wa
kubadilisha mshipa mkubwa wa moyo (aneurysm repair) mgonjwa wakati wa kambi
maalum ya siku 6 ya matibabu ya moyo iliyofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo
Jijini Dar es Salaam
Mtaalam wa kuendesha mashine ya kuusaidia moyo na mapafu kufanya kazi (Heart lung machine) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sophia Lukonge akiendesha mashine hiyo wakati wa kambi maalum ya siku 6 ya matibabu ya moyo iliyofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya King Faisal Specialist iliyopo nchini Saud Arabia na kumalizika mwishoni mwa wiki katika Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam.
*********************************************************************************************************
Na: Genofeva Matemu
Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na madaktari kutoka Hospitali ya King Faisal Specialist iliyopo
nchini Saud Arabia chini ya Taasisi ya Muslim World League wamefanya upasuaji
maalum wa kufungua tundo dogo (minimal invasive surgery) kwenye kifua na
kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa wagonjwa watatu katika kambi maalum ya
matibabu ya siku sita.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi hiyo
iliyomalizika mwishoni wa wiki Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji wa Moyo wa
JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema kuwa katika upasuaji huo wanawake wanafanyiwa upasuaji
chini ya ziwa na kwa wanaume upasuaji unafanyika pembeni karibu na kwapa.
“Kwetu sisi wataalam wa JKCI huu ni upasuaji wetu wa kwanza
tumefanya wa kufungua tundu dogo kwenye kifua (minimal invasive surgery) na
moja ya malengo yetu ni kuongeza utaalam kila baada ya muda, tumekusudia mwaka
huu tuanze kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa kufungua kifua kwa sehemu ndogo
kwasababu ndio upasuaji wa viwango vya juu kwa sasa duniani”,
“Tumejifunza hatua za awali, tumejua vifaa gani vinahitajika,
maandalizi ya aina gani ya ziada yafanyike kwa wagonjwa na pia baada ya
upasuaji tumejifunza ni jinsi gani tunapaswa kuwahudumia wagonjwa hao, upasuaji
wa moyo siyo lazima uwe na mshono mkubwa, unakuwa na mshono kidogo, maumivu
kidogo na unapona haraka”, alisema Dkt. Angela
Akizungumzia idadi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji katika
kambi hiyo Dkt. Angela alisema kuwa jumla ya wagonjwa 15 ambao walihitaji
kubadilishiwa milango ya moyo, kupandikiza mishipa na kubadilisha mshipa mkubwa
wa moyo (aneurysm repair) wamefanyiwa upasuaji.
“Wagonjwa 8 walifanyiwa upasuaj wa kubadilishiwa milango ya
moyo ambapo kati yao wagonjwa 3 walifanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kwa kufungua
kifua sehemu ndogo chini ya ziwa ambapo wagonjwa hao walitoka chumba cha
uangalizi maalumu ICU baada ya siku moja na kwenda wodini wakiwa na kidonda
kidogo sana”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema wagonjwa wengine 5 walifanyiwa upasuaji
wa kupandikiza mishipa (bypass surgery) zaidi ya mitatu kwa njia ya kawaida
kutokana na matatizo yao kuwa makubwa hivyo kukosa nafasi ya kufunguliwa tundu
dogo ambapo wagonjwa 3 walifanyiwa upasuaji bila ya kuusimamisha moyo na wawili
walifanyiwa upasuaji kwa kuusimamisha moyo.
“Wagonjwa wawili wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa
kubadilisha mshipa mkubwa wa moyo (aneurysm repair) na hadi sasa wagonjwa wote
wanaendelea vizuri na wengine wameshatoka katika chumba cha uangalizi maalum
(ICU) wamerudishwa wodini”, aliasema Dkt. Angela
Aidha Dkt. Angela amewataka wananchi kujiwekea utaratibu wa
kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili wanapokuwa na tatizo la moyo
liweze kugundulika mapema kwani tatizo
linapojulikana mapema matibabu huwa rahisi kufanyika kwa wakati hivyo kuwezesha kupata matokeo mazuri zaidi na maisha bora baada ya upasuaji .
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa
ya damu kutoka Hospitali ya King Faisal Specialist iliyopo Nchini Saud Arabia chini
ya Taasisi ya Muslim World League Ali Haneef alisema kuwa madaktari wa Saud
Arabia wamekua wakishirikiana na madaktari wa JKCI mara kwa mara ambapo katika
kambi hiyo wamekuja na mbinu mpya ya upasuaji wa moyo wa kufungua tundu dogo
katika upasuaji mkubwa wa moyo.
“Tunaendeleza lengo letu la kuwasaidia wagonjwa wa moyo
lakini pia kubadilishana uzoefu na wataalam wenzetu wa hapa JKCI ambapo katika
kambi hii tumewafundisha mbinu mpya ya upasuaji wa moyo kwa kufungua sehemu
ndogo ya kifua na kufanya upasuaji mkubwa mbinu ambayo inarahishisha matibabu
na mgonjwa anapona haraka”,
“Wataalam wa JKCI wanaendelea kupanda viwango kwani hapo
awali ilitulazimu kuja kundi kubwa la wataalam wa maeneo yote kuanzia madaktari
wa usingizi, wauguzi wa chumba cha upasuaji na ICU na madaktari wa upasuaji
lakini katika kambi hii tumekuja wataalam wachache kwasababu uzoefu tuliobadilishana
nao umeleta matokeo chanya sasa tunafanya kwa pamoja”, alisema Dkt. Ali
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Muslim World League nchini
Tanzania Hassan Katungunya ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano
ambao wanautoa kufanikisha ujio wa wataalam hao kutoka nchini Saud Arabia kwa
ajili ya kutoa ujuzi na matibabu kwa watanzania.
“Naishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mliotupatia,
lakini pia nawashukuru wataalam wa afya waliotoka Saud Arabia kwa kufanikisha
zoezi la kuwasaidia watanzania wenye uhitaji wa kufanyiwa upasuaji wa moyo
lakini pia kuwaongezea wataalamu wetu ujuzi” alisema Hassan
Comments
Post a Comment