CRDB Marathon yarudisha tabasamu kwa watoto 200 waliofanyiwa upasuaji wa moyo

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mbio za CRDB Marathon msimu wa tatu zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 Agosti, 2022 kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo pamoja na matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi leo katika ukumbi wa mikutano wa Johari Rotana uliopo Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wadau mbalimbali wakifuatilia yaliyokuwa yakiendelea wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mbio za CRDB Marathon msimu wa tatu zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 Agosti, 2022 kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo pamoja na  matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi  leo katika ukumbi wa Johari Rotana uliopo jijini Dar es Salaam.

Mkugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela akiungana na wakurugenzi wa Taasisi washirika wa mbio za CRDB Marathon kutambulisha vifaa vitakavyotumika katika mbio hizo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mbio hizo msimu wa tatu zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 Agosti, 2022 kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo pamoja na matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi leo katika ukumbi wa mikutano wa Johari Rotana uliopo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela pamoja na wadau kutoka taasisi mbalimbali wakati wa mkutano na waandhishi wa habari kuhusu mbio za CRDB Marathon msimu wa tatu zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 Agosti, 2022 kwaajili ya kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo pamoja na  matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi leo katika ukumbi wa mikutano wa Johari Rotana uliopo jijini Dar es Salaam.


***************************************************************************************

Na: Genofeva Matemu

Watoto 200 wenye magonjwa ya moyo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia fedha zilipatikana katika msimu wa kwanza na wa pili wa CRDB Marathon.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu msimu wa tatu wa mbio hizo uliofanyika leo katika ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema kupitia mbio za CRDB watoto ambao familia zao hazina uwezo wameweza kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Prof. Janabi alisema kwa misimu miwili ya mbio za CRDB wamewafanyia upasuaji wa moyo watoto 200, ambapo kuna watoto kama wasingepata huduma za matibabu mapema labda wengine wasingeweza hata kusherehekea mwaka mmoja wa kuzaliwa kwao.

“JKCI ukiondoa Afrika ya Kusini sisi ndio tunafuata kuwa Taasisi ya kibingwa ya magonjwa ya moyo, hivyo tunaushukuru uongozi wa CRDB na wadau wote wanaochangia mbio hizi kwa lengo la kuokoa maisha ya watoto wenye uhitaji wa kupatiwa matibabu ya moyo”, alisema Prof. Janabi

Prof. Janabi aliwataka watanzania kujitokeza kushiriki mbio za CRDB kuendelea kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo pamoja na wanawake wajawazito wanaopitia changamoto mbalimbali zinazoweza kuwasababishia ugonjwa wa fistula.

“Rai yangu kwa watanzania nawaomba mjitokeze kushiriki mbio hizi za CRDB kuchangia matibabu ya watoto na wanawake lakini pia niwakumbushe kuwa kila mtu ajisajili kwenye mbio ambazo ana uwezo nazo kwani mazoezi yaliyopita kiwango ni hatari kwa afya zetu”, alisema Prof. Janabi

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela aliwashukuru wadau na wananchi ambao wamekuwa mstari wa mbele kujisajili na kutoa michango mbalimbali kwaajili ya kuongeza tabasamu kwa watanzania wenye uhitaji wa kupatiwa matibabu kupitia mbio hizo.

“Kama ambavyo kauli mbiu ya mbio hizi inavyosema ‘Kasi isambazao tabasamu’ mbio hizi zinalenga kumfurahisha kila mtu atakayeshiriki, kuleta uelewa wa changamoto zilizopo katika jamii yetu, kuishirikisha jamii changamoto hizo pamoja na kurejesha tumaini na kusambaza tabasamu kwa watoto wetu wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo JKCI na kuwagusa akina mama wenye ujauzito hatarishi wanaotibiwa CCBRT”,.

“Msimu wa tatu wa mbio za CRDB Marathon umelenga kukusanya fedha kwa ajili ya kuendelea kuwafikia watoto wenye uhitaji wa kufanyiwa upasuaji wa moyo na wanawake wenye ujauzito hatarishi ambapo hadi sasa watu zaidi ya 4,200 tayari wameshajisajiri kushiriki mbio hizi na kati yao watu 801 ni wakimbiaji kutoka nje ya nchi, haya ni mafanikio makubwa sana kwetu CRDB”,.

Nsekela alisema benki hiyo iliona mafanikio makubwa yaliyopo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwa hospitali kubwa ya kibingwa Afrika Mashariki na Kati, yenye teknolojia ya hali ya juu, wataalam wabobezi na yenye vifaa vya kisasa hivyo kupata motisha na kuona kuwa mahali sahihi kwa benki hiyo kuwekeza katika matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya bima ya maisha ya Sanlam Julius Magabe alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa washirika wa mbio za CRDB kutokana na mbio hizo kujikita zaidi katika kuhamasisha watu kusaidia jamii yenye uhitaji.

“Tunaishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizi zinazowaleta watanzania kushiriki katika kutatua changamoto katika jamii, Sanlam ni kampuni ambayo inajali afya na mazingira ya watu wake hivyo tunakila sababu ya sisi kushiriki katika mbio hizi”, alisema Magabe.

Mbio za CRDB zinatarajiwa kufanyika tarehe 14 Agosti 2022 ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango, huku viongozi mbalimbali wa Serikali wakimuunga mkono akiwemo Waziri wa Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu waziri wa Michezo Mhe. Pauline Gekule, Naibu Spika Mhe.  Mussa Zungu, Waziri wa TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, Katibu Mkuu wa CCM Mhe. Daniel Chongolo na viongozi kutoka Taasisi mbalimlbali nchini.


 

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)