Wasimamizi wa Mikataba ya Ununuzi JKCI wapatiwa mafunzo
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Ununuzi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Idd Lema akiwaelekeza wasimamizi wa mikataba ya ununuzi ya JKCI namna ya
kutekeleza majukumu yao wakati wa mafunzo ya jinsi ya kusimamia mikataba ya
JKCI yaliyofanyika leo katika Ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es
Salaam.
Wasimamizi wa mikataba ya Ununuzi ya Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kusimamia mikataba ya Ununuzi ya
Taasisi hiyo kwa mujibu wa vigezo, viwango vya ubora (technical specifications)
na matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 kama
ilivyorekebishwa mwaka 2016.
Akizungumza na wasimamizi wa mikataba ya JKCI, mwezeshaji wa
mafunzo kutoka Bodi ya Wataalamu wa Ugavi na Ununuzi (PSPTB) Jackson Musiba
alisema kuwa shughuli za manunuzi sio kwa Maafisa wa Kitengo cha Menejimenti ya
Ununuzi (PMU) peke yake bali zinamhusisha kila aliyehusika katika mchakato wa
ununuzi.
Mafunzo hayo ya siku moja kwa wasimamizi wa mikataba ya Ununuzi
ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete yalifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa
Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam na kubainika kuwa na changamoto kubwa
katika uandaaji wa viwango vya ubora (technical specifications).
“Mtumiaji wa vifaa (Idara Tumizi) zina jukumu la kusimamia
mikataba ya Ununuzi na kutunza taarifa zote zinazohusu mikataba lakini pia
mnahitaji mafunzo maalum ya uandaaji wa viwango vya ubora (technical
specifications) kwani hapa kuna changamoto kubwa ya uandaaji wa viwango vya
ubora”,
“Jukumu la Ununuzi wa mahitaji ya Ununuzi Serikalini ni la
Maafisa Ugavi na Ununuzi, kisheria jukumu hilo si la kila mtu hivyo pale Afisa
anapotaka kufanya manunuzi ni lazima awashirikishe watumishi wa Kitengo cha
Menejimenti ya Ununuzi (PMU) tofauti na hivyo mtumishi huyo atakuwa amevunja
Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016”,
alisema Musiba.
Musiba alisema kuwa fedha nyingi za Serikali hutumika katika
manunuzi ambapo Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 kama
ilivyorekebishwa mwaka 2016 imebainisha adhabu atakayopewa mtumishi
atakayetumia vibaya fedha ya serikali hivyo kuwataka watumishi wa JKCI wanapohusishwa
katika michakato ya manunuzi ya mali za umma kuwa waangalifu.
“Watumishi tunapaswa kuwashirikisha Maafisa Ugavi na Ununuzi katika
hatua zote za kuandaa mipango ya ununuzi ya Idara na Vitengo vyao, kuna kasumba
ambayo ipo katika taasisi nyingi ambapo Idara moja ama zaidi wanafanya mipango
ya manunuzi bila kuwahusisha watumishi wa Kitengo cha Menejimenti ya Ununuzi
(PMU) halafu mwisho wa siku wanatoa lawama kwa watumishi wa PMU kwa
kuchelewesha huduma wakati kama wangeshirikishwa tokea mwanzo taratibu za
ununuzi zingefanyika mapema”, alisema Musiba.
Aidha, Musiba alisema kuwa uandaaji wa viwango vya ubora
(technical specifications) ya vifaa ni moja ya changamoto kubwa inayokabili
masuala ya ununuzi na lawama nyingi hupelekwa kwa watumishi wa PMU wakati
kiuhalisia changamoto hiyo husababishwa na Idara Timizi (User Department)
ambaye aliomba vifaa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya kazi.
“Unapoandaa mahitaji yako lazima ujue unataka nini,
kinapatikana kwa msambazaji yupi ambaye ana bidhaa bora kuliko wengine na
gharama zake ni zipi, ukiyaainisha vizuri mahitaji yako itakua rahisi kuwaondoa
wasambazaji wengine ambao bidhaa zao hadhikidhi mahitaji yako na kubakia na
msambazaji ambaye anakidhi mahitaji yako”, alisema Musiba
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Ununuzi wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Idd Lemmah alisema kuwa mafunzo hayo kwa
wasimamizi wa mikataba ya Ununuzi yatasaidia kuboresha utendaji wa kazi
hususani suala zima la usimamizi wa mikataba ya ununuzi ya Taasisi hiyo.
“Mafunzo kama haya yataendelea kutolewa mara kwa mara kwa
wasimamizi wa mikataba ya Ununuzi ya JKCI ili kuondoa changamoto zote
zinazotukabili katika manunuzi ya mali za Taasisi”,
“Michango iliyotolewa na wasimamizi wa mikataba ya JKCI
wakati wa mafunzo inaonyesha ni jinsi gani somo limeeleweka, lakini katika
mafunzo haya tumebaini ipo changamoto ya uandaaji wa viwango vya ubora
(technical specifications) wakati wa ununuzi, changamoto hiyo tumeichukua na
kuahidi kuifanyia kazi”, alisema Lemmah.
Naye Fundi Sanifu vifaa tiba (Biomedical Engineer) wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete Veronica Mugendi alisema kuwa mafunzo ya jinsi ya
kusimamia mikataba ambayo ipo JKCI yamempa uelewa mkubwa na kumuainishia wajibu
na majukumu yake katika kusimamia mikataba.
“Mafunzo haya yataleta mabadiliko makubwa kwetu sisi
wasimamizi wa mikataba kwa sababu awali hata uandishi wangu wa ripoti haukuwa
katika mfumo ambao ni sahihi hivyo sasa nitabadilika kwani leo nimeweza kujua
napaswa kufanya nini na mipaka yangu ya kazi ni ipi”,
“Wito wangu kwa Taasisi ni kuhakikisha kuwa mafunzo haya
yanatolewa walau mara mbili kila mwaka kwasababu kila mwaka wasimamizi wa
mikataba wanabadilika ili hata wale ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria leo
wapate nafasi hiyo na wale watakaopewa jukumu hili mwakani waweze kuwa na elimu
hii tuliyoipata”, alisema Veronica
Comments
Post a Comment