JKCI yawagusa wananchi Njombe kupitia kampeni ya “Jua Namba Zako”
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Mbilinyi akimpa vipeperushi vya elimu ya magonjwa ya moyo Dorah Kachele ambaye ni Mkurugenzi wa vipindi na maudhui wa Kings FM ya mjini Njombe alipofika katika Hoteli ya Agreement kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali zinayotolewa kwenye Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kilichoandaliwa na Idara ya Habari- Maelezo.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Modesta Nyagawa akimpima shinikizo la damu mkazi wa Njombe aliyefika katika Hoteli ya Agreement iliyopo mjini Njombe kwaajili ya kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali zinazotolewa kwenye Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kilichoandaliwa na Idara ya Habari- Maelezo.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Modesta Nyagawa akimpima kiwango cha sukari kwenye damu mkazi wa Njombe aliyefika katika Hoteli ya Agreement iliyopo mjini Njombe kwaajili ya kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali zinayotolewa kwenye Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kilichoandaliwa na Idara ya Habari- Maelezo.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kupitia kampeni ya “Jua Namba Zako” ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa ya moyo na kupata matibabu kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari wa Taasisi hiyo Samweli Mbilinyi
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma za upimaji wa moyo
zinazotolewa na JKCI kwenye Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano,
Itifaki na Uhusiano Serikalini kinachofanyika katika Hoteli ya Agreement iliyopo
mjini Njombe.
Dkt. Mbilinyi alisema wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha
kuhusu magonjwa ya moyo jambo linalosababisha baadhi yao kuishi na matatizo
hayo bila kujitambua hadi wanapofika hospitalini wakiwa na matatizo mengine.
Alitoa mfano wa mgonjwa aliyefika katika upimaji huo ambao huduma
za upimaji wa magonjwa mbalimbali zinatolewa kwajili ya matatizo ya miguu
lakini baada ya kupimwa alibainika kuwa na shinikizo kubwa la damu lililozidi
kiwango cha kawaida hali iliyowalazimu wataalamu wa JKCI kumfanyia vipimo vya
moyo na kuanza matibabu mara moja.
“Tumegundua wananchi wengi hawajawahi kupima afya ya moyo wala
kufahamu viwango vyao vya afya. Kupitia kampeni ya Jua Namba Zako
tunawahamasisha wananchi wajitokeze kupima ili kujua hali zao mapema na kupata
tiba stahiki”, alisema Dkt. Mbilinyi.
Dkt. Mbilinyi alisema katika upimaji unaoendelea wamebaini watu
wengi wenye shinikizo la juu la damu na matatizo ya moyo ambao hawakuwahi
kufanyiwa vipimo vya moyo wala kujua hali zao za afya.
Aliishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa
kuwezesha upatikanaji wa dawa bure kwa wananchi wanaobainika kuwa na matatizo
mbalimbali ya afya ikiwemo magonjwa ya moyo katika upimaji huo.
“Ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupima afya zao.
Watakaobainika kuwa na changamoto watapatiwa ushauri wa kitaalamu, tiba, dawa
bila malipo na rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI”, alisisitiza.
Kwa upande wao wananchi waliopata huduma hizo walieleza
kufurahishwa na ujio wa wataalamu wa JKCI mkoani Njombe huku wakisema
umewasaidia kupata huduma karibu na maeneo yao na kupunguza gharama za kusafiri
kwenda Dar es Salaam.
Mmoja wa wananchi hao Farida Fredrick kutoka kijiji cha Ihalula,
alisema alifika kupata huduma baada ya kusikia madaktari wa JKCI wanatoa huduma
Njombe.
“Mimi ni mgonjwa wa moyo na huwa nahudhuria kliniki ya JKCI Dar es
Salaam. Niliposikia madaktari wako hapa Njombe nikaona nitumie nafasi hii
kupata huduma karibu na nyumbani, huduma ni nzuri sana na wananchi wengi
wajitokeze kupima”, alisema Farida.
Joseph Mwakalonge mkazi wa Njombe mjini alisema alikuwa
akisumbuliwa na maumivu ya kichwa pamoja na uchovu wa mara kwa mara bila
kufahamu chanzo chake lakini baada ya kufanyiwa uchunguzi alibainika kuwa na
shinikizo la juu la damu na kupewa matibabu.
“Naishukuru sana JKCI kwa kuleta huduma hizi karibu yetu. Sikuwahi
kujua kama nina tatizo la presha kubwa kiasi hiki lakini leo nimepata elimu,
vipimo na dawa kitu ambacho kitanisaidia kuutunza moyo wangu mapema ili usipate
madhara zaidi”,alisema Mwakalobe.
Naye Rehema Mlowe mkazi wa Makambako alisema alikuwa hajawahi
kupima afya ya moyo tangu alipogundulika kuwa na changamoto ya presha miaka
miwili iliyopita lakini ujio wa madaktari wa JKCI umempa nafasi ya kufanyiwa
uchunguzi wa kina na kupata ushauri wa namna ya kuishi kwa kufuata mtindo bora
wa maisha.
“Nimepata huduma nzuri na wataalamu wanatoa elimu kwa upendo
mkubwa. Ninawaomba wananchi wenzangu watumie fursa hii kuja kupima afya zao
mapema kabla hali haijawa mbaya”, alisema Rehema.
Katika upimaji huo JKCI inatoa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, uchunguzi wa shinikizo la damu, kipimo cha kuangalia uwingi wa sukari kwenye damu, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, elimu ya lishe bora na mtindo sahihi wa maisha, elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa moyo.




Comments
Post a Comment