Dkt. Kisenge awapongeza Wafanyakazi JKCI, Asisitiza ufanisi na weledi kazini
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni tano Mfanyakazi Hodari wa taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 Afisa Tawala Adila Musa wakati wa hafla ya kuwatambua na kuwapongeza wafanyakazi Hodari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni mbili Mfanyakazi Hodari wa taasisi hiyo nafasi ya pili kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 Mkaguzi wa Hesabu za Ndani Sitty Hamis wakati wa hafla ya kuwatambua na kuwapongeza wafanyakazi Hodari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni moja na nusu Mfanyakazi Hodari wa taasisi hiyo nafasi ya tatu kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 Afisa Muuguzi Edna Kajuna wakati wa hafla ya kuwatambua na kuwapongeza wafanyakazi hodari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa taasisi hiyo pamoja na wafanyakazi Hodari wa mwaka wa fedha wa 2025/2026 mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kuwatambua na kuwapongeza wafanyakazi Hodari iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa JKCI.
****************************************************************************************************************************************************************************************
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, amewapongeza wafanyakazi wa taasisi hiyo kwa kujituma na kufanya kazi kwa weledi hususan katika kuwahudumia wagonjwa wenye uhitaji maalum wakiwemo wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Dkt. Kisenge aliyasema hayo hivi karibuni wakati
wa mkutano wa wafanyakazi wa taasisi hiyo wa kuwatambua wafanyakazi hodari wa
mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo alisisitiza kuwa mafanikio ya taasisi hiyo
yanatokana na mchango wa kila mfanyakazi.
Alieleza kuwa licha ya kutolewa kwa tuzo kwa
baadhi ya wafanyakazi ukweli ni kwamba wafanyakazi wote ni hodari kutokana na
mchango wao katika kuendeleza huduma za moyo nchini.
“Utaratibu wa kuchagua wafanyakazi bora
ulifanyika kwa njia ya mfumo shirikishi wa kidijitali wa Best Employee System unaowezesha
wafanyakazi kupiga kura kwa uwazi na haki”, alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge aliwataka viongozi wa
taasisi hiyo kuwa karibu zaidi na wafanyakazi wanaowaongoza kwa kusikiliza
changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati ili kuongeza ufanisi na ari
ya kazi.
Pia alisisitiza umuhimu wa uwazi katika
ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya kila idara pamoja na kuongeza wigo wa
utoaji huduma ikiwemo kufanya upasuaji hata wakati wa sikukuu na mwishoni mwa
wiki.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu
wa JKCI, Ghati Chacha alisema ushindani wa kumpata mfanyakazi hodari ulikuwa
mkubwa akibainisha kuwa kwa mara ya kwanza mchakato huo pia umehusisha ngazi za
menejimenti na wasimamizi wa vitengo ili kuimarisha uwajibikaji katika kada
zote.
Aliongeza kuwa utaratibu wa kuchagua
wafanyakazi bora unafanyika kila mwaka kupitia mfumo wa kidijitali wa Best
Employee System ambapo kila kurugenzi huchagua wawakilishi wake kabla ya
kushindanishwa katika ngazi ya taasisi.
Kwa upande wake Mfanyakazi Hodari wa mwaka wa
fedha 2025/2026 Afisa Utawala Adila Musa aliwashukuru wafanyakazi wenzake kwa
imani waliyoonyesha kwake huku akisema ushindi huo ni wa pamoja kwani kila mfanyakazi
ana mchango katika mafanikio ya taasisi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa
taasisi hiyo Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Moyo kwa Watoto Dkt. Sulende
Kubhoja aliwahimiza wafanyakazi Hodari waliochaguliwa kuwa mfano bora kwa
wenzao kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi huku akisisitiza kwa
wafanyakazi wengine ambao hawakuchaguliwa umuhimu wa kuthamini na kusherehekea
mafanikio ya wenzao.
Wafanyakazi
hodari wa mwaka huu waliochaguliwa katika taasisi hiyo wote ni wanawake jambo
linaloonesha kwa mchango mkubwa wa wanawake katika kuendesha na kuimarisha
huduma za afya pamoja na kufanikisha malengo ya taasisi.
Afisa Utawala Adila Musa alishika nafasi ya kwanza kama Mfanyakazi Hodari wa mwaka wa fedha 2025/2026 akifuatiwa na Mkaguzi wa Hesabu za Ndani Sitty Hamis aliyeshika nafasi ya pili na Afisa Muuguzi Edna Kajuna aliyeshika nafasi ya tatu hatua inayoonesha wazi ufanisi na umahiri wa wanawake katika nyadhifa mbalimbali za kitaaluma ndani ya taasisi hiyo.





Comments
Post a Comment