JKCI yapongezwa kupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza
Afisa Uuguzi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Edna Kajuna akimuonesha jinsi moyo unavyokuwa
mwananchi aliyetembelea banda la JKCI wakati wa maonesho ya Dental Expo 2026 yaliyomalizika
leo katika viwanja vya Mlimani City vilivyopo jijini Dar es Salaam.
Na JKCI
*********************************************************************************************************
Washiriki wa maonesho
ya Dental Expo 2026 wameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuendelea
kutoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kutoa motisha
kwa jamii kufuata mtindo bora wa maisha.
Pongezi hizo zimetolewa
leo wakati wa kuhitimisha maonesho ya Dental Expo 2026 yaliyokuwa yakifanyika
katika viwanja vya Mlimani City vilivyopo jijini Dar es Salaam.
Washiriki hao walisema
elimu waliyoipata kupitia maonesho hayo itawasidia kuzingatia mtindo bora wa
maisha na kuisaidia jamii inayowazunguka kutambua magonjwa hayo ili isiwe
sehemu ya kupata magonjwa ya moyo.
Shadrack Mgeni mkazi wa
Tanga aliiomba JKCI inapopata nafasi ipeleke huduma na elimu kuhusu magonjwa ya
moyo mkoani Tanga kuisaidia jamii hiyo ili iweze kufuata mtindo bora wa maisha
hasa katika masuala la lishe.
Kwa upande wake Purity
Wanjiru kutoka Nairobi nchini Kenya alisema Tanzania imekuwa mfano mzuri katika
kutoa elimu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na kuitaka Kenya kuongeza nguvu ya
kutoa elimu ya magonjwa hayo, na madhari ya vilevi kuokoa vijana ambao ni taifa
la kesho.
“Nimefurahi kuifahamu
JKCI kabla sijaondoka Tanzania nitafika JKCI katika tawi lake la Arusha
Lutheran Medical Centre (ALMC) kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya kwani dalili
za magonjwa ya moyo nilizoambiwa hapa moja wapo imekuwa ikinipata lakini
sikuchukua hatua”, alisema Purity.
Akielezea muitikio wa wananchi kufika katika banda la
Taasisi hiyo kupata elimu Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Edna Kajuna alisema mwitiko wa rika la vijana umekuwa
mkubwa ukilinganishwa na watu wazima hivyo kuonesha kuwa vijana wameanza
kutambua umuhimu wa kuyajua na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
“Vijana wengi wamevutiwa
na kampeni ya “Jua Namba Zako” na kuona umuhimu wa kwenda kubadilisha mfumo wao
wa maisha, kama kweli watakuwa mstari wa mbele kubadilika itapunguza idadi ya
watu wanaopata magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Edna.
Edna alisema kampeni ya
“Jua Namba Zako” inalenga kuihamasisha jamii kujua viashiria vitano vinavyoweza
kusababisha magonjwa yasiyoambukiza ili iweze kujikinga na magonjwa hayo na
kutoathiri nguvu kazi ya taifa.
“Tumeshuhudia matukio
ya vifo vya gafla vinavyojitokeza katika jamii ambapo sababu mojawapo ni
kutokufanya uchunguzi wa mapema na kufahamu hali zetu kiafya”, alisema Edna.





Comments
Post a Comment