JKCI yawahimiza Wafanyakazi kupima Afya mara kwa mara kuepuka magonjwa yasiyoambukiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi zawadi ya mashine ya kupimia shinikizo la damu, joto la mwili na kiwango cha sukari Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha, Lucius Mwenda mara baada ya kumaliza kutoa elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo wakati wa zoezi la upimaji wa afya kwa watumishi wa Wizara hiyo jijini Dodoma.
.jpeg)
Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge wakati akitoa elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo katika zoezi la upimaji wa afya ya moyo kwa watumishi wa wizara hiyo jijini Dodoma.
*****************************************************************************************************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo ambayo yamekuwa chanzo cha vifo vya ghafla.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akitoa elimu ya jinsi ya
kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa wafanyakazi wa Wizara hiyo katika ukumbi
wa Kambarage jijini Dodoma.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo
alisema elimu hiyo imeenda sambamba na huduma za uchunguzi wa afya ya moyo kwa
wafanyakazi hao ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha jamii kujenga
utamaduni wa kujali afya zao mapema.
Akizungumza na wafanyakazi hao Dkt. Kisenge alisema magonjwa
yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi kutokana na mabadiliko ya mtindo wa
maisha, ulaji usiofaa, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe
uliopitiliza pamoja na msongo wa mawazo.
“Hivi sasa Taasisi yetu imekuja na kampeni ya ‘Jua Namba
Zako’ inayolenga kuhamasisha wananchi kufahamu viwango vya afya zao
ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, uzito unaolingana na
urefu pamoja na kiwango cha mafuta mwilini”, alisema Dkt. Kisenge.
Alifafanua kuwa shinikizo la damu linapaswa kuwa chini ya 120/80,
kiwango cha sukari kwenye damu chini ya 5.6, uzito unaolingana na urefu (BMI)
kati ya 18.5 hadi 24.9, mzunguko wa kiuno chini ya sentimita 94 kwa wanaume na
sentimita 80 kwa wanawake pamoja na mapigo ya moyo kati ya 60 hadi 100 kwa
dakika.
Dkt. Kisenge alisema unene kupita kiasi hususan kuongezeka kwa
ukubwa wa kiuno ni moja ya vihatarishi vya magonjwa ya moyo huku akiongeza kuwa
kadri umri unavyoongezeka ndivyo hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza
ikiwemo moyo, kisukari na saratani inavyoongezeka.
“Magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri afya za watu pamoja na
uzalishaji wa kiuchumi. Ni muhimu wananchi na wafanyakazi kuchukua hatua za
mapema kwa kupima afya zao mara kwa mara na kubadili mtindo wa maisha”, alisema.
Katika elimu hiyo wafanyakazi walihimizwa kufanya mazoezi mara kwa
mara, kutumia ngazi badala ya lifti inapowezekana, kupunguza muda wa kukaa
ofisini bila kufanya mazoezi, kula lishe bora, kunywa maji ya kutosha pamoja na
kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa
pombe kupita kiasi ikiwemo shisha.
“Watu wanaofanya mazoezi
wana nafasi kubwa ya kuishi maisha marefu na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Hata mazoezi madogo madogo yanayofanyika eneo la kazi yanaweza kusaidia
kuboresha afya”, alisema Dkt. Kisenge.
Alisema JKCI imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia
matawi yake ya Kariakoo, Kawe, Oysterbay, Hospitali ya Dar Group pamoja na
Arusha huku ikiwa na mpango wa kufungua tawi jipya Chato.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara
ya Fedha Lucius Mwenda aliishukuru JKCI kwa kutoa elimu na huduma za uchunguzi
wa afya ya moyo kwa wafanyakazi wa wizara hiyo.
“Ili tuweze kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi ni lazima tuwe na
afya njema. Elimu hii tuliyoipata imetukumbusha umuhimu wa kujali afya zetu na
tunatarajia kuona mabadiliko chanya kwa wafanyakazi wetu”, alisema Mwenda.
Aliongeza kuwa wafanyakazi wa wizara hiyo wamepokea elimu hiyo kwa
hamasa kubwa huku akiomba huduma za uchunguzi wa afya ziendelee kutolewa mara
kwa mara ili kuwasaidia wafanyakazi kutambua hali zao za afya mapema na
kuchukua hatua stahiki.
JKCI inaendelea na kampeni ya kuhamasisha wananchi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kupitia utoaji wa huduma za uchunguzi wa afya kwa kuwafuata wananchi mahali walipo ikiwemo kwenye maeneo yao ya kazi kwa lengo la kusaidia jamii kutambua hali zao za afya mapema na kupata ushauri wa kitaalamu.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Comments
Post a Comment