Zaidi ya watu 150 wabainika na matatizo ya Moyo katika kambi ya uchunguzi Njombe
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mahawa Asenga akimpima shinikizo la damu na mapigo ya moyo mwananchi aliyefika katika banda la JKCI Dar Group kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya wakati wa maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyomalizika hivi karibuni Mkoani Njombe. Jumla ya watu 386 wamefanyiwa uchunguzi wa afya katika maonesho hayo.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Happiness Shirima akitoa elimu ya mtindo bora wa maisha kujilinda na magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe waliofika katika banda la JKCI Dar Group kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya wakati wa maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyomalizika hivi karibuni Mkoani Njombe. Jumla ya watu 386 wamefanyiwa uchunguzi wa afya katika maonesho hayo.
****************************************************************************************************************************************************************************************
Jumla ya watu 386 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group.
Kambi hiyo ya siku sita ilifanyika
kwenye maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyomalizika hivi karibuni katika
viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema Mkoani Njombe.
Akizungumza na waandishi
wa habari wakati wa kuhitimisha kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moses Manumbu alisema kati ya watu
386 waliowahudumia 158 wamekutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kupewa rufaa
kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.
“Baada ya kuwafanyia
vipimo tumebaini watu wengi kuwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu bila
ya wao kujua lakini pia wengine tumewakuta na matatizo ya mfumo wa umeme wa
moyo na matatizo ya mishipa ya damu kuziba hivyo kuwapa rufaa kwaajili ya
matibabu zaidi”, alisema Dkt. Moses.
Mtaalamu huyo wa magonjwa
ya moyo alisema kwa upande wa watoto waliowahudumia waliwakuta na na matatizo
ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa
katika mpangilio wake na ugonjwa wa moyo
unaosababishwa na bakteria wanaoshambulia valvu za moyo (Rheumatic Heart
Diseases).
“Tunaendelea kuihamasisha
jamii kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kujali afya zao kwani afya
ndio mtaji wa maendelea, tukiwa na afya bora tutakuwa na uwezo wa kufanya kazi
na kupata maendeleo”, alisema Dkt. Moses.
Kwa upande wake Bernadetha
Kindu aliyefanyiwa uchunguzi wa afya katika banda la JKCI Dar Group alisema
amekuwa akisumbuliwa na maumivu makali ya kichwa kwa muda mrefu bila ya kujua
kama maumivu hayo ni dalili ya kuwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.
“Nawashauri wananchi
wenzangu tukiona dalili zozote za ugonjwa tufike katika vituo vya afya kufanya
uchunguzi, mimi nilichukulia kawaida na kutumia dawa bila ya ushauri wa daktari
jambo ambalo halikuwa salama kwa afya yangu”, alisema Bernadetha.
Bernadetha alisema baada
ya kuonana na daktari ameambiwa kuwa kutumia dawa bila kufanya uchunguzi wa
afya kungeweza kumletea madhara makubwa kiafya lakini pia kuhatarisha maisha
yake.
Naye Kazinja Ngoyai mkazi
wa Songea alisema imekuwa rahisi kwake kufuata huduma bingwa bobezi za moyo
katika Mkoa wa Njombe tofauti na angezifuata Dar es Salaam ingemgharimu na
kuchukua muda wake mwingi.
“Tunaposikia fursa kama hizi tusiziache zipite, mfano mzuri ni mimi nimetumia masaa machache kutoka Songea hadi hapa kuja kupima moyo wangu lakini pia nimetumia gharama ndogo ya usafiri tofauti na ningezifuata Dar es Salaam”, alisema Ngoyai.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment