Shinikizo la Damu laua kimyakimya, JKCI yatoa wito wa hatua za haraka

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima shinikizo la damu mwandishi wa habari wakati wa zoezi la upimaji afya ikiwa ni kuelekea katika  Maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani yanayofanyika kila mwaka tarehe 17 Mei.

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kliniki ya Oysterbay Noel Mushi akimpima shinikizo la damu mwandishi wa Azam TV Esterbella Malisa wakati wa zoezi la upimaji afya ikiwa ni kuelekea katika  Maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani yanayofanyika kila mwaka tarehe 17 Mei.

***************************************************************************************************************************************************************************************************

Mtindo usiofaa wa maisha umetajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazochangia kuongezeka kwa tatizo la shinikizo la juu la damu ugonjwa unaoendelea kuwa tishio kubwa la afya duniani na kusababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 10 kila mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2023 takribani watu bilioni 1.28 duniani wenye umri wa miaka 30 hadi 79 wanaishi na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu  huku karibu theluthi mbili ya wagonjwa hao wakiishi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati  ikiwemo nchi nyingi za Afrika.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kliniki ya Oysterbay jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Mei 17.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo alisema jamii inapaswa kuchukua hatua za mapema kujikinga dhidi ya ugonjwa huo huku  akieleza kuwa shinikizo la juu la damu lisipodhibitiwa linaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo na kupunguza nguvu kazi ya taifa.

"Wananchi wanapaswa kujua namba zao za shinikizo la damu kwani hatua hiyo rahisi inaweza kusaidia kugundua ugonjwa mapema, kuanza matibabu kwa wakati na kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza”. alisema Dkt. Kisenge.

Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi mara kwa mara, kula lishe bora yenye matunda na mboga za majani, kupunguza matumizi ya chumvi, pamoja na kuacha matumizi ya sigara na unywaji wa pombe kupita kiasi ili kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Dkt. Kisenge alieleza kuwa shinikizo la juu la damu ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayoweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kiharusi, matatizo ya moyo na figo kushindwa kufanya kazi vizuri hali inayochangia pia kudorora kwa uzalishaji na maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Dkt. Tatizo Waane alisema ugonjwa wa shinikizo la juu la damu umeendelea kuwa "muuaji wa kimyakimya" kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu dalili na madhara yake.

"Licha ya ugonjwa huu kuua kimyakimya  unaweza kudhibitiwa ikiwa wananchi watachukua tahadhari kwa kupima afya zao mapema, kutumia dawa kwa usahihi na kutositisha matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari", alisema Dkt. Waane.

Aliongeza kuwa katika mkutano huo JKCI pia ilitoa huduma ya uchunguzi wa afya pamoja na elimu kupitia kampeni ya “Jua Namba Zako”, inayolenga kuhamasisha wananchi kufahamu viwango vya afya zao ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, uwiano wa uzito na urefu pamoja na kiwango cha mafuta mwilini.

Akisisitiza umuhimu wa kauli mbiu ya mwaka huu isemayo: "Kudhibiti shinikizo la damu kwa pamoja: Pima shinikizo lako la damu mara kwa mara ushinde ugonjwa huu unaoua kimyakimya", Dkt. Waane alisema jamii na sekta ya afya zinapaswa kushirikiana katika kukabiliana na tatizo hilo.

Katika mkutano huo waandishi wa habari walipata fursa ya kupima afya zao bila malipo ambapo baadhi yao walieleza kufurahishwa na huduma hiyo kwa kuwa imewasaidia kutambua hali zao za afya na kuchukua hatua za kuimarisha mtindo bora wa maisha.

"Huduma hii imekuwa msaada mkubwa kwetu kwani kutokana na majukumu ya kazi mara nyingi tunakosa nafasi ya kufika vituo vya afya na kujua hali zetu kiafya. Nashauri huduma hizi ziendelee kutolewa hata kwenye maeneo yetu ya kazi ili watu wengi zaidi wajue namba zao", alisema Esterbella Malisa wa Azam TV.

Comments

Popular posts from this blog

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi