Watumishi wa Wizara ya Fedha wanufaika na kambi maalumu ya uchunguzi wa Moyo
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha wakisubiri kupata huduma za uchunguzi wa afya zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa afya iliyomalizika jana jijini Dodoma.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akitoa elimu ya “Jua Namba Zako” kwa mtumishi wa Wizara ya Fedha wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa afya kwa watumishi hao iliyomalizika jana jijini Dodoma.
Kambi hiyo iliratibiwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter
Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na mtaalamu wa kuzibua
mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo Dkt. Kisenge alisema lengo la kambi
hiyo ilikuwa ni kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo karibu zaidi
na wananchi pamoja na kutoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa
yasiyoambukiza.
“Magonjwa ya moyo hususan shinikizo la juu la damu ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo
vya watu wengi duniani. Kutokana na hali hiyo tumeona ni muhimu kutoa elimu ili
wananchi waone umuhimu wa kupima afya zao, kutambua hali zao mapema na kuchukua
hatua kabla hawajapata matatizo makubwa ya kiafya”.
“Kati ya watu tuliowaona 76 walibainika kuwa na shinikizo la juu
la damu, 18 walikutwa na tatizo la kisukari, 60 walikuwa na kiwango kikubwa cha
mafuta mwilini huku 33 wakipewa rufaa ya kuja JKCI kwa ajili ya uchunguzi na
matibabu zaidi”, alisema Dkt. Kisenge. . Aidha, watu 123 walifanyiwa kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
Dkt. Kisenge alisema baadhi ya watu waliokutwa na tatizo la shinikizo
la juu la damu hawakuwa wanajijua kabisa kuwa na shida hiyo, mmoja alikutwa na
tatizo la kutanuka kwa kuta za moyo na mmojatatizo la kuziba kwa mishipa ya
damu ya moyo nao hawa hawakuwa wanajijua kuwa na shida hizo.
“Kati ya watu tuliowaona kuna ambao walikuwa na changamoto ya
shinikizo la juu la damu. Wachache walikuwa tayari wanajua hali zao lakini
wengine walikuwa hawajui kabisa na kwa baadhi yao tumewaanzishia matibabu”
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya
zao angalau mara moja kwa mwaka ili waweze kutambua hali zao mapema na kuchukua
hatua stahiki kabla magonjwa hayajawa makubwa.
Kwa upande wao watumishi wa
Wizara ya Fedha waliopata huduma hizo waliishukuru JKCI kwa kuwafikishia huduma
ya upimaji wa moyo karibu na maeneo yao
ya kazi huku wakisema zimewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata elimu
muhimu ya namna ya kuishi maisha yenye afya.
John Nicodem ambaye ni Mhasibu Mwandamizi wa Wizara ya Fedha alisema
huduma hizo zimemwezesha kupata tathmini ya afya yake pamoja na ushauri wa
kitaalamu kuhusu namna ya kuendelea kuishi kwa afya bora.
“Nimefurahi kupata huduma hizi kwa sababu zimenisaidia kujua hali
yangu ya afya. Watanzania wengi hatuna utamaduni wa kupima afya mara kwa mara
lakini ni jambo muhimu sana ili tujue hali zetu mapema na kupata ushauri wa
kitaalamu”, alisema John.
Naye Neema Nyipamato Msaidizi wa Usimamizi wa Kumbukumbu alisema
elimu ya maogonjwa ya moyo aliyoipata imemsaidia kutambua umuhimu wa kuanza
mapema kujenga msingi wa maisha bora ya afya.
“Nimejifunza umuhimu wa kula lishe bora, kufanya mazoezi na kujenga mtindo mzuri wa maisha tangu ukiwa kijana. Afya bora ya uzeeni inaanza na maamuzi tunayofanya leo” alisema Neema.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment