Kampeni ya Jua Namba Zako yawafikia Maafisa Utawala na Rasilimali Watu nchini
Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akitoa mada kuhusu
magonjwa ya moyo kwa maafisa Utawala na Rasilimali watu wakati wa Mkutano Mkuu
wa pili Jumuishi wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali
watu katika Utumishi wa Umma Tanzania unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa Arusha (AICC).
Mkurugenzi wa Tiba
Shirikishi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa
na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Salehe Mwinchete akielezea huduma
ambazo Hospitali hiyo inazitoa kwa maafisa Utawala na Rasilimali watu wakati wa
Mkutano Mkuu wa pili Jumuishi wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Usimamizi
wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma Tanzania unaofanyika katika Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Afisa Muuguzi wa
Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Faustine akimpima sukari kwenye damu Afisa
Utawala aliyefika katika kliniki ya JKCI wakati wa Mkutano Mkuu wa pili
Jumuishi wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu
katika Utumishi wa Umma Tanzania unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa Arusha (AICC).
Daktari wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akimpatia ushauri wa wa kitaalamu mara
baada ya kumfanyia uchunguzi wa afya Afisa Utawala aliyefika katika kliniki ya
JKCI wakati wa Mkutano Mkuu wa pili Jumuishi wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala
na Usimamizi wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma Tanzania unaofanyika
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Picha na: JKCI
*******************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) yafikisha kampeni ya Jua Namba Zako kwa maafisa Utawala na
Rasilimali Watu wanaoshiriki Mkutano Mkuu wa pili Jumuishi wa Jumuiya za
Wataalamu wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma
Tanzania.
Kupitia Mkutano huo
unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) JKCI inatoa
huduma za uchunguzi wa viashiria vya magonjwa ya moyo kwa wataalamu hao huku
ikitoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya
moyo.
Akizungumza jana wakati
wa mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imetoa elimu kuwahimiza maafisa Utawala na
Rasiliamli Watu nchini kupima afya zao mara kwa mara na kujua namba zoa za
afya.
“Lengo letu kuu ni
kuihamasisha jamii kujua namba zao, kupima na kuchukua hatua, haya yote
yatatimia kama jamii itapima shinikizo la damu, uzito, urefu, sukari katika
damu, mapigo ya moyo na mafuta katika damu kwani vitu hivi vinachangia kwa
kiasi kikubwa magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo” alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge aliwaambia
maafisa Utawala na Rasilimali Watu wakijua namba zoa mapema watajizuia kupata
maathiriko makubwa yanayoweza kujitokeza na kuathiri utendaji kazi wao.
“Sambamba na malengo ya
mkutano huu, kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto, na kuboresha utendaji
kazi katika sekta ya umma pia tumieni muda huu kujua namba zenu kwani JKCI
tunataka kuhakikisha tumepunguza idadi ya watu wanaopata magonjwa ya moyo”, alisema
Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Afisa
Utumishi Mkuu kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba Rosada
Mbowe aliwashukuru wataalamu wa JKCI kufikisha huduma hizo katika mkutano huo
kwani umetoa fursa kwao kupima afya zao.
Rosada alisema kutokana
na yeye kuishi Bukoba ingekuwa ngumu kwake kufika JKCI kufanya uchunguzi kama
ambao amefanyika, labda ingemlazimu kufanya vipimo hivyo kama angekutana na
changamoto za kiafya.
“Utaratibu huu wa
kuchunguza afya kabla ya kuumwa ni mzuri, inatubidi tuwe tunafanya hivi mara
kwa mara kwani inakuweka kuwa salama, unajijua vizuri na kuchukua hatua mapema
kutokana na ushauri wa wataalamu wa afya”, alisema Rosada
Naye Afisa Utawala
kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Muguha Titus Muguha alisema
amekuwa na utaratibu wa kupima shinikizo la damu mara kwa mara hivyo akaona ni
wakati sasa kukutana na wataalamu wa JKCI kupata uhakika wa vipimo hivyo.
“Mambo ni mengi na maisha yamebadilika, ni
muhimu kufanya uchunguzi wa afya ikiwezekana JKCI iandae waraka wa kushauri
uongozi wa juu watumishi wa umma iwe ni lazima kufanya vipimo hivi kwani
itasaidia kuboresha afya za watumishi wa umma na kulinda nguvu kazi ya Taifa”,
alisema Mugaha
Mugaha alisema ikiwa
lazima kwa watumishi wa umma kupima na kujua namba zao hata jamii itachukua
hatua ya kupima na kujua namba zao lakini pia watumishi watakuwa mstari wa
mbele kuhakikisha familia zao nazo zinapima na kujilinda na magonjwa ya moyo.
“Magonjwa haya sio tu
yanaigharimu Serikali bali pia yanazigharimu hata familia zetu kwani inapotokea
familia ikakutana na changamoto za magonjwa ya moyo nguvu kazi katika familia
inapungua, kipato cha familia kinaelekezwa katika kupata matibabu na
kusababisha uchumi wa familia kushuka”, alisema Mugaha.
Comments
Post a Comment