Watumishi REA wahimizwa kufahamu “Namba Zao” kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Fatma Suedy akimpima shinikizo la damu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy wakati wa kambi maalumu ya utoaji wa elimu na uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.
Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kliniki ya Oysterbay Hamisi Msangi akimpima kiwango cha sukari kwenye damu Afisa Usafirishaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Samwel Sumwa wakati wa kambi maalumu ya utoaji wa elimu na uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa REA iliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Monica Kaganga akitoa elimu ya “Jua Namba Zako” kwa wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma wakati wa kambi maalumu ya utoaji wa elimu na uchunguzi wa afya.
Afisa Masoko wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Mndasha akieleza huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo wakati wa kambi maalumu ya utoaji wa elimu na uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Monica Kaganga akitoa elimu ya “Jua Namba Zako” kwa Mhandisi Miradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Isaac Sanga wakati wa kambi maalumu ya utoaji wa elimu na uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.

Baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakifuatilia elimu ya “Jua Namba Zako” iliyokuwa inatolewa na Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Monica Kaganga wakati wa kambi maalumu ya utoaji wa elimu na uchunguzi wa afya iliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.
******************************************************************************************************************************************************************************************************
Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kufahamu “namba zao” ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha sukari, mafuta mwilini, mapigo ya moyo na uwiano wa uzito kwa urefu (BMI) ili kutambua mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza kabla hayajaleta madhara makubwa kiafya.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Monica Kaganga wakati wa zoezi la utoaji wa elimu na huduma za
uchunguzi wa afya kwa watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) jijini
Dodoma kupitia kampeni ya Jua Namba Zako.
Akizungumza katika zoezi hilo Dkt.
Monica alisema njia mojawapo ya kugundua mapema magonjwa yasiyoambukiza ni
wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara na kufahamu viwango vya
afya zao kabla hali haijawa mbaya.
“Njia mojawapo ya kutambua dalili za
magonjwa haya mapema ni kujua namba zako. Tunapima shinikizo la damu, kiwango
cha sukari, mafuta mwilini, mapigo ya moyo pamoja na uwiano wa uzito kwa urefu
(BMI)”, alisema Dkt. Monica.
Alisema mwitikio wa watumishi wa REA
umekuwa mkubwa tangu kuanza kwa zoezi hilo ambalo lilifanyika kwa muda wa siku
tatu jambo linaloashiria kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa
kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
“Mwitikio umekuwa wa kuridhisha na tunaamini
elimu hii imewasaidia wafanyakazi kuelewa umuhimu wa kujua hali zao za afya.
Tutaendelea kuimarisha kampeni ya Jua Namba Zako ili kuwafikia wananchi
wengi zaidi”, alisema Dkt. Monica.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi
Hassan Saidy aliishukuru JKCI kwa kupeleka huduma za elimu na uchunguzi
wa afya kwa watumishi wa taasisi hiyo.
“Tunamshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa
JKCI, Dkt. Peter Kisenge pamoja na wataalamu wake kwa kutuletea huduma hizi
muhimu. Watumishi wamepima vipimo vya shinikizo la damu, sukari pamoja na
huduma nyingine za uchunguzi wa afya”, alisema Mhandisi Saidy.
Alitoa rai kwa waajiri wengine kuiga
utaratibu huo kwa kuwaleta wataalamu wa afya katika maeneo ya kazi ili
kuwasaidia watumishi kupima afya zao mapema.
Naye Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa REA, Magdalena Muhazi alisema elimu ya
jinsi ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza waliyoipata imewasaidia kuongeza
uelewa kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo yakiwemo ya moyo.
“Tumeelezwa mambo mengi muhimu kuhusu
afya zetu ikiwemo madhara ya matumizi mabaya ya pombe, ulaji usiofaa, msongo wa
mawazo na umuhimu wa kupima afya mara kwa mara”, alisema Magdalena.
Mkurugenzi wa Umeme Vijijini wa REA, Mhandisi Jones Olotu alisema huduma
hiyo imewapa fursa watumishi kujua hali zao za afya mapema pamoja na kupata ushauri
wa kitaalamu kuhusu mazoezi na mtindo bora wa maisha.
“Tumepata fursa ya kufahamu hali za afya zetu
kupitia kampeni ya Jua Namba Zako. Mbali na vipimo pia tumepata
ushauri wa kitaalamu kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi na kuishi maisha yenye
mtindo unaolinda afya zetu”, alisema Mhandisi Olotu.
Kampeni ya Jua Namba Zako inaendelea kuwa chachu ya kuhamasisha wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza kupitia elimu na vipimo vinavyotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment