JKCI yawataka wanamichezo, mashabiki kuchunguza afya ya moyo kuepuka vifo vya ghafla

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Samuel Rweyemamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group na Makamu wa Rais wa Timu ya Mpira wa Miguu wa Azam FC Abdulkarimu Popat pamoja wakijadili namna wataweza kuboresha ushirikiano baina yao baada ya kutembelea taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.


Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Gudila Swai akimpima mapigo ya moyo Diwani wa Kata ya Vingunguti na Meya Mstaafu wa jiji la Dar es Salaam Mhe. Omar Kumbilamoto aliyefika katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa mashabiki wa timu ya mpira wa miguu Azam FC iliyofanyika katika viwanja vya Hospitali hiyo jijini Dar es Salaam

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Helman Nicolaus akimpima kiwango cha sukari kwenye damu shabiki aliyefika katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa mashabiki wa timu ya mpira wa miguu wa Azam FC iliyofanyika katika viwanja vya Hospitali hiyo jijini Dar es Salaam.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Agnes Kajange akimpima uwiano wa urefu kwa uzito shabiki aliyefika katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa mashabiki wa timu ya mpira wa miguu wa Azam FC iliyofanyika katika viwanja vya Hospitali hiyo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya mashabiki wa Azam FC na Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospital ya Dar Group wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mazoezi ya pamoja katika viwanja vya Hospitali hiyo jijini Dar es Salaam.


 Makamu wa Rais wa Timu ya Mpira wa Miguu wa Azam FC Abdulkarimu Popat akiwa katika picha ya pamoja kwenye kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa mashabiki wa timu hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali Dar Group jijini Dar es Salaam.

Picha na JKCI

Na Mwandishi Maalumu-Dar es Salaam.

Wanamichezo na mashabiki wametakiwa kuchunguza afya ya moyo kabla ya kufanya mazoezi na kushiriki katika shughuli za michezo ili kuepuka vifo vya gafla vinavyoweza kujitokeza uwanjani.

Hayo yamesemwa na daktari bingwa wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group  Eva Wakuganda wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya ya moyo kwa wanamichezo na mashabiki wa timu ya mpira wa miguu ya Azam FC iliyofanyika jana katika viwanja vya Hospitali ya JKCI Dar Group iliyopo jijini Dar es Salaam.

Kambi hiyo iliambatana na utoaji wa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa pamoja na matembezi ya pamoja ya wafanyakazi wa JKCI Hospital ya Dar Group ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kueleka mchezo wa mzizima Derby kati ya Azam FC na Simba Sports Club.

Dkt. Eva alisema jumla ya mashabiki 95 walifanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo lengo likiwa kuhamasisha jamii hasa wanamichezo kufanya uchunguzi wa afya na kujua hali zao.

“Mashabiki wa Azam FC wameonyesha umuhimu wa kujua hali ya afya zao kabla ya kushuhudia mechi kati ya timu hiyo na Simba Sports Club kwani uchunguzi wa afya ya moyo ni muhimu katika kuzuia vifo vya gafla vinavyotokea wakati wa michezo”, alisema Dkt. Eva.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Timu ya Mpira wa Miguu ya Azam FC Abdulkarimu Popat alisema ataendelea kushirikiana na wataalamu wa JKCI Hospital ya Dar Group katika kuhakikisha kuwa mashabiki na wachezaji wanapata huduma za afya.

“Sikujua kama natakiwa kuchunguza afya yangu kabla ya kwenda uwanjani kushabikia, tumekuwa tukiona mashabiki wenye mapenzi na timu zao wanapata mstuko wa moyo pale timu zao zinapofungwa na hata wakati mwingine kupoteza maisha hivyo ni muhimu kufahamu hali zetu ili tusipate madhara”, alisema Popat.

Naye Diwani wa Kata ya Vingunguti na Meya Mstaafu wa jiji la Dar es Salaam Mhe. Omar Kumbilamoto aliishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa jamii.

 

“Zamani tulijua ubora wa huduma unapatikana katika hospital binafsi lakini baada ya kufika hapa na kufanyiwa uchunguzi wa afya nimejionea maboresho makubwa ya vifaa tiba na uwekezaji uliofanywa katika sekta ya afya”, alisema Kumbilamoto.

Mmoja wa mashabiki wa timu ya mpira wa miguu ya Azam FC Octavian Achimpota alisema zoezi la kufanyiwa uchunguzi wa afya kwa mashabiki limekuwa la kipekee na kuleta mchango mkubwa katika  kuimarisha afya za mashabiki na wanamichezo.

“Niwaombe wale ambao hawajanufaika na zoezi hili wajitokeze tarehe 16 mwezi huu kwani zoezi la uchunguza wa afya kwa mashabiki na wanamichezo litaendelea katika viwanja vya chamazi jijini Dar es Salaam”, alisema Octavian

-       Mwisho – 

Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma