Daktari wa upasuaji mdogo wa moyo kwa
watoto kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo
nchini Saudi Arabia Dkt. Jameel Al-Ata akiwaeleza wajumbe wa Kamati ya kudumu ya
Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii kuhusu upasuaji wa moyo kwa watoto
wanaofanyika katika Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI). Wajumbe hao walitembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona kambi ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka nchini Saudi Arabia.

Mbunge wa Jimbo la Mchinga ambaye pia ni
mjumbe wa Kamati
ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii Mhe. Salma Kikwete akisoma bango la Kituo cha Mfalme Salman cha
Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia ambacho kimetuma wataalamu
wake kwenda katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kushirikiana na wataalamu wa taasisi hiyo kufanya
upasuaji wa moyo kwa watoto. Kushoto ni Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo akifuatiwa na Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel.
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii Mhe. Stanslaus Nyongo, wajumbe wa kamati hiyo wakiwa katika
picha ya pamoja na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Kituo cha
Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia ambao
wako katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kufanya upasuaji
wa moyo kwa watoto kwa kushirikiana na wataalamu wa JKCI.
*******************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Na Andrew Chale - Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Huduma na Maendeleo ya Jamii imetembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
na kukutana na Wataalamu wa magonjwa ya moyo ya watoto kutoka Saudi Arabia
wanaoendesha kambi maalum ya upasuaji bure kwa watoto.
Kamati hiyo ikiongozwa na
Mwenyekiti wake, Stanslaus Nyongo (MB) iliambatana na Naibu Waziri
wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ambapo Wajumbe wa Kamati hiyo (Wabunge) waliweza
kupatiwa maelezo juu ya kambi hiyo ya matibabu na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Prof. Mohamed
Janabi.
Kambi hiyo ya matibabu ya moyo kwa watoto iliaanza Septemba
3, mwaka huu na kutarajia kumalizika Septembe 9, 2022 inafanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini
Saudi Arabia.
Aidha, JKCI kupitia kwa Dkt. Winnie Masakuya ilisema wanafanya kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto bure, ambapo
aliomba wazazi waweze kuwapeleka watoto wao kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupewa matibabu.
"Tunawaomba wazazi na
Madaktari wenye watoto wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo kama;matundu, mishipa
ya damu ya moyo kutokuwa katika mpangilio wake (ASD for device closure, PDA for
device closure, BAD, & Pulmonary valvular stenosis) wawalete kwa ajili ya
kufanyiwa uchunguzi na upasuaji kwa wale itakaolazimika." alisema
Dkt.Winnie Masakuya.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mchinga ambaye pia ni
mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii Mhe. Salma
Kikwete aliwaomba wazazi kutoka mikoa yote kuweza kujitokeza kwa wingi kupeleka
watoto wao wenye matatizo ya moyo katika Taasisi hiyo ili kupatiwa uchunguzi wa
moyo, kwani ni fursa ya kipekee ya uwepo wa wataalam hao hapa nchini.
Comments
Post a Comment