TPDC MARATHON YACHANGIA MILIONI 100 MATIBABU YA MOYO KWA WATOTO
Rais Mstaafu awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 100 Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi iliyotolewa leo
katika Viwanja vya Farasi Oyster bay Jijini Dar es Salaam na Shirika la Mafuta
la Taifa (TPDC) fedha zilizokusanywa kutoka kwa washiriki wa mbio za TPDC
Marathon wa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto 50 wenye magonjwa ya moyo
wanaotibiwa JKCI
Rais Mstaafu awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
akimkabidhi zawadi mshindi wa tatu mbio za kilometa 5 kwa watoto Cathleen
Maokola wakati wa mbio za TPDC Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya
watoto 50 wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika Viwanja vya Farasi
vilivyopo Oyster bay Jijini Dar es Salaam
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Atukumbukwe Ulimboka akimpima wingi wa sukari mwilini mwananchi aliyeshiriki
mbio za TPDC Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa
ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika Viwanja vya Farasi vilivyopo Oyster bay
Jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moris Obwanga akimpima Shinikizo la damu mwananchi aliyeshiriki mbio za TPDC Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika Viwanja vya Farasi vilivyopo Oyster bay Jijini Dar es Salaam
Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth
Mmari akimpa ushauri mwananchi aliyeshiriki mbio za TPDC Marathon kwa ajili ya
kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika
Viwanja vya Farasi vilivyopo Oyster bay Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akimsomea majibu ya vipimo vya viashiria vya magonjwa ya moyo mwananchi aliyeshiriki mbio za TPDC Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika Viwanja vya Farasi vilivyopo Oyster bay Jijini Dar es Salaam
Afisa Uuguzi kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama
(NBTS) Rosemary Bulemo akimtoa damu
mwananchi aliyeshiriki mbio za TPDC Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya
watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika Viwanja vya Farasi vilivyopo
Oyster bay Jijini Dar es Salaam. Wananchi hao pia walishiriki zoezi la
kuchangia damu kwa ajili ya watoto wanaofanyiwa upasuaji wa moyo.
Picha na: Khamis Mussa
************************************************************************************************************
Shilingi Milioni 100 zimetolewa na Shirika la Mafuta la Taifa
(TPDC) kupitia mbio za TPDC Marathon msimu wa kwanza kwa ajili ya kuchangia matibabu
ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete.
Akikabidhi hundi ya fedha hizo leo katika viwanja vya Farasi
vilivyopo Oyster bay jijini Dar es Salaam Rais wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete alisema kuwa mbio za TPDC zimeanza na madhumuni mazuri ya
kusaidia na kugharamaia upasuaji wa moyo kwa watoto 50 wenye matatizo ya moyo
wanaotibiwa JKCI.
Mhe. Kikwete alisema upasuaji wa moyo una gharama kubwa hivyo
mtu akiwa na lengo la kugharamia matibabu kwa wale ambao hawana uwezo wa kiuchumi
inapendeza ndani ya jamii yetu kwani hii inaonyesha dhumuni la kuiunga
mkono serikali ambayo baada ya kuona
jamii ina uwezo mdogo wa kiuchumi ikasukumwa kujenga Taasisi hiyo ili wananchi
wake wapate huduma kirahisi.
“Hapo awali Tanzania tulilazimika kupeleka wagonjwa nje kwa
matibabu ambapo gharama yake ilikua dola elfu saba kwa kila mgonjwa ambayo ni
ngumu kwa mtu wa kawaida kumudu matibabu, lakini pia serikali ilikua na mzigo
mkubwa hivyo kutupa motisha ya kuanza safari ya kujenga uwezo wetu wa ndani ambao
leo hii tunaona matunda yake”,
Mhe. Dkt. Kikwete alisema JKCI ndani ya miaka saba tangu
kuanzishwa kwake imekua kituo cha ubingwa kinachotoa huduma za matibabu ya moyo
kwa ukanda wa Afrika mashariki na kati hivyo kuwataka wadau kujitokeza
kushirikiana na JKCI ili kufanikisha lengo lake la kuokoa maisha ya watanzania
na kupunguza idadi ya watoto wanaosubiria kufanyiwa upasuaji wa moyo.
“Tusingekuwa na Taasisi hii sina hakika wale wote ambao
wameshapata matibabu JKCI wangekuwa sasa hivi wako katika hali gani, kwasababu
tangu kuanzishwa kwa Taasisi hii jumla ya wagonjwa wa moyo elfu saba na mia
sita wameshafanyiwa upasuaji wa moyo”,
“Nawapongeza wataalam wote waliopo katika Taasisi hii kwa
hatua kubwa waliyopiga na kuiheshimisha nchi yetu kwa kutoa msaada kwa
watanzania wenzetu, Tunaokoa maisha ya watu wengi na hadi sasa kuna watoto 511
wanaohitaji matibabu haya wapo kwenye foleni ya kusubiri huduma ya upasuaji wa
moyo”, alisema Mhe. Dkt. Kikwete
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Mafuta la Taifa (TPDC)
Dkt. James Mataragio alisema kuiachia serikali yenyewe kufanikisha huduma za
matiababu kwa watu wasiokuwa na uwezo haiwezekani inahitaji pia watu wengine
ili maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo yaokolewe.
“Nawashukuru wakimbiaji wote kwa kujitokeza siku hii ya leo
kuweza kutuunga mkono kuchangia watoto wenye magonjwa ya moyo, naamini wote
mlioshiriki mmekubali na kuguswa kuchangia watoto ambao wanatuhitaji ili
kufanikisha matibabu yao”,
“TPDC imekua ikijishughulisha na kufanya kazi na jamii
mbalimbali ambazo zinatuzunguka kwa kuchangia katika masuala ya elimu, michezo
na shughuli mbalimbali za kijamii lakini leo tumeona twende katika hatua
nyingine ya kusaidia kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo”, alisema Dkt.
James
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema kuwa kila mwaka Tanzania wanazaliwa watoto
milioni 2 ambapo asilimia 0.8 mpaka 1 ya watoto wanaozaliwa wanakuwa na
matatizo ya moyo na katika hao asilimia 25 uhitaji upasuaji wa moyo.
“Toka kuanzishwa kwa Taasisi yetu kila mwaka tumekuwa
tukifanya upasuaji wa moyo kwa watoto kati ya 250 na 300, kupitia mbio za TPDC
Marathon watoto 50 wamechangiwa shilingi milioni 100 ambapo kila mtoto
amechangiwa milioni 2 na fedha nyingine iliyobaki katika matibabu ya watoto hao
itajaziwa na serikali”,
“Tunawashukuru sana TPDC kwa kuguswa kuchangia matibabu ya
watoto wetu, kupitia msaada huu tunaweza kuwafanyia upasuaji watoto wote 50
ndani ya mwezi mmoja na kuwamaliza”, alisema Prof. Janabi
Comments
Post a Comment