Watu 791 wafanyiwa uchunguzi na matibabu katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanyika mkoani Arusha
Mkuu wa idara ya utafiti na mafunzo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge akimwonesha kitabu cha jinsi ya kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza mwananchi aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC wanafanya kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani.
Mkuu wa idara ya utafiti na mafunzo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) mwananchi aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC wanafanya kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani.
Mkuu wa kitengo cha utafiti kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo akiangalia dawa za moyo anazotumia mwananchi aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC wanafanya kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani.
*************************************************************************************************************************************************************************************
Watu 791 wamefanyiwa uchunguzi na kupata matibabu katika kambi
maalum ya matibabu ya moyo inayofanyika katika hospitali ya Arusha Lutheran
Medical Centre (ALMC) ambapo wengi wao wamekutwa na matatizo mbalimbali ya moyo
huku asilimia 25 wakiwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.
Kambi hiyo ya siku tano iliyoanza tarehe 26 na itamalizika
tarehe 30 mwezi huu inafanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha Lutheran Medica Centre.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha mkuu wa
idara ya utafiti na mafunzo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge alisema kufanyika kwa kambi
hiyo ya matibabu ni mojawapo ya maadhimisho ya siku ya moyo duniani
itakayofanyika tarehe 29 mwezi huu.
“Katika kambi hii wananchi wanapimwa vipimo mbalimbali vya
moyo ikiwa ni pamoja na urefu, uzito, kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito,
kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) na mfumo wa
umeme wa moyo (Electrocardiography). Wengine kwa mara ya kwanza wamegundulika
kuwa na matatizo ya moyo ikiwa ni pamoja
na kutanuka na kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo ambapo asilimia 5 tumewapa
rufaa ya kuja kufanyiwa vipimo zaidi katika Taasisi yetu”.
“Tumewafanyia pia uchunguzi watoto ambapo wengine tumewakuta
na matatizo ya valvu za moyo na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni
matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake hawa nao
tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge aliwaomba wananchi kuepuka tabia hatarishi
zinazoweza kuharibu mioyo yao hii ikiwa ni pamoja na uvutaji wa sigara na
unywaji wa pombe uliokithiri.
“Ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwa ni
pamoja na magonjwa ya moyo ni muhimu watu wakafuata mtindo bora wa maisha hii
ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi na kula vyakula bora”, alisema Dkt. Kisenge.
Mkuu huyo wa idara ya utafiti na mafunzo alisema Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete itaendelea kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo kwa kuwafuata mahali walipo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya
wa jinsi ya kutambua na kutibu magonjwa ya moyo kwani Serikali imenunua mashine
za kisasa za kuchunguza moyo na kuzisambaza katika Hospitali mbalimbali hapa
nchini.
Kwa upande wake mganga mkuu msaidizi wa Arusha Lutheran
Medical Centre (ALMC) ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani Wailesy Adam alisema kufanyika kwa kliniki ya pamoja kati ya hospitali hiyo na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kumeweza kuwasogezea huduma karibu wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani.
‘Kitu kikubwa walichokiona ni muitikio mkubwa wa watu na tumeona wagonjwa wengi na
bado kuna wengine ambao hawajapata nafasi ya kuonwa hivyo basi wataonwa siku
mbili zilizobaki. Watu wengi wanamatatizo ya moyo lakini wanakosa nafasi ya
kukutana na madaktari bingwa wa moyo, kuwepo kwa wataalamu hawa kumewasaidia
wananchi kupata huduma ya matibabu kirahisi”,.
“Tumejifunza kuna wagonjwa wengi wa moyo tofauti na tulivyokuwa
tunafikiria hapo awali na kama wataalamu wa afya tumejifunza kutoka kwa wenzetu
jinsi ya kuwatambua na kuwatibu wagonjwa hao”, alisema Dkt. Wailesy.
Afisa muuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Veronica
Vedastus alisema wako Arusha kwa ajili ya kupima magonjwa ya moyo na wamewapima
watu na kuwakuta na matatizo ya uzito mkubwa na shinikizo la damu kuwa juu
wamewapa ushauri wa lishe bora na matumizi sahihi ya dawa.
Veronica alisema, “Changamoto tuliyokutana nayo ni wagonjwa wenye
matatizo ya shinikizo la juu la damu wakipewa dawa wanazitumia kwa muda mfupi na
kuziacha pale wanapopata naafuu, tatizo likirudi tena wanatumia tena dawa na
kusababisha tatizo kuwa kubwa zaidi”.
“Ninatoa wito kwa
wauguzi wenzangu kutoa elimu za afya kwa wagonjwa ikiwemo magonjwa ya moyo, shinikizo
la juu la damu, lishe bora na umuhimu wa kufanya mazoezi pia wawashauri wagonjwa
wawe na utaratibu na kupima afya zao
mara kwa mara na kufuatilia ushauri wa wataalamu wa afya wanaopewa”.
Naye mzee Godfrey Ukio mkazi wa Arusha ambaye alipata huduma
ya uchunguzi na matibabu alisema aliambiwa mapigo ya moyo wake yako chini hivyo
basi baada ya kusikia madaktari kutoka JKCI watakuwepo katika hospitali hiyo akaamua
naye aende kufanyiwa uchunguzi.
“Baada ya kufanyiwa uchunguzi nimeambiwa kuna dawa ambazo
ninazitumia niendelee kuzitumia lakini nikija katika kliniki nyingine nitabadilishiwa
dawa. Huduma niliyoipata ni nzuri na wafanyakazi wamenivutia sana nawashauri wananchi
wenzangu ni muhimu wakapima afya zao na kupata ushauri wa jinsi ya kuishi na
kuepukana na magonjwa ya moyo.
“Huduma kama hizi ni za muhimu sana kwa wananchi hasa katika
sehemu ambazo zinadalili au uwezekano wa haya magonjwa kuwa mengi. Ninaiomba
Serikali iangalie namna ambavyo wananchi watapata huduma kama hii ya kupima afya zao kila wakati”,
alisema Mzee Ukio.
Comments
Post a Comment