Balozi wa Israel aishauri JKCI kuongeza ujuzi zaidi katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa
watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akimuelezea
Balozi wa Israel nchini Mhe. Michael Lotem kuhusu huduma za matibabu
zinazotolewa kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wakati wa ziara yake ya
kuangalia huduma zinazotolewa na JKCI jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimuonesha maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo Balozi wa
Israel nchini Mhe. Michael Lotem wakati wa ziara yake ya kuangalia huduma
zinazotolewa na Taasisi hiyo jana jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu akielezea namna ambavyo Israel kupitia
Shirika la Okoa moyo wa mtoto (Save a child heart – SACH) limeweza kusaidia
upatikanaji wa huduma bora za upasuaji wa moyo wakati balozi wa Israel nchini alipotembelea
JKCI kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa.
Balozi wa Israel nchini Mhe. Michael Lotem akizungumza na
viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake katika Taasisi hiyoya kuangalia huduma zinazatolewa
Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakimsikiliza balozi wa Israel nchini Mhe. Michael Lotem wakati wa ziara yake ya kuangalia huduma zinazotolewa na JKCI jana
jijini Dar es Salaam
Na: JKCI
*********************************************************************************************************************
Balozi wa Israel nchini Mhe. Michael Lotem ameishauri Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuongeza ujuzi zaidi katika kutoa huduma za
kibingwa za upasuaji wa moyo kwa kuwa Taasisi hiyo ni moja kati ya Hospitali
chache zinazotoa huduma hiyo barani Afrika.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam wakati Mhe.
Balozi Lotem alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya
kuangalia huduma zinazotolewa pamoja na kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya
Israel na Tanzania.
“Taasisi hii imekuwa ikishirikiana na Taasisi ya Okoa moyo wa
mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel kwa muda mrefu lengo
likiwa ni kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo, ujio wangu hapa ni
pamoja na kuangalia huduma wanazozitoa na kuendeleza ushirikiano uliopo”,
alisema Mhe. Balozi Lotem.
Balozi Lotem alisema kama JKCI inatembea, hivi sasa inatakiwa kukimbia kwani
huduma za matibabu ya moyo ni za muhimu na kuahidi kuwa nchi ya Israel
itaendelea kushirikiana na JKCI kuongeza ujuzi na kuwasaidia watoto wenye
magonjwa ya moyo.
“Taasisi hii haitakiwi kufurahia idadi ya namba za wagonjwa mnaowapatia huduma
bali mnatakiwa kufarahia uwepo wa huduma hizi za matibabu ya moyo hapa nchini
kwani zipo nchi ambazo hazina kabisa huduma za matibabu haya”, alisema Mhe.
Balozi Lotem.
Akizungumzia ujio wa Balozi wa Israel Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
ya JKCI Prof. William Mahalu alisema
JKCI na Israel wamekuwa na uhusiano wa muda mrefu, uhusiano unaozaa matunda
kwani Taasisi imefaidika na taaluma zinazotolewa Israel pamoja na watoto kwenda
nchini Israel kwa ajili ya matibabu ya moyo.
“Tunaamini baada ya Balozi wa Israel kufika hapa JKCI na
kuona tunachokifanya uhusiano wetu utaendelea kujengeka zaidi kwani taaluma ya
upasuaji wa moyo ni endelevu na wenzetu kutoka Israel wameendelea zaidi”.
“Israel inapokuja kufanya kambi maalum katika Taasisi yetu
utuletea vifaa tiba, taaluma mpya pamoja na kuendelea kujenga uhusiano ambao
umepelekea hata wataalam wetu kwenda nchini Israel kwa ajili ya kujifunza”,
alisema Prof. Mahalu
kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Serikali ya Israel imekuwa ikitoa
vifaa vya matibabu ya moyo na kutoa misaada ya matibabu kwa watoto wenye
magonjwa ya moyo kwa kuwapeleka nchini Israel kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji
wa moyo bila kulipia gharama yoyote ile.
Dkt. Kisenge alisema zaidi ya watoto 1000 wa Tanzania bara na
Zanzibar wameshapata matibabu kupitia wataalam wa afya kutoka nchini Israel lakini
pia wataalam wa JKCI kufaidika na uhusiano huo hivyo kupata nafasi ya kwenda
nchini Israel kwa ajili ya kuongezewa ujuzi.
“Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa kwanza hapa
nchini alipata mafunzo ya miaka mitano nchini Israel, mafunzo hayo ni ya
gharama kwani kumpa mafunzo daktari mmoja iligharimu zaidi ya milioni 60 ambazo
zilitolewa na Serikali ya Israel”.
“Wafanyakazi wengine 16 wa sekta ya afya nao walipata nafasi
ya kwenda nchini Israel kupata mafunzo ili kusaidia katika kutoa huduma wakati
wa upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto”, alisema Dkt. Kisenge ambaye pia ni
daktari bingwa wa magonjwa ya moyo.
Dkt. Kisenge alisema Balozi wa Israel kafurahishwa na huduma
za matibabu ya moyo zinayotolewa hapa nchini hivyo kuiomba JKCI kuendelea
kuwapa ujuzi madaktari wengine ili waweze kutoa huduma kwa wananchi wao pamoja
na nchi za jirani kwani nchi nyingi za Afrika hazina huduma za matibabu ya
moyo.
Aidha Dkt. Kisenge aliwakumbusha wananchi kujiunga na bima ya
afya kwani matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo watakapojiunga na bima ya afya
kutawasaidia kumudu gharama za matibabu kwani ugonjwa utokea wakati wowote.
Comments
Post a Comment