15 Wahitimu mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura
Wauguzi kutoka Hospitali mbalimbali nchini walioshiriki
mafunzo ya wiki 30 ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi
wakisikiliza wakati wa hafla fupi ya kuhitimu mafunzo hayo iliyofanyika hivi
karibuni katika Ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete iliyopo jijini Dar es
Salaam
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ambaye pia ni
mwezeshaji wa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi Joshua
Ogutu akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo wakati wa hafla fupi ya kuhitimu
iliyofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpa cheti mhitimu wa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi mshiriki wa mafunzo hayo wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya wiki 30 ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wahitimu hao iliyofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
**********************************************************************************************************
Wahitimu wa mafunzo ya jinsi ya
kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wametakiwa kuwa na upendo na
kuwajali wagonjwa hao pindi wanapokuwa wanawahudumia kwa sababu wagonjwa hao
wanahitaji upendo wa hali ya juu.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipokuwa katika
hafla fupi ya kuwapongeza wahitimu hao iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi
wa Taasisi hiyo.
Dkt. Kisenge alisema wahitimu hao
wamejifunza namna ya kuwahudumia wagonjwa mahututi kwa muda wa wiki 30 hivyo
wanatakiwa kwenda kufanya vizuri zaidi ya walivyokuwa wakifanya hapo awali
kabla ya kujifunza mafunzo hayo.
“Wagonjwa mahututi wanahitaji huduma
ya karibu, hivyo mnapaswa kuwahudumia kwa kuwaonyesha upendo na kuwajali kwani kwa
kufanya hivyo mtawapa faraja na watapona haraka, pia mfahamu ya kwamba sisi
sote ni wagonjwa wa kesho hivyo basi tuwahudumie wenzetu vizuri ili na sisi
tutakapokuwa wagonjwa tuhudumiwe inavyostahili”, alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt Kisenge alisema Serikali
imeongeza vyumba vya wagonjwa mahututi katika hospitali za kanda hivyo kuongeza
uhitaji wa wauguzi wa wagonjwa mahututi na kuwataka wahitimu hao kutumia fursa hiyo
kwenda kuziba mapengo hayo na kuonyesha ujuzi walioupata kwa ubora na ustadi wa
hali ya juu.
“Huko mnakoenda kwenye vituo vyenu
vya kazi mnatakiwa muwe mfano wa kuigwa kwa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi
vizuri na pia kuwafundisha wengine namna ya kuwahudumia wagonjwa hao kwa
kuwajali na kuwathamini”, alisisitiza Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
Idara ya Uuguzi JKCI Salma Wibonela alisema kupitia mafunzo hayo wahitimu hao
wanaenda kuwa mabalozi wazuri kuwahimiza wauguzi wenzao kupata mafunzo ya
kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi.
“Kupitia mafunzo haya mkaeneze ujuzi
huu kwa wengine ili nao waweze kupata mafunzo haya kwani wauguzi wote mkipata
mafunzo haya wagonjwa watapata huduma inayostahili”, alisema Salma
Naye mhitimu wa mafunzo hayo Cecilia
Luoga alisema wamejifunza namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi,
kutumia vifaa tiba kama vile kifaa cha kupima ufanyajikazi wa moyo (Ventilator)
pamoja na kumhudumia mtu aliyepata shambulio la moyo kwa ghafla (Advance
Cardiovascular heart Attack).
“Katika mafunzo haya tumejifunza
kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura kwa kuwajali na kuwaonyesha tumaini kuwa huduma
wanayoipata inaenda kuondoa changamoto walizokuwa nazo”, alisema Cecilia
Akiushukuru uongozi wa JKCI Cecilia
alisema Uongozi huo uendelee kutoa mafunzo hayo kwa wataalam wa afya nchini
kwani uhitaji wa elimu hiyo ni mkubwa.
“Tunaishukuru sana JKCI kwa jitihada
zote mlizozifanya kutupa mafunzo haya mzuri ya kuokoa maisha ya wagonjwa
wahututi na wanaohitaji huduma ya dharura, tuanaahidi yote mliyotufundisha tutayafanyia
kazi", alisema Cecilia
Comments
Post a Comment