Kongamano la siku ya wanawake Duniani lafanyika JKCI
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Engerasiya Kifai akiwafundisha wanawake wa JKCI namna ya kujali
afya zao wakati wa sherehe iliyoandaliwa na wanawake hao kuadhimisha kilele cha
siku ya wanawake dunia leo katika ukumbi wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es
Salaam
Mkurugenzi Mkuu Benki ya NMB Ruth Zaipuna akimkabidhi zawadi
mmoja ya washindi wa michezo mbalimbali iliyofanywa na wanawake wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete Afisa Muuguzi Magreth Mbaruk wakati wa sherehe ya
kuadhimishia kilele cha siku ya wanawake duniani leo katika Taasisi hiyo
iliyopo jijini Dar es Salaam
Wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) wametakiwa kuwa na ubunifu katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa
wananchi wanaowahudumia huku wakiendeleza upendo walionao kama wanawake.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa sherehe ya
kuadhimisha kilele cha siku ya wanawake duniani iliyofanywa na wanawake wa JKCI
katika Ukumbi wa Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge alisema kuwa kutokana na maumbili
ya uumbaji wanawake wamezawadiwa hali ya kuwa na upendo hivyo kuwahudumia
wagonjwa kwa upendo wa hali ya juu tofauti na wanaume wanavyowahudumia
wagonjwa.
Dkt. Kisenge aliongeza kuwa ni jukumu la
wanaume kuwalinda wanawake kwani wanawake ndio kila kitu katika familia,
ikitokea wanawake wakiumwa watoto wanakosa upendo wa mama kutokana na uzoefu
uliopo kuwa wanaume huwa ‘bize’ hivyo kuacha kazi ya malezi kuwa ya mwanamke.
“Tunaamini kazi kubwa ambayo wanawake
wameifanya katika Taasisi hii hadi kuwa bora Afrika Mashariki na kati,
muendelee kuwa wabunifu na kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia
kufikisha ujumbe wa afya bora kwa wanawake wengi zaidi na kuifanya Taasisi hii
kuwa bora duniani”, alisema Dkt. Kisenge
Akizungumza wakati wa kongamano hilo Mkurugenzi
Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna alisema usawa wa kijinsia bado ni changamoto
ingawa hatua kubwa imepigwa katika harakati za kufanikisha usawa ambapo takwimu
zinawabeba wanawake wengi katika masuala ya ufanisi mahala pa kazi.
Ruth alisema wanawake katika maeneo ya kazi wanatakiwa
kufahamu ya kwamba kazi ni wito na si kufanya kazi kwa mazoea na kuangalia
mshahara kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kukuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia
yaliyopo.
“Teknolojia ndio kila kitu kwani imebadili masuala mengi,
kwetu sisi watu wa Taasisi za fedha teknolojia imesaidia kufanikisha utoaji wa
huduma nje ya matawi yetu ambapo sasa mteja anaweza kujihudumia mwenyewe kwa
simu ya mkononi kuanzia kufungua akaunti hadi kupata mikopo midogo midogo”,
“Kwenye sekta ya afya, teknolojia imewezesha kurahisisha
huduma mbalimbali za kitabibu ikiwemo ‘robot operation’ huku ikipunguza maumivu
na athari za upasuaji sambamba na kuondoa tatizo la upotevu wa damu nyingi
wakati wa upasuaji”, alisema Ruth
Aidha Ruth ameahidi kuwa NMB katika kuboresha huduma
zinazotolewa katika vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU)
katika Taasisi hiyo itatoa vitanda vya ICU, magodoro pamoja na mashuka ili
wagonjwa waendelee kupatiwa huduma bora.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI
Engerasiya Kifai alisema wanawake wanatakiwa kuzingatia kula mlo kamili na
kufanya mazoezi kila siku ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja
na uzito uliokithiri.
“Wanawake tujenge utaratibu wa tuangalie afya zetu kwa ujumla
tuwe na utaratibu wa kupima kiwango cha sukari kila siku na msukumu wa damu,
pia tufanye mazoezi ya kuruka kamba na kufanya kazi za nyumbani hii itasaidia
miili yetu kuwa imara na afya bora”.
Dkt. Kifai alisema wanawake watumie muda wao pia kupumzika
walau masaa saba hadi nane kila siku kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia miili
yao kutokuchoka, kutumia muda wao pia kutoka kwenda kupumzika maeneo mazuri
kupumzisha akili.
“Wanawake mnatakiwa kufanya vitu ambavyo hamfanyi kila siku,
kujitafakari wenyewe, kwenda kwenye fukwe na hii itaboresha afya ya akili na
kuifanya akili ifikiri vema na kupunguza mawazo”, alisema Dkt. Kifai
Comments
Post a Comment