Watu 251 wapimwa magonjwa ya moyo Dodoma
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt.Godwin Mollel akiwapongeza wauguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutokana na huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo waliyoitoa kwa wananchi katika maadhimisho ya miaka 70 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga yaliyoenda sambamba na maonesho ya siku tatu ya huduma zinazotolewa na wauguzi yaliyomalizika jana katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Uuguzi wa JKCI Robert Mallya.
Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel akisaini kitabu cha wageni katika
banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maadhimisho ya miaka
70 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga yaliyoenda sambamba na maonesho ya siku tatu
ya huduma zinazotolewa na wauguzi yaliyomalizika jana katika viwanja vya
Nyerere Square jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Uuguzi wa JKCI Robert
Mallya.
Mkurugenzi wa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akimweleza Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel huduma za matibabu ya moyo zilizotolewa katika banda la Taasisi hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga yaliyoenda sambamba na maonesho ya siku tatu ya huduma zinazotolewa na wauguzi yaliyomalizika jana katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Jumla ya watu 251 wamepata huduma ya upimaji wa
viashiria vya magonjwa ya moyo pamoja na ushauri wa jinsi ya kuepukana na
magonjwa hayo kutoka kwa wauguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Upimaji huo ulifanyika katika maadhimisho ya miaka 70 ya
baraza la uuguzi na ukunga yaliyoenda sambamba na maonesho ya siku tatu ya
huduma zinazotolewa na wauguzi yaliyomalika jana katika viwanja vya Nyerere
Square jijini Dodoma.
Akitoa taarifa ya upimaji uliofanyika katika banda la Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mlollel, Mkurugenzi wa Uuguzi wa JKCI Robert
Mallya alisema katika banda hilo huduma zilizokuwa zinatolewa ni upimaji wa
kiwango cha sukari mwilini, shinikizo la damu, kueleza huduma za matibabu ya
moyo zinazotolewa, kutoa elimu ya lishe bora na jinsi ya kuepukana na magonjwa
ya moyo.
Mallya alisema kati ya watu 251 waliowafanyiwa vipimo 64 walikuwa
na tatizo la shinikizo la juu la damu ambapo 41 kati yao hawakuwa wanajijua kabisa kuwa na tatizo hilo
na 23 walikuwa wanajijua na wanatumia dawa .
“Kwa wale ambao hawakuwa wanajijua kuwa na tatizo la
shinikizo la juu la damu tumewashauri waende katika Hospitali za karibu na
wanapoishi kwa ajili ya kuanza matibabu na ambao wanajijua tumewashauri
wasiache kutumia dawa hata kama watajisikia wanaendelea vizuri”,.
“Tumetoa elimu ya lishe bora kwa wananchi waliotembelea
katika banda letu hii ikiwa ni pamoja na kuepuka kula vyakula vyenye chumvi na
mafuta mengi, wasipende kula na kunywa vinywaji vilivyosindikwa kwani vinamadhara katika afya ya moyo”, alisema Mallya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel
aliwapongeza wauguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kutoa huduma ya
upimaji na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa wananchi na kuwataka kuendelea kutoa
huduma hiyo pindi wanapopata nafasi ya kufanya hivyo.
“JKCI inatoa huduma nzuri ya matibabu ya moyo kwa wagonjwa wanaowatibu na kwa wananchi
wanaowahudumia katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ninawaomba muendelee kutoa
huduma hii nzuri ili isitokee Hospitali nyingine ikawashinda katika utoaji wa huduma bora ya matibabu ya
moyo hapa nchini”, alisisitiza Dkt. Mollel.
Jumla ya Taasisi na Hospitali za serikali na binafsi 26 zilishiriki katika maonesho hayo ambapo kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 70 ya baraza la uuguzi na ukunga ilikuwa ni Bima ya Afya kwa Wote Muuguzi na Mkunga Tarajio la Huduma Bora kwa Jamii.
Comments
Post a Comment