Dkt. Kisenge awataka wafanyakazi wa JKCI kuwafundisha wataalamu wa afya jinsi ya kutibu magonjwa ya moyo

 Wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakionesha mshikamano katika kutekeleza majukumu ya kazi kwa kushikana mikono na kuimba wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa JKCI kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Msaidizi wa Baraza hilo Theresia Marombe.

Mkurugenzi wa Idara ya Fedha na Mipango CPA Agnes Kuhenga akifafanua jambo wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa JKCI kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu wa Taasisi hiyo Adv. Maulid Kikondo.

Afisa Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Vida Mushi akiwasilisha makisio ya bajeti ya Taasisi hiyo ya mwaka wa fedha 2023/2024 wakati wa Kikao cha baraza la wafanyakazi wa JKCI kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa Dkt. Janeth Madete Madete akiwapongeza wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuendesha kikao cha baraza na kuwataka wafanyakazi kuzingatia ubora wa huduma wanazozitoa wakati wa kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Mjumbe wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Selemani Charles akisisitiza juu ya kuongeza kasi ya ufanyaji wa mazoezi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Mjumbe wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Haji Mbuta akielezea utekelezaji wa majukumu ya kitengo cha usimamizi wa mali na majengo wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

******************************************************************************************************************************************************************************

Wataalamu  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuwafundisha jinsi ya kuyatibu magonjwa ya moyo wahudumu wa afya wa hospitali mbalimbali hapa nchini ili huduma hiyo iweze kupatikana katika maeneo mengi zaidi.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema ni jukumu la Taasisi hiyo kuhakikisha ujuzi waliokuwa nao wataalamu wake wa kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo unawafikia wataalamu wengi zaidi nchini  jambo ambalo litasababisha wananchi wengi kufikiwa na huduma hiyo.

“Leo hii mtaalamu wa magonjwa ya moyo unaweza kupata tatizo la moyo ukiwa nje ya Dar es Salaam au kijini kwenu ulikozaliwa na unaweza kufa kwa kukosa huduma ya kibingwa kwa kuwa mahali ulipo haipatikani, lakini kama tutawafundisha wataalamu wenzetu jinsi ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo na huduma hii ikapatikana katika Hospitali zote itasaidia kila mgonjwa kupata huduma kwa wakati”.

“Katika Taasisi yetu tumejipanga kila mfanyakazi kuanzia mlinzi hadi wakurugenzi ambao siyo wa kada ya afya kupewa mafunzo ya jinsi ya kuokoa maisha ya mtu aliyepata tatizo la dharura la kiafya ninaamini kwa kuwapatia mafunzo haya kutawasaidia kuokoa maisha ya watu watakaopata matatizo ya dharura ya kiafya mahali popote pale watakapokuwa”,alisema Dkt. Kisenge.

 Aidha Dkt. Kisenge aliwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa baraza hilo kwa utendaji wa kazi wanaoufanya na kuwataka kuendelea kuwahudumia watanzania wenye matatatizo ya moyo huku wakifuata mpango mkakati wa Taasisi hiyo kwa mwaka 2022/23 – 2025/26  kwa kutimiza malengo waliyojiwekea.

Dkt. Kisenge alishukuru, “Ninawashukuru wafanyakazi wa Taasisi hii kwa kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano ninawaomba tuendelee kushikamana kwa kufuata dira ya JKCI ili iwe taasisi ya Kimataifa”, .

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa Dkt. Janeth Madete aliwapongeza viongozi wa baraza hilo kwa kuongoza kikao vizuri na kujadili mambo mbalimbali ya kazi za Taasisi hiyo kwa faida ya watanzania.

Dkt. Janeth alisema kuwepo kwake katika kikao hicho alijifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na namna wajumbe wa baraza hilo walivyojadili kwa pamoja jinsi ya kutoa huduma bora kwa wananchi wakiwemo wagonjwa.

“Nimeona hapa mmejadili maslahi ya wafanyakazi wakiwemo wa chini ambao mishahara yao ni midogo, ninaupongeza uongozi wa JKCI kwa kuangalia maslahi ya wafanyakazi wa chini kwa kufanya hivi utendaji kazi wa Taasisi hii utaenda vizuri”, alipongeza Dkt. Janeth.


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024