Dkt. Kisenge aishukuru Israel kwa kutoa huduma za matibabu kwa watoto
Akizungumza baada ya kusaini mikataba ya miaka mitatu wa
makubaliano na Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda na Hospitali ya Taifa
ya Moyo ya nchini Zambia wa kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo
wataalamu wa afya wa hospitali hizo Dkt. Kisenge alisema SACH imekuwa
ikiwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo kupata matibabu pamoja na kuwapa ujuzi
madaktari wa JKCI.
Dkt. Kisenge alisema SACH ilianza ushirikiano na JKCI tangu
mwaka 2015 kwa kuwachukuwa watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo hayakuweza
kutibiwa hapa nchini na kuwapeleka Israel kwa ajili ya matibabu ambapo sasa
JKCI imekuwa na uwezo wa kutibu magonjwa hayo kwa watoto hivyo kuiunganisha
JKCI na nchi za Rwanda na Zambia ili nazo ziweze kupata ujuzi huo.
“Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la Nchini Israel limekuwa
likiwahudumia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotoka katika familia duni kuokoa
maisha yao na pale walipohitaji kuwapeleka nchini Israel walifanya hivyo kwa
upendo”,alisema Dkt. Kisenge.
Akizungumza katika Hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel Simon
Fisher alisema hatua iliyofikia hadi Rwanda na Zambia kukubali kusaini mikataba
hiyo imetokana na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya SACH na JKCI.
“Leo hii Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inafanya upasuaji
mkubwa wa moyo pamoja na upasuaji wa tundu dogo kwa watoto kwa kujitegemea
naamini baada ya miaka kadhaa wenzetu wa Rwanda na Zambia nao watakuwa na uwezo
huo”, alisema Fisher
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya
nchini Zambia Dkt. Shumba Chabwela alisema kusaini mkataba wa makubaliano ya
kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa nchini
Zambia kunaonyesha utimilifu wa ushirikiano uliojengwa na waasisi wa nchi za
Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na wa Zambia Keneth Kaunda.
“Kwa niaba ya nchi ya Zambia tunatoa shukrani zetu za dhati
kwa kutupa nafasi ya kushirikiana nasi kuwahudumia wagonjwa wetu, kabla hata ya
kusaini mkataba huu tayari tulishaanza kuleta wataalam wetu kujifunza katika
Taasisi hii”, alisema Dkt. Shumba.
Naye Naibu Mtendaji Mkuu Hospitali ya King Faisal ya nchini
Rwanda Frederic Ngirabacu alisema ushirikiano katika sekta ya afya na sekta
nyingine vinapaswa kufanyika baina ya nchi za Afrika ili kwa pamoja ziweze
kukuwa na kuacha kutafuta huduma katika mataifa ya mbali.
“Tumeanza ushirikiano na JKCI wiki hii lakini pia tumefurahi
kukuta waafrika wenzetu kutoka Zambia wanashirikiana nao, hii inaonyesha
ukomavu katika nchi zetu za Afrika”, alisema Ngirabacu.
Ngirabacu alisema Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la nchini
Israel limekuwa likisaidia kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto wenye
magonjwa ya moyo waliopo nchini Rwanda na sasa kuwaunganisha na JKCI ili
kuendeleza mashirikiano jambo ambalo hawakulitarajia hapo awali.
Comments
Post a Comment