Iringa washukuru kupata huduma za matibabu ya moyo
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Epheta
Edward akimpima wingi wa sukari mwilini mkazi wa Iringa Magreth Sanga wakati wa
kambi maalum ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanywa na
wataalam wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Iringa.
Daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) Regina
Kipemba akishirikiana na Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Gerson Mpondo kumfanyia mwananchi kipimo cha kuangalia jinsi mfumo wa
umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG) wakati wa kambi
maalum ya siku tano inayofanywa na wataalam kutoka JKCI kwa kushirikiana na
wenzao wa IRRH.
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo jakaya Kikwete (JKCI) Makrina
Komba akimuuliza maswali ya ufahamu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo
magonjwa ya moyo mkazi wa Iringa Christina Chibona kabla ya kufanyiwa uchunguzi
na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano inayoendelea katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Na: JKCI
***********************************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Iringa wameishukuru Serikali ya awamu ya
sita kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuwezesha huduma za kibingwa
za uchunguzi na matibabu ya moyo kuwafikia kwa karibu kwani wananchi wengi
hawana uwezo wa kufuata huduma za kibingwa mahali zilipo.
Pongezi hizo zimetolewa na wananchi mbalimbali waliofika
katika kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo inayoendelea katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH).
Akizungumza baada ya kupatiwa matibabu ya moyo mkazi wa
Iringa Mzee Nicholas Kinyamagoha alisema hakuwahi kufanya uchunguzi wa moyo
wake tangu kuzaliwa kwake kutokana na huduma hizo kuwa mbali na sehemu
anayoendesha maisha yake.
Mzee Nicholas alisema baada ya kusikia ujio wa madaktari
bingwa wa moyo Mkoani Iringa akaona ndio fursa pekee anayoweza kutumia
kuchunguza moyo wake kwani kutokana na umri wake kuwa zaidi ya miaka 60 yupo
katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Nashukuru leo nimefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Iringa na kupata fursa ya kupimwa moyo wangu, awali walishangaa kuona shinikizo
langu la damu kuwa juu lakini baada ya kuwaeleza taarifa mbaya niliyopokea
wakati nikiwa kwenye foleni kusubiri matibabu walinipa muda wa kupumzika na
kuchunguzwa tena shinikizo langu la damu”, alisema Mzee Nicholas.
Mzee Nicholas alisema ikiwezekana huduma za uchunguzi wa magonjwa
yasiyoambukiza ambayo sio rahisi kuyapata katika Hospitali zilizopo mikoani
ziwe zinatolewa angalau mara moja kwa mwaka ili wananchi wapate nafasi ya
kutibiwa kwa wakati pale wanapokutwa na magonjwa hayo.
“Nimefurahi sana leo nimepima moyo wangu kwa mara ya kwanza,
nimeweza kujua namna ya kujikinga ili nisipate magonjwa ya moyo na
nimesisitizwa nisiache kutumia dawa za shinikizo la damu ambazo nimekuwa
nikizitumia kwa miaka miwili sasa”, alisema Mzee Nicholas.
Akizunguma kwa nyakati tofauti mkazi wa Iringa Felister
Chang’a alisema mwaka 2020 alikuwa na dalili za kupumua kwa shida, maumivu
makali upande wa kushoto wa kifua yaliyoenda hadi mgongoni hivyo kufika katika
moja ya Hospitali zilizopo Iringa na kupimwa moyo lakini majibu yalitoka kuwa
hana shida ya moyo.
Felister alisema baada ya uchunguzi aliofanyiwa mwaka 2020
alipewa dawa za maumivu na kuendelea na maisha lakini mwaka huu zile dalili
zimerudi na hakuwa na chakufanya kwani hapo awali alishaambiwa sio shida ya
moyo.
“Niliposikia ujio wa madaktari bingwa wa moyo kutoka JKCI
kwakweli nilifurahi sana kwani naamini leo naenda kupata suluhu ya tatizo
nililinalo kwasababu ninapopata maumivu ya kifua na kushindwa kupumua
kunanifanya nishindwe hata kufanya shughuli zangu”, alisema Felister.
“Jana nilimleta mtoto wangu hapa kwa ajili ya kutibiwa, baada
ya kufika hapa nikaona bango linaloonyesha uwepo wa madaktari bingwa wa moyo
nikakumbuka mimi pia nahitaji kumuona daktari wa moyo kutokana na hali yangu ya
maumivu ya kifua, nashukuru sijakutwa na shida ya moyo wameweza kunichunguza na
kuona tatizo la vidonda vya tumbo”, alisema Felister.
Akiongea kwa furaha Felister amewashukuru Madaktari bingwa wa
moyo kwa kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi wa Iringa kwani bila ya wao kufika
asingejua kama maumivu anayoyapata yanasababishwa na vidonda vya tumbo.
Naye mkazi wa Songea aliyesafiri kufuata huduma za matibabu
ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa Zamda Bakari alisema baada
ya kusikia ujio wa madaktari bingwa wa moyo hakuona shida kusafiri kutoka
Songea kufuata huduma hiyo kwani amekuwa akihitaji kuchunguza moyo kwa muda
mrefu.
“Nilimpoteza baba yangu kwa kifo cha ghafla na baada ya
kufuatilia tuliambiwa alipata shambulio la moyo hivyo kumsababishia kupata kifo
cha ghafla, baada ya kifo cha baba yetu nimekuwa makini nikisikia huduma za
kibingwa za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza nawiwa kuchunguza afya yangu
ili nijitambue”, alisema Zamda.
Zamda aliwashauri wananchi wanzake kupima afya zao mara kwa
mara pale wanapopata nafasi kwani kumpoteza mtu wa karibu kwa kushindwa kujua
kama alikuwa anaumwa inaumiza.
Comments
Post a Comment