Dkt. Kisenge: Fanyeni kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi kazini
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia tawi la JKCI uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia Taifa Dkt. Samuel Rweyemamu akizungumza na wanachama wa chama hicho tawi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter
Kisenge wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa JKCI.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema kukiwa na ushirikiano wa vyama vya wafanyakazi, wafanyakazi na uongozi kunasababisha watu kufanya kazi
kwa kujituma na kutoa huduma bora kwa wagonjwa lakini kama hakuna ushirikiano
atakayeumia ni mgonjwa.
“Dira ya Taasisi yetu ni kuwa kiwango cha juu kimataifa kwa
usimamizi, utafiti na mafunzo ya moyo haya yote yatawezekana kama tutafanya
kazi kwa pamoja na kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanapatikana, kusikiliza
changamoto za wafanyakazi na kuzifanyia kazi”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema
viongozi wa chama hicho bado wanakazi kubwa ya kuwakusanya pamoja madaktari na
wafamasia ili waweze kutetea maslahi yao na kushirikiana katika taaluma zao.
“Angalieni namna ya kufanya uwekezaji mkubwa ili chama kipate
fedha zaidi na kuweza kujiendesha zaidi kuliko kutegemea fedha za michango ya
wanachama”, alishauri Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Dkt. Samuel
Rweyemamu aliushukuru uongozi wa Taasisi hiyo kwa kukiwezesha chama hicho
kufanya kazi zao bila tatizo lolote lile.
Dkt. Rweyemamu alisema lengo la kuanzishwa kwa chama cha
wafanyakazi, madaktari na wafamasia ni kutetea maslahi ya wanachama hivyo basi ni
muhimu wanachama hao wakaungana kwa pamoja na kutetea haki zao za msingi.
“Madaktari na Wafamasia wanakutana na changamoto mbalimbali
za kazi hivyo basi kama tutaungana kwa pamoja na kuweza kutatua changamoto hizi
tunaweza kufika mbali zaidi na kufanya kazi zetu bila ya kuwa na manung’uniko”,
alisema Dkt. Rweyemamu.
Naye katibu wa chama hicho Tawi la JKCI aliyemaliza muda wake
Dkt. George Longopa alisema ni muhimu kwa madaktari na wafamasia wakaona
umuhimu wa kujiunga na chama hicho ili waweze kufanya maamuzi ya pamoja.
“Chama hiki ni muhimu kwani kinawakusanya watu wa kada moja
ambao wanakutana na kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata fursa
za mafunzo na kutatua changamoto zinazowakabili”,alisema Dkt. Longopa.
Katika mkutano huo pia ulifanyika uchaguzi wa viongozi
watakaoongoza chama cha wafanyakazi, madaktari na wafamasia tawi la Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha miaka miwili ambapo Dkt. Tryphone
Kagaruki alichaguliwa kuwa mwenyekiti, Mfamasia Hadija Madende mwenyekiti
wanawake, Dkt. Khairoon Mohamed mwenyekiti vijana, Mfamasia Yusuph Mwakatobe
katibu na Dkt. Nakigunda Kiroga katibu wanawake.
Wajumbe waliochaguliwa ni Dkt. George Longopa, Mfamasia
Miraji Dhahir , Dkt. Honoratha Maucky na Mfamasia Ndenasha Kimario.
Comments
Post a Comment