Watu 601 wapimwa moyo Iringa
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zabella
Mkojera akimsikiliza mkazi wa Iringa Sifael Kivamba wakati akimfanyia utafiti
wa ufahamu wa magonjwa ya moyo kabla ya kufanyiwa vipimo vya moyo katika kambi
maalum ya matibabu ya moyo iliyomalizika leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Iringa (IRRH)
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna
Faraji akimpima mzinguko wa tumbo mkazi wa Iringa kabla ya kufanyiwa vipimo vya
moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyomalizika leo katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH)
Na: JKCI
********************************************************************************************************************
Jumla ya watu 601 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo katika
kambi maalum iliyokuwa ikifanywa na madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Iringa (IRRH).
Kambi hiyo ya siku tano iliyoenda sambamba na utoaji wa
mafunzo ya kutumia mashine ya kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography – ECHO) kwa wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Iringa imemalizika leo ambao watu wazima
571 na watoto 30 wamepatiwa matibabu ya moyo huku tatizo kubwa lililoonekana kwa
watu wazima likiwa ni shinikizo la juu la damu.
Akizungumza na waandishi wa habari Daktari wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallagyo alisema wametoa rufaa kwa wagonjwa 80
waliohitaji uchunguzi zaidi na wale waliohitaji upasuaji mkubwa na mdogo wa
moyo kwenda JKCI kwa ajili ya kupatiwa matibabu hayo.
Dkt. Pedro alisema watu wazima wengi waliofanyiwa uchunguzi
katika kambi hiyo wamekutwa na magonjwa ya shinikizo la juu la damu, magonjwa
ya mishipa ya moyo kuziba na magonjwa ya valvu za moyo kuziba au kuvujisha damu
kwenye moyo.
“Asilimia 56 ya watu wazima waliofanyiwa vipimo vya moyo
walikutwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, utafiti tulioufanya tumeona
wagonjwa hawa hawapo katika matumizi mazuri ya dawa, bado kuna ule uelewa mdogo
wa kwamba dawa za presha zinatumika kwa muda mfupi na mtu anavyojisikia vizuri
anaziacha hivyo kuleta matokeo mabaya yanayoweza kusababisha matatizo ya figo,
uoni hafifu, kiharusi na matatizo mengine”, alisema Dkt. Pedro
Upande wa watoto Dkt. Pedro alisema wamewapa rufaa watoto 16
waliokutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ambapo watoto watano walikuwa na
magonjwa ya moyo waliyoyapata baada ya kuzaliwa yaani moyo kutanuka na valvu
kutokufanya kazi vizuri.
“Watoto wengine 11 tuliowapa rufaa ni wale wenye magonjwa ya
moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu, mishipa mikubwa inayotoa damu kwenye
moyo kupeleka mwilini na kwenye mapafu kupishana hivyo kuhitaji rufaa ya haraka
kufika JKCI kwa ajili ya upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Pedro
Dkt. Pedro alisema watoto walioonwa katika kambi hiyo na
kupewa rufaa wengi wao walikuwa katika hali mbaya hivyo kuhitija kusafirishwa
haraka kwenda Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya matibabu zaidi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Iringa (IRRH) Dkt. Alfred Mwakalebela amewapongeza wataalam wa JKCI kwa kufanya
kazi kwa kujituma kuwahudumia wananchi wa Iringa kwa upendo.
Dkt. Mwakalebela alisema kupitia kambi hiyo wameweza kupata
maono yanayoonyesha ukubwa wa matatizo ya moyo kwa wananchi wanaowahudumia
kwani hapo awali hawakujua kama uhitaji wa tiba ya moyo kuwa mkubwa kama
ambavyo imeonekana katika wiki ya moja ya matibabu hayo.
“Watu wa Iringa wana hamu sana ya kujua afya zao naomba
muendelee kuja Iringa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wetu kwani bado wanayo
kiu ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Dkt.
Mwakalebela
Naye Afisa Lishe Kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Husna Faraji alisema asilimia 60 ya watu waliojitokeza kupimwa moyo walikuwa na
uzito uliopitiliza hivyo kuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
“Matokeo haya tumeyapata baada ya kufanya kipimo cha uwiano kati
ya urefu na uzito pamoja na kipimo cha kuangalia mzunguko wa mafuta kwenye eneo
la tumbo na kuwakuta watu wengi na uzito mkubwa pamoja na viriba tumbo”,
alisema Husna.
Husna alisema uandaaji wa vyakula vya nafaka pamoja na ulaji
wa vyakula hivyo katika Mkoa wa Iringa inaweza kuwa sababu ya watu wengi kupata
uzito uliopitiliza jambo ambalo kiafya si zuri.
“Watu wengi walioshiriki katika zoezi la upimaji huu
wametuambia kwamba uandaaji wa unga wa ugali ujulikanao kwa jina la Kiverege
ambao mahindi uoshwa, kukobolewa, kusagwa na baadaye kuanika tena unga ule kwa
siku tatu hadi nne hivyo kuondoa virutubisho vilivyopo katika mahindi”,
“Upatikanaji na ulaji wa mboga za majini katika Mkoa huu uko
vizuri lakini changamoto inakuja kwenye uandaaji wa mboga hizo kwani zimekuwa
zikipikwa kwa muda mrefu hivyo kupoteza virutubisho vyake”, alisema Husna.
Comments
Post a Comment