China kuleta vifaa tiba nchini
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimuelezea mafanikio ya Taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake
Naibu Waziri Mkuu wa Serikali ya Watu wa China Mhe. Liu Guozhong alipofanya
ziara katika Taasisi hiyo leo kuona huduma zinazotolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimuelezea huduma zinazotolewa katika chumba cha upasuaji
wa tundu dogo (CathLab) Naibu Waziri Mkuu wa Serikali ya Watu wa China Mhe. Liu
Guozhong alipofanya ziara katika Taasisi hiyo leo kuona huduma zinazotolewa.
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel akiwa katika
picha ya pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Serikali ya Watu wa China Mhe. Liu
Guozhong na viongozi wengine wa Serikali mara baada ya ziara ya Naibu Waziri
Mkuu huyo kutembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo kuona huduma
zinazotolewa.
Na: JKCI
****************************************************************************************************
Tanzania na China zakubaliana kuanzisha mfumo wa upatikanaji
wa vifaa tiba vinavyotumika kutoa huduma za matibabu ya moyo kutoka nchini China
kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo.
Ushirikiano huo unatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa vifaa
vinavyotumika kutoa huduma za matibabu ya moyo na matibabu mengine yanayohitaji
vifaa tiba kupunguza rasimu ya upatikanaji wa vifaa tiba.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Naibu
Waziri Mkuu kutoka Serikali ya watu wa China Mhe. Liu Guozhong Naibu Waziri wa
Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel alisema katika majadiliano na Naibu waziri huyo
China imekubali kutoa msaada wa vifaa tiba nchini pamoja na kuanza kwa
ushirikiano wa kuagiza vifaa tiba nchini China.
“Tumekubaliana kupitia Bohari ya Dawa (MSD) tutaenda
kushirikiana na Serikali ya Watu wa China kupata vifaa tiba ambavyo mara nyingi
tumekuwa tukiviagiza katika mataifa ya mbali na kuchukua muda mrefu kutufikia”,
alisema Dkt. Mollel
Dkt. Mollel alisema
Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa Bohari ya Dawa (MSD) inaenda moja kwa moja
katika viwanda vilivyopo nchini China kununua vifaa tiba hivyo kupunguza
gharama za matibabu.
“Tanzania tayari tuna sayansi kubwa, lakini vifaa mbalimbali
vinavyotumika kila siku katika kutoa huduma za matibabu havipatikani hapa
nchini kwasababu hatuna viwanda vinavyozalisha vifaa hivyo”,
“Haya ni matunda ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
kwani tunapomuona akitembelea nchi mbalimbali duniani anafanya mambo makubwa ya
ushirikiano na mataifa anayoyatembelea yaliyokuwa kisayansi na kiteknolojia ili
kwapamoja tujifunze na kutumia fursa zilizopo kuendeleza sekta yetu ya afya”,
alisema Dkt. Mollel
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imekuwa moja ya Taasisi kubwa
zinazotoa huduma za matibabu ya mogonjwa ya moyo barani Afrika, na kuwa
yakwanza kufanya upasuaji mkubwa wa moyo na upasuaji wa moyo kwa watoto nchini
yote hayo yakiwa ni matunda ya ushirikiano wa nchi ya Tanzania na China.
Dkt. Kisenge alisema leo Naibu Waziri Mkuu kutoka Serikali ya
Watu wa China amefika JKCI kujionea vifaa vilivyowekezwa vyenye teknolojia ya
kisasa duniani pamoja na kuwasalimia wataalamu wa afya waliopo nchini kutoka
Serikali ya watu wa China ambao wamekuwa wakibadilishana nao uzoefu.
“Tumepata ugeni wa Naibu Waziri Mkuu kutoka Serikali ya Watu
wa China aliyetembelea Taasisi yetu kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya
Tanzania na china, Namshukuru sana Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwakutusaidia
katika rasilimali watu kwani sasa tuna madaktari bingwa wa hali ya juu, pamoja
na vifaa tiba vya kutosha hivyo kuifanya taasisi yetu kuwa sehemu ya utalii
tiba hapa nchini”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema Naibu Waziri Mkuu kutoka Serikali ya
Watu wa China amefika JKCI kuona jengo ambalo lilijengwa na Serikali hiyo,
kwani msaada walioutoa umekuwa mkubwa na sasa unawasaidia watu kutoka nchi
zaidi ya 20 zilizopo Afrika na mataifa mengine kupata huduma za matibabu ya moyo.
Comments
Post a Comment