Dkt. Batilda Buriani: Changamkieni fursa ya kupima moyo
Na: JKCI
***************************************************************************************************************
Wananchi wa mkoa wa Tabora na mikoa ya jirani wametakiwa
kutumia fursa ya uwepo wa wataalamu wa afya mabingwa wa moyo vizuri kuchunguza
afya za mioyo yao na kupata ushauri wa namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi
Dkt. Batilda Buriani wakati akiwakaribisha wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika ofisi yake kabla ya kuanza kwa kambi maalumu
ya uchunguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan
Outreach Services inayofanyika kwa siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
Tabora – KITETE
Mhe. Batilda alisema huduma hiyo ijulikanayo kama Mhe. Samia
Suluhu Hassan outreach services itasaidia kubadilisha fikra za watu kwani
imehusisha wataalamu wa lishe wanaotoa elimu kuhusu lishe bora na namna ya
kujikinga na magonjwa ya moyo.
“Nimefurahi kuona mmekuja na wataalamu wa lishe kwani katika
mkoa wetu wa Tabora kumekuwa na makundi mawili yanayokinzana katika masuala ya
lishe kwani watu wazima wamekuwa wakila vyakula vya asili na kupunguza kwa
asilimia kubwa vyakula vyenye mafuta mengi lakini upande wa vijana maisha
hayako hivo wao hupendelea kula vyakula vya kisasa na vilivyopikwa na mafuta
mengi”, alisema Mhe. Batilda
Aidha Mhe. Batilda ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE kufikisha
huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa
mkoa wa Tabora na mikoa ya jirani.
“Kupitia kambi maalumu za matibabu ya moyo wanazofanya JKCI
zinatoa ishara ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kuhakikisha kuwa afya za watanzania
zinaboreshwa”, alisema Mhe. Batilda
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
Tabora – KITETE Dkt. Mark Waziri alisema huduma ya uchunguzi na matibabu ya
moyo imekuwa adimu kwa mkoa wa Tabora kwani kumekuwa na changamoto ya
upatikanaji wa madaktari bingwa na wabobezi wanaotibu magonjwa ya moyo.
Dkt. Waziri alisema huduma ya tiba mkoba ya Mhe. Samia Suluhu
Hassan outreach services imesogeza huduma za tiba ya moyo kwa wananchi wa mkoa
wa Tabora ambao wamukuwa wakifuata huduma hizo mkoani Dar es Salaam.
“Kupitia kambi hii wataalamu wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa Tabora – KITETE wataenda kujengewa uwezo ili pale watakapokutana na
wagonjwa wa moyo waweze kuwahudumia kwa wakati”, alisema Dkt. Waziri
Aidha Dkt. Waziri amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza vifaa tiba vya kutosha na
kuruhusu tiba mkoba ya uchunguzi wa matibabu ya moyo kuwafikia wananchi wa
Tabora.
Naye mtafiti wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Loveness Mfanga alisema wataalamu wa afya kutoka JKCI
wamefika mkoani Tabora kwaajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya
moyo kwa wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani.
Loveness ambaye pia ni mratibu wa kambi maalumu ya uchunguzi
na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan outreach services alisema huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi na kuangalia mfumo wa umeme wa moyo.
“Huduma nyingine tutakayotoa ni ile ya kupima magonjwa ya
shinikizo la damu na magonjwa ya sukari mwilini pamoja na kutoa elimu ya lishe
kuwalinda wananchi wasipate magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Loveness
Comments
Post a Comment