JKCI yafanya upasuaji wa moyo kwa watoto saba wa Zambia
Watoto saba wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana nchini Zambia.
Kambi hiyo ya upasuaji ya siku tatu na nusu imefanywa na
wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao
wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo Godwin Sharau ambaye ni daktari
bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) alisema watoto waliofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya matundu,
mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake pamoja na Valvu.
“Tunamshukuru Mungu watoto tuliowafanyia upasuaji wanaendelea
vizuri na kuna ambao wametoka katika chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) na
kwenda wodini kuendelea na matibabu”.
“Tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kuwezesha kufanyika kwa kambi hii ya upasuaji ambayo imesaidia kuokoa maisha ya
watoto hawa saba ambao baada ya kupona wataendelea na maisha kama watoto
wengine”, alisema Dkt. Sharau ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha upasuaji wa
moyo kwa watoto.
Dkt. Sharau alisema katika kambi hiyo walipata nafasi ya
kubadilishana ujuzi wa kazi na wenzao wa hospitali hiyo wa namna ya kufanya upasuaji pamoja na jinsi ya kuwahudumia wagonjwa hao anaamini baada ya miaka ijayo watalamu hao wa Zambia wataweza kusimama na kufanya upasuaji kama JKCI.
Kwa upande wake Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini
Zambia Humphrey Shangarai alisema waliwapokea wataalamu wa JKCI tarehe 18 mwezi
huu ambao walikwenda kufanya uchunguzi na
upasuaji wa moyo kwa watoto
katika Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia.
“Tumefurahi kwani wataalamu wetu wamefanya upasuaji vizuri na
wenyeji wamekiri haijawahi kutokea ushirikiano wa aina hii
katika nchi za Afrika na idadi ya upasuaji waliyoifanya ni kubwa pia
wameamini kazi nzuri inayofanywa na JKCI na kuonesha mfano katika nchi za
Afrika“, alisema Shangarai.
Kwa upande wa wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji katika
kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyopatiwa watoto wao na kusema kuwa
imewapunguzia gharama ya safari ya kuifuata huduma hiyo nje ya Zambia.
“Mwanagu alikuwa na tatizo la kutokupumua vizuri na kukohoa baada
ya kumfanyia vipimo iligundulika anatundu kwenye moyo wakanipa rufaa ya kuja
hapa na wakaniambia anatakiwa kufanyiwa upasuaji, nilipata hofu kwani sikuwa na
uhakika kama hili linaweza kufanyika Zambia.
“Namshukuru Mungu amefanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri,
nawaomba wazazi wenzangu wenye watoto ambao wana matatizo kama haya wasikate
tamaa ipo siku watafanyiwa upasuaji na kupona kama ilivyofanyika kwa mwanangu”,
alishukuru Msopero Gwesi.
“Baada ya vipimo mwanangu aligundulika kuwa na shida ya moyo
na nilikuwa nampeleka hospitali mara kwa mara kwaajili ya matibabu hivi
karibuni alipata shida ya kushindwa kupumua nikapewa rufaa ya kuja hapa baada
ya vipimo nikaambiwa upasuaji hauwezi kufanyika hapa Zambia.
“Wiki iliyopita nikaambiwa kuna wataalamu wanakuja kutoka
Tanzania hivyo mwanangu atafanyiwa upasuaji. Upasuaji umefayika na mwanangu
anaendelea vizuri nashukuru sana kwa huduma hii kwani imetusaidia wanawake
ambao hatuna uwezo wa kusafiri kwenda nje ya nchi kuipata huduma hii hapa
nchini”, alishukuru Achimba Mpundu.
Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH la nchini Israel ndilo lililowezesha kufanyika kwa kambi hiyo ya upasuaji wa moyo kwa watoto nchini Zambia kwa kutoa vifaa tiba na kuwasafirisha wataalamu wa JKCI.
Comments
Post a Comment