Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia
Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
kabla ya wataalamu hao kuanza safari ya kuelekea katika hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia kwaajili ya kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto. Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel ndilo lililowezesha kufanyika kwa kambi hiyo ya upasuaji nchini Zambia.
Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule akizungumza na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo katika uwanja wa ndege wa kimatifa wa Julius Nyerere (JNIA) kabla ya kuanza safari yao ya kwenda katika hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia kwaajili ya kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto. Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel ndilo lililowezesha kufanyika kwa kambi hiyo ya upasuaji nchini Zambia.
Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule akiagana na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya mara baada ya kuwaaga wataalamu wa Taasisi hiyo waliokwenda nchini Zambia kwaajili ya kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto. Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel ndilo lililowezesha kufanyika kwa kambi hiyo ya upasuaji nchini Zambia.
****************************************************************************************************************************************************************************************
Timu ya wataalamu tisa wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo tarehe 17/01/2024 wamesafiri kwenda
nchini Zambia kwa jili ya kutoa huduma ya upasuaji wa moyo kwa watoto katika
Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini humo.
Katika kambi hiyo ya upasuaji ambayo
itafanyika kuanzia tarehe 18/01/2024 hadi tarehe 20/01/2024 wataalamu wa JKCI
kwa kushirikiana na wenzao wa Zambia watafanya upasuaji huo ambao utaenda
sambamba na kuwajengea uwezo na ujuzi wa kazi.
Wataalamu hao ni madaktari bingwa wa watoto, upasuaji
wa moyo, usingizi na wagpnjwa mahututi, maafisa uuguzi wanaohudumia wagonjwa
wanaohitaji uangalizi maalumu na wataalamu wa kuendesha
mashine ya kuusaidia moyo na mapafu kufanya kazi (Heart Lung Machine).
Daktari bingwa mmoja
ametangulia nchini Zambia kwaajili ya kufanya uchunguzi wa moyo kwa watoto ili
kubaini watoto ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya
matibabu.
Kufanyika kwa kambi hii ya upasuaji wa
moyo ni utelelezaji wa mkataba wa miaka mitatu wa makubaliano baina ya JKCI na
Hospitali ya Taifa ya moyo ya nchini Zambia wa kutibu wagonjwa wa moyo pamoja
na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hiyo wa jinsi ya
kuwatibu wagonjwa wa moyo uliosainiwa tarehe 20/04/2023 jijini Dar
es Salaam.
Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a
Child’s Heart – SACH) la nchini Israel ndilo lililowezesha kusainiwa kwa
mkataba huo pamoja na kufanyika kwa kambi hiyo ya upasuaji nchini Zambia.
Mwaka 2015 SACH ilianza ushirikiano
na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwajengea uwezo wataalamu
wa afya kwa kufanya kambi mbalimbali za upasuaji wa moyo kwa watoto na kutoa
mafunzo nchini Israel ambapo hadi sasa JKCI imekuwa na uwezo wa kufanya
upasuaji wa moyo. Kutokana na wataalamu wa JKCI kuwa na ujuzi wa kutosha katika
upasuaji wa moyo kwa watoto SACH imeiunganisha JKCI na nchi ya Zambia ili
waweze kuwasimamia ili nao wapate ujuzi huo na kuweza kufanya upasuaji.
“Afya ya Moyo
Wako ni Jukumu Letu”.
Comments
Post a Comment