Wagonjwa 125,466 watibiwa JKCI Dar Group
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wafanyakazi wa JKCI hospitali ya Dar Group
wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika hivi karibuni katika Hospitali
hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa JKCI Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo
Shemu akielezea mafanikio ya Hospitali hiyo wakati wa kikao cha wafanyakazi
kilichofanyika hivi karibuni katika Hospitali ya JKCI Dar Group iliyopo jijini
Dar es Salaam.
Daktari wa JKCI Hospitali ya Dar Group Mlagwa Yango akielezea
huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wanaofika katika Hospitali hiyo wakati wa
kikao cha wafanyakazi kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Hospitali
hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mteknolojia wa Maabara wa JKCI Hospitali ya Dar Group Elizabeth Manda akitoa pongezi kwa uongozi mzuri unaofanywa na Hospitali hiyo wakati wa kikao cha wafanyakazi wa Hospitali hiyo kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*********************************************************************************************************
Wagonjwa 125,466 waliokuwa na changamoto mbalimbali za kiafya
wamepatiwa matibabu JKCI Hospitali ya Dar Group kuanzia tarehe 1 Januari 2023
hadi 30 Desemba 2023.
Upande wa wagonjwa waliolazwa jumla ya wagonjwa 2,678
walilazwa ambapo watu wazima walikuwa 1,599 huku watoto wakiwa 1,079, na
wagonjwa 1,256 walifanyiwa upasuaji wa aina mbalimbali katika Hospitali hiyo.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi wa JKCI Hospitali
ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu wakati wa kikao cha wafanyakazi wa Hospitali
hiyo na kuongeza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wagonjwa
wanaotibiwa katika Hospitali hiyo kwani sasa hospitali inapokea wagonjwa kati
ya 400 hadi 500 kwa siku tofauti na awali ilipokuwa ikipokea wagonjwa 200 hadi
300 kwa siku.
“Kutokana na utayari wa wafanyakazi wa Hospitali yetu
tumeweza kumudu idadi ya wagonjwa wote wanaofika kwaajili ya matibabu hivyo
kuwapatia huduma bora na kwa wakati”, alisema Dkt. Shemu
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliwapongeza wafanyakazi kwa kazi wanazofanya
na kusema kuwa huduma zinazotolewa zitolewe kwa upendo na kuifanya Hospitali
hiyo kuwa ya mfano Tanzania.
Dkt. Kisenge alisema sambamba na maboresho ya miundombinu ya
Hospitali hiyo yanayofanyika wafanyakazi pia wanatakiwa kuwa mstari wa mbele
kuleta mabadiliko kwa kuwapenda wagonjwa wanaowahudumia kwani upendo usaidia kupunguza
changamoto za kiafya hivyo kujisikia vizuri.
“Uongozi unaendelea kuboresha miundombinu ya Hospitali yetu ambapo
tunaendelea na uboreshaji wa majengo, kuimarisha Idara ya dharura na sasa tumejipanga
kuimarisha chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), pamoja na kununua mashine za
kisasa za kutolea huduma za matibabu”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge amewataka wafanyakazi wa Hospitali hiyo
kuendelea kushiriki katika mafunzo ya jinsi ya kuokoa maisha (Basic Life
Support - BLS) mara kwa mara kwani huduma hiyo ni mtambuka.
“Kuna wafanyakazi 20 tayari wameshapatiwa mafunzo ya kuokoa
maisha (Basic Life Support – BLS), nia yangu ni kuwaona wafanyakazi wote wanashiriki
katika mafunzo haya hasa wale wanaotoa huduma katika wodi za wagonjwa
tunaowahudumia pamoja na madaktari”, alisema Dkt. Kisenge
Naye Mfamasia wa Hospitali hiyo Yusuph Mwakatobe alisema
upande wa Idara ya Famasi huduma zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwani sasa
upatikanaji wa dawa ni wa asilimia 100.
Mwakatobe alisema wagonjwa wanaotembelea duka la dawa
lililopo JKCI Hospitali ya Dar Group wanapata dawa za aina zote kwani kitengo
hicho kimedhamiria kurahisisha huduma za upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa.
“Tumejipanga kuhakikisha katika duka letu la dawa hatupati
changamoto ya upungufu wa dawa ili wagonjwa wanapotibiwa katika Hospitali yetu
wasipate changamoto yakwenda kutafuta dawa sehemu nyingine”, alisema Mwakatobe
Comments
Post a Comment