Waiomba Serikali matibabu ya moyo kufanyika mara kwa mara
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE
Backford John akimpima wingi wa sukari mwilini mwananchi wa mkoa wa Tabora
aliyefika katika Hospitali hiyo kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalumu
ya upimaji na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan tiba
mkoba inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI).
Na: JKCI
************************************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Tabora wameiomba serikali kufikisha
huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo mara kwa mara katika mkoa
huo kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na wananchi mbalimbali waliofika katika kambi
maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia
Suluhu Hassan tiba mkoba inayotolewa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE.
Akizungumza mara baada ya kupata matibabu Samweli Masanja
mkazi wa Tabora alisema amekuwa akisumbuliwa na shinikizo la juu la damu kwa
muda mrefu lililompelekea kupata kiharusi.
“Nimefurahi leo nimeonana na madaktari bingwa wa moyo
waliotumia muda wao kunifanyia uchunguzi wa moyo wangu na kunianzishia dawa, naiomba
Serikali itusaidie wananchi tuwe tunapata huduma kama hizi mara kwa mara”,
alisema Samweli
Samweli alisema hakuwahi kupima moyo lakini kwasababu aliambiwa
tatizo la shinikizo la damu alilonalo linaweza kumsababishia kupata maradhi ya
moyo ndio maana akatumia ujio wa wataalamu wa afya kutoka JKCI kupima moyo
wake.
Mwanaidi Ramadhani ambaye ni mkazi wa Geita aliishukuru
Serikali kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kufikisha huduma za kibingwa
kwa wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani na kuiomba Serikali kuwasambaza
mabingwa wa magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo katika hospitali za Rufaa
za mikoa ili wananchi wapate huduma kirahisi.
“Katika Hospitali zetu za Rufaa tungekuwa na madaktri bingwa
wa moyo ingetusaidia kupata huduma wakati wowote mgonjwa anapohitaji huduma
hivyo kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kucheleweshwa kwa
huduma”, alisema Mwanaidi
Naye mzazi ambaye mtoto wake amezaliwa akiwa na tundu kwenye
moyo Grace Baltazali aliwashukuru wataalamu wa afya wa JKCI kwa kumuondolea
hofu baada ya kumchunguza mtoto wake na kuona tundu alilokuwa nalo mwanaye
limefunga na kubaki kwa kiasi kidogo.
“Nimefurahi mtoto wangu amefanyiwa kipimo na kuonekana tundu
alilokuwa nalo limefunga na kubaki kidogo, nilikuwa naishi kwa hofu kutokana na
tatizo alilokuwa nalo mwanangu”, alisema Grace
Grace alisema mara baada ya kumpata mtoto wake na kuambiwa
kuwa ana matatizo ya moyo alimpeleka mtoto katika Hospitali ya Rufaa Bugando
ambapo alipatiwa matibabu na sasa amefanyiwa uchunguzi tena katika kambi
maalumu inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI.
Comments
Post a Comment