Watu 573 wafikiwa na huduma ya tiba mkoba Tabora
Na: JKCI
*********************************************************************************************************
Watu 573 wamepatiwa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa
ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyofanywa na wataalamu wa afya wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Tabora –KITETE.
Kambi hiyo iliyofanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 15
Januari imemalizika tarehe 19 Januari 2024 mkoani Tabora ambapo jumla ya watu
wazima 531 na watoto 42 walipatiwa matibabu.
Akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa wa Tabora kuhusu kambi hiyo
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Parvina Kazahura alisema wametoa rufaa kwa wagonjwa 84 wakiwemo
watoto na watu wazima kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwani wanahitaji
kupatiwa matibabu zaidi.
Dkt. Parvina alisema upande wa watu wazima wagonjwa wengi
wamekutwa na shikikizo la juu la damu, hitilafu katika misuli ya moyo (Ischemic
heart disease), pamoja na magonjwa ya valvu za moyo.
“Upande wa watoto tumekuta watoto wana magonjwa ya moyo ya
kuzaliwa nayo (Congenital Heart Disease) ikiwemo matundu kwenye moyo na mishipa
ya damu ya moyo iliyoziba au kukaa vibaya ambapo tumetoa rufaa kwa watoto tisa
kufika JKCI kupatiwa matibabu zaidi”,
“Sehemu zote tunazopeleka huduma ya tiba mkoba idadi ya
watoto haiwi kubwa kama ya watu wazima lakini watoto tunaowakuta na shida za
moyo tunabadilisha maisha yao kwasababu kuna shida za moyo ambazo watoto
wanatakiwa wafanyiwe upasuaji kabla ya kufikisha miezi mitatu, nyingine kabla
ya kufikisha mwaka mmoja”, alisema Dkt. Parvina
Dkt. Parvina alisema katika tafiti zilizofanywa kwa wagonjwa
waliotibiwa katika kambi hiyo wagonjwa wengi wameonyesha kununua dawa za presha
katika maduka ya dawa na kutumia bila ya kufika Hospitali kufanyiwa uchunguzi.
“Tafiti pia zimeonyesha asilimia 60 ya watu wazima
waliopatiwa huduma katika kambi hii kuwa na uzito mkubwa, tabia ya kula chakula
cha jioni usiku sana na matumizi ya chuvi ya kuongeza juu ya chakula kuwa
makubwa sana”, alisema Dkt. Parvina
Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi
Dkt. Batilda Buriani amewashukuru wataalamu wa afya wa JKCI na kuwaomba kufikisha
salamu kwa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo kwa kuwafikishia huduma za matibabu ya
moyo.
Mhe. Dkt. Batilda ameomba huduma ya tiba mkoba mkoani Tabora
isiishie hapo bali Taasisi ya Moyo ijipange kurejea tena mkoani humo kwani bado
wananchi wa Tabora wanawahitaji sana.
“Asanteni sana hasa hapo kwa watoto kwani kama mlivosema kama
matibabu ya watoto yatachelewa mtoto anakosa nafasi ya kusaidiwa, kuna dua ya
mzazi mmoja mtoto wake kapatiwa matibabu katika kambi hii anawashukuru sana”,
alisema Mhe. Dkt. Batilda
Aidha Mhe. Dkt. Batilda amewataka wataalamu wa afya wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE kutumia vizuri huduma ya tiba
mtandao kuungana na JKCI kuwasaidia wagonjwa wa moyo watakaoendelea kufika
katika Hospitali hiyo kupata matibabu.
Comments
Post a Comment