Tanzania na China kuendeleza ushirikiano katika matibabu ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi tuzo ya kumshukuru kwa kazi nzuri aliyoifanya
daktari kutoka Jamhuri ya Watu wa China Prof. Zhahg Hailong wakati wa kuwaaga
madaktari watatu kutoka China waliokuwa wanafanya kazi JKCI kwa kipindi cha
miaka miwili hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi cheti cha kuthamini mchango wake daktari kutoka
Jamhuri ya Watu wa China Sun Xufang wakati wa kuwaaga madaktari watatu kutoka
China waliokuwa wanafanya kazi JKCI kwa kipindi cha miaka miwili hivi karibuni
jijini Dar es Salaam.
Madaktari kutoka Jamhuri ya Watu wa China wakimkabidhi
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
zawadi ya kumshukuru kwa kuwa na ushirikiano mzuri kwa kipindi cha miaka miwili
ya utendaji kazi wao katika Taasisi hiyo hivi karibuni wakati wa hafla fupi ya
kuwaaga iliyofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es
Salaam.
Baadhi ya wataalamu wa afya wa Jamhuri ya watu wa China na
wenzao wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia wakati wa hafla
fupi ya kuwaaga madaktari watatu kutoka Jamhuri wa Watu wa China baada ya
kumaliza muda wao wa kutoa huduma katika Taasisi hiyo hivi karibuni jijini Dar
es Salaam.
Na: JKCI
**********************************************************************************************************
Tanzania na China kuendelea kushirikiana katika sekta ya afya
kwa kuwaleta madaktari bingwa kushirikiana na wenzao mabingwa wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kubadilishana uzoefu na kuboresha huduma za kibingwa
nchini.
Ushirikiano huo umeleta tija katika sekta hiyo kwani unatoa
fursa kwa watalamu wa afya kupata ujuzi, pamoja na kuendelea kujenga mahusiano
mazuri baina ya nchi hizo mbili.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati wa
kuwaaga madaktari watatu kutoka nchini China Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliwapongeza madaktari hao kwa
kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watanzania kwa kipindi cha miaka miwili.
Dkt. Kisenge alisema madaktari bingwa kutoka China wamekuwa
sehemu ya wataalamu wa afya wa JKCI kwa kufanya kazi kwa pamoja na kujitoa
kushiriki katika shughuli zote za Taasisi hivo kuondoka kwao kunaacha pengo
kutokana na ushirikiano uliokuwepo baina yao.
“Mmekuwa mkijitoa kushirikiana na wataalamu wetu tangu
mlipofika hapa JKCI, tunawaomba mnavyoondoka msisite kurudi wakati wowote kwani
sasa JKCI ni kama nyumbani kwenu”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Daktari kutoka Jamhuri ya Watu wa China Prof.
Zhahg Hailong ameushukuru uongozi wa JKCI na wafanyakazi kwa kuonyesha uaminifu
kwao kwa kipindi chote walichokuwa wakifanya kazi JKCI.
Zhahg alisema kufanya kazi na wataalamu wa afya wa JKCI
kumewaongezea ujuzi, na uwezo wa kufanya upasuaji wa moyo wa aina mbalimbali
pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
“Sisi tunavyoondoka madaktari wengine kutoka China wanakuja
kuendeleza ushirikiano na Taasisi hii, nimesikia kuna mwenzetu alishafanya kazi
hapa JKCI anarejea naamini na mimi ninavyoondoka leo nitarejea tena hapa kwani
tayari hapa ni nyumbani”, alisema Prof. Zhahg
Naye Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Moyo kwa watu wazima Dkt.
Evaristi Nyawawa alisema madaktari hao kutoka Jamhuri ya Watu wa China wamekuwa
wakifanya kazi mchana na usiku kuhakikisha watanzania wanapata huduma.
Dkt. Nyawawa alisema madaktari hao wameonyesha mfano mzuri wa
kuiwakilisha nchi ya China vizuri kwani wameweza kuacha familia zao kwa kipindi
chote hicho na kufanya kazi kwa amani.
“Tunathamini sana mchango wenu, mmeacha alama hapa JKCI kwa
kufanya kazi kwa upendo na bidii, tutaendelea kushirikiana nanyi kwani lengo
letu wote ni moja la kuokoa maisha ya wagonjwa wa moyo wanaotutegemea”, alisema
Dkt. Nyawawa
Comments
Post a Comment