JKCI kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nchini Congo
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeombwa kufanya kambi maalumu ya matibabu ya moyo nchini Congo pamoja na kuendelea kukuza umoja na ushirikiano katika sekta ya afya na utalii matibabu.
Rai hiyo imetolewa jana na Balozi wa Congo nchini Tanzania Mhe. Jean Pierre Massala alipotembelea Taasisi hiyo leo na kuona fursa zinazopatikana ikiwemo ushirikiana uliojengwa nan chi mbalimbali duniani.
Mhe. Balozi Massala alisema kutokana na ushirikiano uliopo kati ya Congo na Tanzania katika nyanja mbalimbali ni vyema sasa ushirikiano mkubwa ukawekezwa katika sekta ya afya na kutoa fursa kwa wataalamu wa afya kutoka Congo na Tanzania kubadilishana ujuzi.
“Nimeona mabadiliko makubwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma nilipotembelea hapa, hii ni chachu kwetu sisi kama Congo kushirikiana na ndugu zetu wa Tanzania ili tuweze kujifunza namna wanavyofanya kazi, tunaweza kuwaleta madaktari wetu hapa JKCI kubadilishana uzoefu na kujifunza pia wanafunzi wetu wa elimu ya juu kuja kufanya tafiti zao katika Taasisi hii”,
“Nadhani ni wakati sasa JKCI kuweka kambi maalumu ya matibabu ya moyo ama kufungua tawi nchini Congo kama inaweza tupo tayari kununua vifaa tiba vyote vinavyohitajika kwaajili ya matibabu na JKCI ikatupatia wataalamu”, alisema Mhe. Balozi Massala.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Congo Taasisi itazungumza na uongozi wa Wizara ya Afya kuweka mikakati ya kurahisisha mashirikiano hasa katita upande wa matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Tunaweza kukaa na Serekali zetu kupitia Wizara ya Afya na kuangalia ni njia gani nzuri tunaweza kuifanya ili tuweze kushirikiana kwani kumekuwa na mwendelezo mzuri wakutembeleana na kubadilishana ujuzi kati yetu na wenzetu wa Congo.
Aidha Dkt. Kisenge amewakaribisha raia wa Congo na watu kutoka mataifa mbalimbali Barani Afrika na nje ya Afrika kufika JKCI kutibiwa kwani huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa asilimia tisini zinapatikana JKCI.
“Nawakaribisha sana ndugu zangu kutoka Congo na wote wanaotoka ndani na nje ya Afrika kwani huduma nyingi za matibabu ya moyo ambazo zilikuwa zinafanyika nje ya bara letu la Afrika sasa zinafanyika tena kwa bei nafuu na kwa ubora wa hali ya juu hapa JKCI, hali inayoweza kumsaidia mwananchi wa hali ya kawaida kupata huduma kwa urahisi na haraka”, alisema Dkt. Kisenge
Ugeni Balozi wa Congo nchini Tanzania Mhe. Jean Pierre Massala katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete umefanyika ikiwa ni maandalizi ya kupokea
madaktari kutoka nchini humo kutembelea JKCI mwanzoni mwa wiki ijayo.
Comments
Post a Comment