Wanafunzi 965 wapimwa moyo Dar es Salaam
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya
Shandong Provincial iliyopo nchini China ambaye pia anafanya kazi Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Zhao Lijian akimpima kipimo cha kuangalia
jinsi moyo unavyofanya kazi mwanafunzi wa Shule ya Msingi Msasani wakati wa
kambi maalumu ya siku mbili iliyomalizika leo jijini Dar es Salaam. Jumla ya
wanafunzi 965 wa Shule za Msingi Hananasif na Msasani wamefanyiwa kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi.
Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Theophylly Ludovick akizungumza na mzazi ambaye mtoto wake amefanyiwa kipimo cha moyo wakati wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wanafunzi wa Shule ya Misingi Msasani leo jijini Dar es salaam. Jumla ya wanafunzi 965 wa Shule za Msingi Hananasif na Msasani wamefanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi.
Daktari kutoka Hospitali ya YUNNAN FUWAI iliyopo nchini China
Zhang Shuyue akisikiliza mapigo ya moyo ya mwanafunzi wa Shule ya Msingi
Msasani wakati wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wanafunzi wa Shule ya
Misingi Msasani leo jijini Dar es salaam. Jumla ya wanafunzi 965 wa Shule za
Msingi Hananasif na Msasani wamefanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi.
Dakatari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya
YUNNAN FUWAI iliyopo nchini China Duo Lin akizungumza na Afisa Utafiti na
Mafunzo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba pamoja na Mratibu
wa Tiba na magonjwa yasiyoambukiza Wilaya ya Kinondoni Dkt. Omary Mwangaza wakati wa uchunguzi wa
magonjwa ya moyo kwa wanafunzi wa Shule ya Misingi Msasani leo jijini Dar es
salaam. Jumla ya wanafunzi 965 wa Shule za Msingi Hananasif na Msasani
wamefanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi.
Na: Stella Gama
*********************************************************************************************************
Wanafunzi 965 wa shule za msingi za Hananasif na Msasani za
jijini Dar es Salaam wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kupimwa
kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO).
Wanafunzi hao wamefanyiwa kipimo hicho wakati wa kambi
maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ya siku mbili iliyofanywa na madaktari
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwakushirikiana na wenzao kutoka
Hospitali ya YUNNAN FUWAI iliyopo nchini China.
Akizungumza na waandishi
wa habari wakati wa kuhitimisha kambi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa niaba
ya Mkurungenzi Mtendaji wa JKCI Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Theophylly Ludovick alisema watoto 743 wa shule ya msingi Hananasif na
watoto 222 wa shule ya msingi Msasani wamefanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi.
Dkt. Theophylly alisema upimaji huo uliofadhiliwa na Shirika
la Afya Duniani (WHO) umehusisha uchunguzi wa viashiria vya matatizo ya moyo
kugundua kama kuna matatizo ya moyo ambayo hayajawahi kugundulika.
“Katika Shule ya Msingi Hananasif tumekuta watoto watatu wana
matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambapo mmoja wao anahitaji upasuaji wa kuziba
tundu lililopo katika moyo wake, mtoto huyo ameshafika katika Taasisi yetu tumemlaza
na kesho atafanyiwa upasuaji wa moyo”,
“Kwa hapa shule ya Msingi Msasani pia tumewakuta watoto
watatu wana matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo, watoto hawa tutawapanga katika ratiba
zetu kwaajili ya kuwafanyia upasuaji wa kuziba matundu yaliyopo katika mioyo
yao”, alisema Dkt. Theophylly
Dkt. Theophylly alisema Taasisi kwakushirikiana na Hospitali ya YUNNAN FUWAI iliyopo nchini China watatoa huduma za matibabu kwa watoto sita waliogundulika kuwa na matatizo ya moyo bila gharama.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka
Hospitali ya Shandong Provincial iliyopo nchini China ambaye pia anafanya
kazi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zhao Lijian aliwapongeza
wazazi kwa kuitikia wito wa kuwafikisha watoto katika kambi hiyo kwaajili ya
kufanyiwa uchunguzi.
Dkt. Zhao alisema kambi
hiyo imefanyika kama sehemu ya mafanikio ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya
Tanzania na China katika sekta ya afya kuendelea kutoa huduma za afya hasa kwa
watoto.
“Huu ni mwanzo wa
progamu hii ya kuwafuata watoto mashuleni kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya
moyo, zoezi hili litaendelea tena kwa awamu nyingine ili tuweze kuwagundua
watoto wenye matatizo ya moyo mapema na kuwapatia matibabu kwa wakati”, alisema
Dkt. Zhao
Kwa upande wa wazazi ambao
watoto wao walipata huduma hiyo walizishukuru Serikali za Tanzania na China kwa
kuwa na wazo la kuwapima wanafunzi waliopo mashuleni na kuomba zoezi hilo liendelee
na kwa watoto wengine.
Mzazi wa mtoto aliyegundulika kuwa na tundu kwenye moyo Iptsam
Anwary alisema tangu ajifungue mtoto huyo hajawahi kuwa na dalili zozote
zinazoendana na magonjwa ya moyo hadi jana alipopimwa akiwa shuleni Hananasif.
“Naishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na
Serikali ya watu wa China kuanzisha progamu hii ya kuwafanyia uchunguzi wa
magonjwa ya moyo watoto waliopo mashuleni kwani bila hivyo nisigejua kama mtoto
wangu ana tundu kwenye moyo”,
“Sikuwa na wazo la kwenda kumpima mtoto wangu moyo wala
sikuwahi kuhisi kama mtoto wangu ana tatizo la moyo lakini baada ya kufanyiwa
kipimo na kukutwa na tatizo hili daktari kaniambia tatizo alilonalo linaweza
kutibika”, alisema Iptsam
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani Edward Mollel
ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuifikiria jamii na
kuiwezesha kupata huduma muhimu za uchunguzi wa afya.
Mollel alisema jamii bado haijapata elimu ya kutosha kuhusu
uchunguzi wa afya na hiyo imejidhihirisha kwa watoto wengi wa shule ya msingi
Msasani kufanyiwa kipimo cha kuchunguza moyo unavyofanya kazi kwa mara ya
kwanza.
“Nilikuwa najua tatizo la moyo kwa watoto sio kubwa lakini
leo nimethibitisha kupitia watoto wetu waliopimwa hapa kwani watoto hawa uwezi
kuwafikiria kama wana matatizo ya moyo”, alisema Mollel
Comments
Post a Comment