Mhe. Mhagama: Hakikisheni huduma za matibabu ya kibingwa zinawafikia wananchi wa hali ya chini



 Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ndogo za wizara  hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuapishwa kuwa waziri wa wizara ya Afya.

Naibu Waziri wa Afya  Mhe. Godwin Mollel akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo wakati wanasubiri kumpokea Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama aliyeapishwa  Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa waziri wa wizara ya Afya.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya  Bw. Ismail Rumatila akiwasalimia wafanyakazi wa wizara hiyo katika ofisi ndogo za wizara  zilizopo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)  Dkt. Irene Isaka akiwasalimia wafanyazi wa wizara ya Afya wakati wa mkutano na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Jenista Muhagama uliofanyika  katika ofisi ndogo za wizara   zilizopo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama akimsalimia Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda alipowasili  katika ofisi ndogo za wizara  hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuapishwa kuwa waziri wa wizara ya Afya. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. John Jingu.


Baadhi ya wafanyakazi wa wizara ya Afya wakimsikiliza  Waziri wa wizara hiyo Mhe. Jenista Muhagama wakati akizungumza nao katika ofisi ndogo za wizara zilizopo jijini Dar es Salaam.

*********************************************************************************************************************************************************************************************************************************

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewataka wafanyakazi wa wizara hiyo kuhakikisha huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa mbalimbali zinawafikia wananchi wa hali ya chini bila ya kuwa na vikwazo vyovyote.

Mhe. Waziri Muhagama alitoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wafanyakazi hao katika ofisi ndogo za wizara ya Afya mara baada ya kuapishwa kuwa waziri wa wizara hiyo.

Mhe. Mhagama alisema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vya kisasa, kujenga majengo ya kisasa, kusomesha wataalamu na kuboresha maslahi ya wafanyakazi jukumu lililobaki kwao ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu.

“Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali yetu asilimia 95 ya huduma za matibabu ya kibingwa zinapatikana hapa nchini ni jukumu lenu kuhakikisha uwekezaji huu uliofanywa na Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unawafikia wananchi wengi zaidi waliopo ndani na nje ya nchi yetu”.

“Kuna wakati mgonjwa anahitaji kupata maneno mazuri ya faraja na akipata mane no hayo kwa asilimia kubwa anakuwa na matumaini ya kupona ugonjwa wake, tunahitaji kuwasaidia watanzania kwani sisi tumebeba usalama wa afya za watanzani hivyo basi tutimize wajibu wetu wa kazi kwa kufuata sera na miongozo iliyopo”, alisema Mhe. Mhagama.

Akizungumzia kuhusu utalii wa matibabu Mhe. Mhagama alisema miaka michache iliyopita hakukuwa na uwekezaji wa kutosha katika sekta ya afya kutokana na uwekezaji uliofanyika wananchi kutoka nchi za jirani wanakuja kutibiwa hapa nchini.

“Mimi na viongozi wenzangu tutatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wizara yetu inakwenda mbele zaidi na kutoa huduma bora kwa watanzania na wasio watanzania ambao wanakuja katika nchi yetu kupata huduma za matibabu”, alisema Mhe. Mhagama.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya  Mhe. Godwin Mollel alimpongeza Mhe. Waziri Mhagama kwa kuteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo na kusema kuwa uzoefu aliokuwa nao utasaidia kuifikisha wizara hiyo mbali zaidi.

“Katika wizara yetu tunawataalamu wazuri ambao wamebobea katika fani mbalimbali za utoaji wa huduma za afya ili kuhakikisha afya za watanzania zinakuwa salama”, alisema Dkt. Mollel.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. John Jingu alisema kazi kubwa ya wizara ya Afya  ni  kuzuia magonjwa, kutibu na kupambana na magonjwa yanayoibuka pamoja na kutekeleza majukumu mengine yaliyopo ya kuhakikisha usalama wa afya unakuwepo nchini.

“Katika wizara yetu tuna hospitali ya taifa moja, taasisi maalumu za afya tano, taasisi za afya  tano,  hospitali za kanda saba,  hospitali za rufaa za mikoa 28, vyuo vya afya 42 na tuna wafanyakazi wa kutosha hivyo basi hatutawaangusha katika utendaji kazi za kuwahudumia watanzania ”, alisema Dkt. Jingu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wafanyakazi hao Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. alisema kwa wao waliosoma miaka ya nyuma matibabu mengi walikuwa wanayasoma katika vitabu na hawakuweza kuyatoa kwa wagonjwa hiyo ni kutokana na kutokuwa na vifaa vya kutolea huduma hizo.

“Ni jambo la kujivunia kwani sasa hivi huduma zote za matibabu zinatolewa hapa nchini hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika, tunakuahidi Mhe. Waziri tutatoa huduma bora kwa wagonjwa ili watanzania wafurahie matunda ya mafaniko ya wizara ya afya”, alisema Dkt. Julius Mwaiselage.

Mhe. Waziri Muhagama aliambatana na viongozi wapya wa wizara hiyo ambao Naibu Katibu Mkuu wa Afya  Bw. Ismail Rumatila na  Dkt. Irene Isaka Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024