JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Izina tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 tuzo hiyo ameitoa wakati akifungua kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa Taasisi za umma kinachofanyika jijini Arusha. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa JKCI Dkt. Angela Muhozya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Izina na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya kabla ya kuwakabidhi tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024. Tuzo hiyo imetolewa leo jiji Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa Taasisi za umma.
Taasisi ya Moyo Jakaya
kikwete (JKCI) imepokea tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee
kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka
2023/2024.
Tuzo hiyo imetolewa leo na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua
kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa Taasisi za umma kilichoandaliwa na ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa Arusha (AICC).
Tuzo hiyo imeielezea JKCI kwenda hatua moja zaidi mbele katika
kufanikisha malengo ya taasisi na kusaidia taasisi zingine nazo ziweze kufikia
hatua ambayo taasisi hiyo imefikia katika utoaji wa matibabu ya moyo.
Akielezea tuzo hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na
Msemaji Mkuu wa Serikali Thobias Makoba alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja
uliopita JKCI ilitoa huduma za upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua kwa wagonjwa
654 ambapo kwa miaka ya nyuma wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kupata
matibabu.
“Kupitia upasuaji huo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
imeokoa fedha za kitanzania zaidi ya shilingi bilioni 9.8 kutokana na huduma
hii kupatikana hapa nchini”, alisema Makoba.
Makoba alisema JKCI pia imezijengea uwezo nchi za jirani
katika kutoa huduma na matibabu ya magonjwa ya moyo ikiwemo Hospitali ya Moyo
ya Zambia, Hospitali ya King Faisal ya Rwanda, Hospitali ya Queen Elizabeth ya Malawi
pamoja na hospitali mbalimbali za hapa nchini.
Akizungumza kuhusu tuzo hiyo Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya Taasisi hiyo Asha Izina aliishukuru ofisi ya Msajili wa Hazina kwa
kutambua na kuthamini huduma zinazotolewa na JKCI na kusema kuwa watahakikisha
wananchi wengi wanafaidika na uwepo kwa taasisi hiyo.
“Tutaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuhakikisha tunawafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi ili nao waweze kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na kwa wataalamu wa afya tutaendelea kuwajengea uwezo ili waweze kuwatambua na kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya moyo”, alisema Asha.
Comments
Post a Comment