JKCI yaandaa mkutano wa kimataifa wa moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wadau leo wakati wa uzinduzi wa mkutano wa
tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo (Cardiotan Africa) utakaofanyika mwezi
Aprili 2025 katika Hoteli ya Sea Cliff iliyopo mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa tatu wa
kimataifa wa magonjwa ya moyo (Cardiotan Africa) utakaofanyika mwezi Aprili 2025 katika Hoteli ya Sea Cliff
iliyopo mjini Zanzibar Dkt.
Delilah Kimambo akielezea malengo ya mkutano huo leo wakati wa uzinduzi wa
mkutano huo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wafanyakazi na wadau wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wakifuatilia wakati wa uzinduzi wa mkutano wa tatu wa kimataifa
wa magonjwa ya moyo (Cardiotan Africa) uliokuwa ukifanyika leo katika ukumbi wa
Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Na: Stella Gama
*************************************************************************************************************************************************
Zaidi
ya washiriki 1000 kutoka nchi 40 wanatarajiwa kushiriki katika mkutano wa tatu
wa kimataifa wa magonjwa ya moyo unaoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI).
Mkutano
huo utafanyika mwezi Aprili mwakani katika Hoteli ya Sea cliff & Spa,
visiwani Zanzibar.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kutambulisha mkutano
huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge alisema kupitia mkutano huo wataalamu wa afya watafundishwa kutumia
teknolojia mpya ya kutibu magonjwa ya moyo kwa kutumia njia za kisasa kama vile
akili mnemba.
“Mkutano
wa Cardiotan 2025 utaelekeza namna ya kutibu matatizo ya magonjwa ya moyo,
madaktari kutoka nchi za Afrika ni wakati wetu sasa kupitia mkutano huu
kujifunza mbinu mbalimbali za kutibu wagonjwa wa moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa maandalizi ya mkutano huo Dkt. Delilah Kimambo
alisema lengo kubwa la mkutano huo ni pamoja na kukusanya wataalamu wa afya ambao
wanamchango mkubwa katika sekta ya matibabu ya moyo kujadili mada zitakazohusiana
na kinga, lishe na matibabu ya moyo.
Dkt.
Delilah alisema kupitia mkutano huo kwa mara ya kwanza JKCI inaenda
kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar kuwafundisha watu
ambao sio wataalamu wa afya jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa anayehitaji
huduma ya kwanza na kuwaleta watu pamoja.
“Kupitia
mkutano wetu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo tunaenda kujadili na kuona jinsi
gani tunaweza kuisaidia Afrika kwa njia rahisi kabisa ili matibabu ya moyo
yaweze kupatikana kwa urahisi”, alisema Dkt. Delilah.
Naye
Kaimu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Aziwa Issa Makame alisema
kupitia mkutano huo utaenda kuisaidia Zanzibar kuongeza idadi ya watalii wanaoingia
nchini na wale wanaoongoza watalii wataweza kupatiwa mafunzo ambayo yataweza
kuwasaidia wageni wao pale wanapopata changamoto za kiafya.
Aziwa
aliishukuru JKCI kwa kuwa na wazo la kupeleka mkutano huo Zanzibar na kuichagua
sekta ya utalii kuwa miongoni mwa sekta zitakazopatiwa mafunzo kwani mafunzo
hayo ni muhimu kuifikia jamii.
“Nachukua
nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa utalii kujiandikisha kwaajili ya kupatiwa
mafunzo ya namna ya kumsaidia mtu anayehitaji huduma ya kwanza ili kulinda afya
za watalii wetu”, alisema Aziwa.
Mkutano
wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wa
mwaka 2025 wenye kaulimbiu “Kuimarisha
huduma za moyo barani Afrika kupitia jitihada za pamoja” utakuwa mkutano wa
tatu tangu kuanzishwa mkutano huo mwaka 2023 ambapo mkutano wa pili wa mwaka 2024
ulikuwa wa mafanikio makubwa ambayo uliwakutanisha wataalamu wa afya zaidi ya
500 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Comments
Post a Comment