Watu 558 wafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Mlagwa Yango akimpima kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mwananchi
aliyepatiwa huduma katika kambi maalumu ya siku nne ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanyika katika Zahanati ya Bungoni kata ya Ilala
na kumalizika jana jijini Dar es Salaam. Kambi hiyo imefanywa na Hospitali ya
JKCI Dar Group kwakushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Ilala Mhe. Mussa
Azzan Zungu.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya
Dar Group Yona Jeremia akimshauri mwananchi wa Ilala baada ya kufanya vipimo
vya magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku nne ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanyika katika Zahanati ya Bungoni kata ya Ilala
na kumalizika jana jijini Dar es Salaam. Kambi hiyo imefanywa na Hospitali ya
JKCI Dar Group kwakushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Ilala Mhe. Mussa
Azzan Zungu.
Afisa Uuguzi kutoka Mpango wa Taifa wa damu salama akimtoa
damu mwananchi aliyejitokeza kuchangia damu wakati wa kambi maalumu ya siku nne
ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanyika katika
Zahanati ya Bungoni kata ya Ilala na kumalizika jana jijini Dar es Salaam.
Kambi hiyo imefanywa na Hospitali ya JKCI Dar Group kwakushirikiana na Ofisi ya
Mbunge wa jimbo la Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu.
Na: JKCI
*************************************************************************************************************************
Julma ya watu 558 wa Wilaya ya Ilala na vitongoji vyake wamefanyiwa
uchunguzi na wengine kupewa matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu
ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba.
Kambi hiyo maalumu ya siku nne iliyomalizika jana imefanywa
na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Zahanati ya
Bungoni Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Ilala
Mhe. Mussa Azzan Zungu.
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo Daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali
ya Dar Group Eva Wakuganda alisema asilimia 67 ya watu wote waliofanyiwa vipimo
vya moyo wamekutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la juu la
damu, moyo kutanuka, moyo kushindwa kufanya kazi na kuziba kwa mishipa ya damu.
“Katika kambi hii pia
tumeweza kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa watoto 75 ambapo kati yao
watoto 12 tuliwagundua kuwa na matatizo ya matundu kwenye moyo”, alisema Dkt.
Eva
Dkt. Eva alisema katika kambi hiyo watu 215 walipewa rufaa
kufika JKCI kwaajili ya kuendelea na matibabu zaidi na wale waliohitaji kutumia
dawa walipewa dawa bila gharama.
“Sambamba na upimaji wa magonjwa ya moyo katika kambi hii
watu 400 wamepimwa kipimo cha homa ya ini na kupewa chanjo hiyo bila gharama”,
alisema Dkt. Eva
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Bungoni Dkt.
Ester Akili alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu kwa
kuwafikishia huduma za kibingwa za matibabu ya moyo wananchi wa Ilala bila
gharama.
Dkt. Ester alisema mwitikio wa watu kujitokeza kupima moyo
umekuwa mkubwa tofauti na walivyotarajia kwani watu kutoka Wilaya ya Ilala na
wilaya za jirani waliweza kujitokeza kufanya uchunguzi wa afya.
Tunaishukuru sana JKCI kwa kutuletea wataalamu hawa mabingwa
wa moyo, kupitia kambi hii watu wameweza kukitafuta kituo chetu mahali kilipo
na kufika kwani kituo hiki ni kipya na watu wengi walikuwa hawakifahamu.
“Zahanati ya Bungoni ni mypa tangu ianze kutoa huduma ina
miezi saba sasa, tunashukuru kupitia kambi hii zahanati yetu imetambulika
katika jamii ya watu kutoka maeneo mbalimbali”, alisema Dkt. Ester
Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Willium Kiwazo
alisema alikutwa na shida ya moyo miaka mitano iliyopita lakini baada ya kupata
matibabu na kuendelea vizuri hakuweza kurudi tena hospitali kuangalia maendeleo
yake.
Willium alisema kushindwa kwake kuendelea kufuatilia matibabu
kumetokana na bima yake ya afya kuisha muda wake miaka miwili iliyopita na
kushindwa kukata bima nyingine.
“Nilifanyiwa uchunguzi JKCI miaka mitano iliyopita na kukutwa
na tatizo la moyo ambalo nilipewa dawa lakini baada ya hapo sijarudi tena
hospitali kutokana na kadi yangu ya bima kuisha muda wake na kushindwa kukata
bima nyingine”, alisema Willium
Willium alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupima afya zao
pale fursa za upimaji wa magonjwa mbalimbali zinapojitokeza kupunguza gharama
ya kuzifuata mahali zilipo.
Comments
Post a Comment