JKCI yaimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani kufanya upasuaji changamani wa moyo
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la CardioStart International la nchini Marekani wakimfanyia upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu mgonjwa ambaye mishipa yake imeziba wakati wa kambi maalumu ya siku tano inayofanywa na wataalamu hao katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa kuendesha mashine
inayosaidia moyo na mapafu kufanya kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Sophia Lukonge akiendesha mashine hiyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano
ya upasuaji wa moyo inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao
kutoka Shirika
la CardioStart International la nchini Marekani.
Na: JKCI
*******************************************************************************************************
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) waendelea kuongezewa ujuzi na uzoefu katika kufanya
upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo yanayohitaji utaalamu
zaidi.
Ujuzi huo umeongezwa kupitia
kambi maalumu ya siku tano ya upasuaji wa moyo inayofanywa na wataalamu wa JKCI
kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la CardioStart International la
nchini Marekani.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hii daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Nely Kahamba alisema wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ni
wale wenye matatizo ya mishipa ya damu iliyotanuka, magonjwa ya valvu za moyo
na matatizo ya mishipa inayosafirisha damu kwenda kwenye moyo.
“Kupitia kambi hii tumeweza
kubadilishana ujuzi na uzoefu katika kutoa huduma hizi bingwa za upasuaji wa
moyo na kuiongezea utaalamu Taasisi yetu katika kutoa huduma bingwa za matibabu
ya moyo hapa nchini”,
“Katika kambi hii tumefanya
upasuaji wa moyo wa aina mbalimbali ikiwemo kuunganisha mshipa wa damu ili
kupitisha damu pembeni ya mshipa wa moyo ulioziba, kukarabati mshipa mkuu wa
damu pamoja na kubadilisha valvu za moyo”, alisema Dkt. Nely.
Kwa upande wake Daktari Bingwa
wa Usingizi kutoka Shirika la CardioStart International la nchini Marekani Dkt.
Doug Ribar alisema kambi hiyo imekuwa na mafanikio kutokana na ushirikiano
mzuri kati ya wataalamu hao katika kutoa huduma kwa wagonjwa.
Alisema ushirikiano huo
umewezesha wataalamu wa pande zote mbili kujifunza kutoka kwa wenzao, ikiwemo
namna ya kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi katika kutoa huduma kwa
wagonjwa.
“Huu umekuwa ushirikiano mzuri
wa timu zote mbili, tumefanya kazi kubwa ya kuhakikisha tunawatibu wagonjwa
waliokuwa wanahitaji huduma zetu lakini pia tumepata muda wa kujifunza kwa
pamoja”, alisema Dkt. Ribar.
Ujuzi uliopatikana kupitia kambi
hiyo imewafikia wataalamu wote walioshiriki kutoa huduma wakiwemo madaktari
bingwa wa upasuaji wa moyo, madaktari bingwa wa usingizi, wauguzi na wataalamu
wa kuendesha mashine ya moyo na mapafu ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja
katika kutoa huduma kwa wagonjwa.


Comments
Post a Comment