Watu zaidi ya 200 wapimwa moyo Geita, 17 wapewa rufaa
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingido akigawa vipeperushi vya lishe kwa wakazi
wa Geita waliofika katika kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo
iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita (GRRH) ikiwa ni
sehemu ya maandalizi ya kuelekea hafla ya chakula cha hisani kuchangisha fedha
za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yatimuni Mushi akimpima mkazi wa geita kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) wakati wa
kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo iliyokuwa ikifanyika katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita (GRRH) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea
hafla ya chakula cha hisani kuchangisha fedha za matibabu ya watoto wenye
magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Daktari bingwa wa watoto wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Winnie Masakuya akimpima mtoto kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) wakati wa kambi
maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Geita (GRRH) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea
hafla ya chakula cha hisani kuchangisha fedha za matibabu ya watoto wenye
magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kliniki ya Kawe Johnstone Kayandabila
akimsomea majibu mwananchi wa Geita aliyefika katika kambi maalumu ya uchunguzi
wa magonjwa ya moyo iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Geita (GRRH) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea hafla ya chakula cha
hisani kuchangisha fedha za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo
wanaotibiwa JKCI.
Na JKCI
****************************************************************************************************************
Watu zaidi ya 200 wafanyiwa uchunguzi
wa magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya siku tano iliyokuwa ikifanyika
mkoni Geita kuelekea hafla ya chakula cha hisani kuchangisha fedha za matibabu
ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo maalumu imefanyika katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita (GRRH) ambapo watu 17 walikutwa na matatizo
ya moyo na kupewa rufaa kwenda Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam kwaajili
ya matibabu zaidi.
Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa
afya baadhi ya watu walibainika kuwa na changamoto ya shinikizo la juu la damu
bila kujijua huku wengine wakiwa na uzito uliopitiliza unaoweza kuleta madhara
ya kiafya.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha
kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Kliniki ya Kawe Johnstone Kayandabila alisema wananchi wanatakiwa
kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi mara kwa mara na kudhibiti uzito wa
mwili ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza yanayoweza
kuathiri afya ya moyo.
“Watu 17 tuliowapa rufaa kufika
katika Taasisi yetu kwaajili ya uchunguzi zaidi wengi wao wanahitaji kufungiwa
mashine ya kurekodi mwenendo wa moyo kwa saa 24, wengine wanahitaji kuzibuliwa
mishipa ya moyo iliyoziba na wengine wanahitaji upasuaji mkubwa wa moyo
kurekebisha milango ya moyo (valves) iliyoathirika”, alisema Dkt. Johnstone.
Dkt. Johnstone alieleza kuwa
uchunguzi uliofanyika umeonesha wagonjwa wengi kuwa na tatizo la shinikizo la
juu la damu hali inayohusishwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mtindo wa
maisha ikiwemo ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi ya mwili.
“Watu wengi wameacha kutembea au
kufanya mazoezi kutokana na mabadiliko ya mfumo wa usafiri na maisha kwa ujumla
hali hii inachangia kuongezeka kwa uzito na hatimaye kuongeza hatari ya kupata
shinikizo la juu la damu, kuziba kwa mishipa ya damu pamoja na ugonjwa wa
kisukari”, alisema Dkt. Johnstone.
Kwa upande wake Daktari wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita (GRRH) Mohamed Muyeka alisema kambi hiyo
imekuwa na manufaa kwa wananchi na wataalamu wa GRRH kutokana na kupata maarifa
na uwezo wa kuwatambua wagonjwa wa moyo.
“Wataalamu wa GRRH wameshirikiana
na wataalamu wa JKCI kutoa huduma katika kambi hii, hivyo kupata maarifa mapya
na uwezo wa kuwatambua wagonjwa wa moyo na namna ya kuwatibu”, alisema Dkt. Muyeka.
Akizungumzia namna alivyonufaika
na kambi hiyo mkazi wa Geita Rwenzaku Jackson alisema alifika hospitalini hapo
baada ya kupata taarifa za uwepo wa wataalamu kutoka JKCI waliokuwa wakitoa
huduma za uchunguzi wa afya ya moyo.
“Tumepata huduma kama
tulivyotangaziwa, madaktari wametuhudumia vizuri na nashukuru Mungu tumepata
majibu tuliyokuwa tunahitaji kupitia vipimo tulivyofanyiwa”, alisema Rwenzaku.
Naye mkazi wa Katoro mkoani Geita
Ngenzi Mbai alisema elimu ya lishe iliyotolewa wakati wa kambi hiyo imemsaidia
kuelewa umuhimu wa kula chakula kwa kiasi na kuchagua vyakula vinavyofaa kwa
afya ya mwili.
“Tumepata semina nzuri sana
kuhusu lishe kwa kweli tulikuwa tunakula vyakula bila kuzingatia umuhimu wake
lakini kupitia elimu tuliyopewa tumeelewa kuwa tunapaswa kula chakula kwa kiasi
na si kula kupita kiasi”, alisema Mbai.
Kambi hiyo ya uchunguzi wa
magonjwa ya moyo ni sehemu ya juhudi za Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwakushirikiana
na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Geita kusogeza huduma za kibingwa karibu na
wananchi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea hafla ya chakula cha hisani
kuchangisha fedha za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa na JKCI.





Comments
Post a Comment