Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB
Abdulmajid Nsekela akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu mbio za CRDB Bank Marathon ambazo
lengo lake ni kuchangisha fedha za
matibabu ya moyo kwa watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo
wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Benki ya CRDB imeandaa mbio
za CRDB Bank Marathon kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu ya moyo kwa
watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wa kuchangia gharama za
matibabu wanaotibiwa katika Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia
Hassan Suluhu anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi katika mbio hizo zitakazofanyika tarehe 16/08/2020 kuanzia saa 12
asubuhi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika
mkutano wa waandishi wa Habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema
lengo la kuandaa mbio hizo ni kuleta tabasamu kwa watoto wenye matatizo ya moyo
pamoja na familia zao.
Nsekela alisema licha ya
kuandaa mbio hizo Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto
wenye matatizo ya moyo ambao wanatoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa
kuchangia gharama za matibabu wanapata matibabu kama watoto wengine.
“Hadi sasa Benki yetu
imechangia kiasi cha shilingi milioni 100 fedha ambazo
zilitumika kulipa gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto 50”.
“Kiasi cha fedha kitakachopatikana
katika mbio hizi kitaenda kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete”, alisema Nsekela.
Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema kila mshiriki wa mbio hizo
ambazo zitafanyika Tanzania nzima mahali ambako benki hiyo ipo (Virtual
Marathon) atachangia kiasi cha shilingi
30,000/= na kutakuwa na mbio za kilomita 5, 10 na 21 pamoja na mbio za
baiskeli.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi aliipongeza Benki ya CRDB kwa kutambua haki ya mtoto ya kupata matibabu na
kuamua kuwasaidia watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Prof. Janabi alisema
asilimia kubwa ya watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wanasumbuliwa na
magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo
kutokuwa katika mfumo wa kawaida.
Naye Meneja wa kanda ya
Mashariki wa mpango wa Taifa wa damu salama Dkt. Kokuhabwa Mkurasi aliwaomba
wananchi wenye afya njema kujitokeza kwa wingi kuchangia damu siku hiyo ya CRDB
Bank Marathon.
Dkt. Kokuhabwa alisema
wataalamu kutoka katika ofisi yake watakuwepo kuanzia asubuhi hadi mwisho wa
mbio hizo ili wananchi waweze kuchangia damu kwani wanahitaji damu za kutosha.
Sambamba na mbio hizo ambazo
zitafanyika katika uwanja wa Farasi
Oster bay jijini Dar es Salaam kutakuwepo na huduma za ushauri na upimaji
wa magonjwa ya moyo, homa ya ini pamoja na uchangiaji wa damu.
|
Comments
Post a Comment