Wananchi wameshauriwa kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara na kuwa na bima ya afya ambayo itawasaidia pindi watakapouguwa
Wananchi wameshauriwa
kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara kwa kufanya hivyo watatambua
kama wana maradhi au la na kama wana maradhi wataweza kupata huduma za matibabu
kwa wakati.
Pia wameombwa kuwa na
bima ya afya ambazo zitawasaidia kupata matibabu pindi watakapouguwa kwani
maradhi huja muda wowote, wakati wowote na mahala popote bila ya kupiga hodi.
Rai hiyo imetolewa hivi
karibuni na aliyekuwa Mbunge wa Nzega Mhe. Lucas Lumambo Selelii aliyefanyiwa
upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na kupandikiza mshipa wa damu kwenye moyo
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza kwa furaha na
mwandishi wa habari hii Mhe. Selelii alisema huduma za matibabu ya moyo ya
kibingwa ambayo hapo awali yalikuwa yakipatikana nje ya nchi sasa yanapatikana
hapa nchini kwa kiwango cha juu kupitia madaktari wabobezi na wataalam wa
upasuaji wa moyo.
“Matibabu niliyoyapata
pamoja na mengine yanatotolewa katika Taasisi hii yanatokana
na jitihada zilizofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kuwekeza vifaa tiba vya matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo ili
kuwawezesha wananchi wa matabaka yote kupata huduma hapa nchini.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu, upasuaji mkubwa wa
moyo wa kuvuna mshipa wa damu kutoka kwenye mguu na kuupandikiza katika moyo
ulifanyika vizuri na hivi leo ninavyoongea kama mnavyoniona maumivu yote
niliyokuwa nayo mwanzo yameacha na ninajisikia vizuri,” alisema Mhe Selelii.
Mhe. Selelii alisema
kabla ya kufanyiwa upasuaji huo alianza kusikia moyo unapata vichomi maumivu
ambayo yalikuwa yakienda hadi mgongoni, ni ugonjwa ambao hakuwahi kuugua katika
maisha yake.
“Nilikuja Dar es Salaam
kwa ajili ya mambo yangu binafsi lakini ghafla nikiwa hotelini usiku ndio
nikaanza kupata maumivu ambayo yalinifanya niamke asubuhi na mapema kwenda hospitali
kwa ajili ya matibabu,”
“Vipimo vya awali vilionesha
nina shinikizo la juu la damu la 170 kwa 120, na kushauriwa nitumie dawa za
presha, baada ya kuwasiliana na ndugu na jamaa kuhusu hali niliyokutwa nayo
walinishauri nifike hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi
zaidi,” alisema Mhe Selelii.
Baada ya kufanyiwa vipimo
katika hospitali ya Muhimbili ilionekana kuwa na viashiria vya magonjwa ya moyo
hivyo kufikishwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya
vipimo zaidi na matibabu.
“Kwakuwa sijawahi kuugua
toka kuzaliwa kwangu, sikuwahi kukata bima ya afya, hivyo nilivyoambiwa nina
tatizo la moyo niende JKCI niliwakatalia na kuwaambia sina hela wala bima ya
afya, nashukuru wahudumu wa afya walinishawishi na kuniambia hela hutafutwa lakini
maisha huwezi kuyatafuta mara ya pili hivyo ni vyema kufanyiwa uchunguzi wa
kina ili ijulikane unanatizo gani,”
“Nimefurahia kwa huduma
ya upasuaji wa moyo niliyoipata hapa JKCI maana waliniandaa na kuniambia kila
kitu nitakachofanyiwa katika upasuaji huo na hivyo kunifanya kuwa tayari kufanyiwa
upasuaji bila uoga wowote”, alizungumza kwa furaha Mhe. Selelii.
Kwa upande wake daktari
bingwa wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evarist
Nyawawa alisema walimpokea Mhe. Selelii akiwa na matatizo ya kushindwa kupumua
na kuishiwa nguvu, ambapo baada ya vipimo ilionekana mishipa mitatu ya damu
inayopeleka damu katika misuli ya moyo kuziba.
“Upasuaji tuliomfanyia ni
wa kuvuna mishipa ya damu kutoka katika miguu na kuipandikiza kwenye moyo,
upasuaji huu umechukua masaa matano na baada kufanikisha matibabu hayo mgonjwa
tulimuhamishia katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) baada ya hali yake
kuimarika alipelekwa wodini na anaweza kuruhusiwa siku yoyote kuanzia sasa”,
alisema Dkt. Nyawawa.
Upasuaji uliofanyika ni
wa kuvuna mshipa mkubwa wa damu kutoka kwenye mguu na ndani ya kifua na kuipandikiza juu ya mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba ili
kuifanya damu iweze kupita vizuri (Coronary
Artery Bypass Grafting -CABG).
Comments
Post a Comment