TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) YAOMBWA KUWAFIKIA WANANCHI WENGI ZAIDI HASA WANAOISHI MAENEO YA VIJIJINI
Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wakiwapima wananchi waliotembelea banda la JKCI lililopo ukumbi
wa Karume shinikizo la damu (BP) pamoja na kutoa ushauri wa magonjwa ya moyo
wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Mary Haule akimpima kiwango cha sukari mwilini mwananchi aliyetembelea banda la JKCI JKCI
lililopo ukumbi wa Karume wakati wa maonesho
ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Smitha Bhalia akimweleza kuhusu ugonjwa wa
kutanuka kwa moyo mwananchi aliyetembelea banda la JKCI lililopo ukumbi wa
Karume wakati wa maonesho ya 44 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Winnie Masakuya akimuelezea mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi
hiyo namna ambavyo mishipa inayopeleka damu kwenye moyo inavyoweza kuziba
kutokana na kuganda kwa mafuta katika
mishipa hiyo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es
Salaam.
Wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wakiwahudumia wananchi
waliotembelea banda la JKCI wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa
ya Dar es Salaam. Katika maonesho hayo Taasisi hiyo inatoa huduma za upimaji na
ushauri wa magonjwa ya moyo.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Ipyana Mwailafu kiwango cha sukari mwilini mwananchi aliyetembelea banda la JKCI
lililopo ukumbi wa Karume wakati wa
maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wakiwahudumia wananchi
waliotembelea banda la JKCI wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa
ya Dar es Salaam. Katika maonesho hayo Taasisi hiyo inatoa huduma za upimaji na
ushauri wa magonjwa ya moyo.
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeombwa
kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini ili waweze
kupata huduma za upimaji, ushauri na matibabu ya moyo kama wanazozitoa kwa
wananchi wanaoishi mjini.
Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wananchi
waliotembelea banda la Taasisi hiyo lililopo ukumbi wa Karume kwa ajili ya
kufanya vipimo na kupata ushauri wa magojwa ya moyo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam.
Wananchi hao walisema watu wengi wanaoishi maeneo ya
mjini wanapata nafasi ya kupima afya zao mara kwa mara hii ni kutokana na
taasisi mbalimbali za afya kufanya upimaji wa bila malipo tofauti na ilivyo kwa
wanachi wanaoishi vijijini.
“Leo hii nimetembelea katika maonesho haya nimepata
bahati ya kupima afya na kupata ushauri wa mtaalamu wa lishe ambao utanisaidia
kula chakula bora ambacho hakitaniletea madhara katika mwili wangu”, alisema Patricia
Chikojo ambaye ni mkazi wa Mkuranga mkoani Pwani.
Patricia aliwashauri wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam
pamoja na mikoa ya jirani kutembelea banda la Taasisi hiyo lililoko katika
ukumbi wa Karume ili waweze kupata huduma mbalimbali za upimaji wa magonjwa ya
moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi hiyo.
“Wito wangu kwa wananchi watembelee maonesho hayo na
kwenda kupima magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa moyo kwa kufanya hivyo
watatambua hali zao kuliko kusubiri waumwe ambapo wanaweza kugundulika kuwa na
magonjwa makubwa ambayo matibabu yake yakawa ya gharama au magonjwa hayo
yakashindwa kutibika kutokana na kuchelewa kugundulika”, alisema Patricia.
Kwa upande wake Cyril Kessi ambaye ni mkazi wa Dar es
Salaam alifurahia huduma aliyoipata ya upimaji na ushauri wa magonjwa ya moyo
pia alipata muda wa kupima vipimo mbalimbali ikiwemo urefu, uzito, damu,
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) na umeme wa moyo (ECG).
“Huduma niliyoipata ni nzuri, kuna vipimo nimepima
bure na vingine nimelipia gharama kidogo ukilinganisha na kama ningekwenda
Hospitali kupima. Pia nimepata muda wa kutosha wa kuzungumza na daktari ambaye
amenieleza kwa kina kuhusu magonjwa ya moyo”, alisema Kessi.
Akizugumzia kuhusu maonesho hayo Mkuu wa kitengo cha
Utafiti na Mafunzo wa Taasisi hiyo Dkt. Naiz Majani alisema katika maonesho hayo wanatoa
huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo bila malipo yoyote, upimaji wa
magonjwa ya Moyo vikiwepo vipimo vya damu, ECHO na ECG.
Ushauri wa kiafya
kuhusiana na magonjwa ya moyo, elimu ya lishe bora, kuelezea kwa kina huduma
zinazotolewa na Taasisi hiyo na kutoa Rufaa ya moja kwa moja kwa wagonjwa
watakaokutwa na matatizo ya Moyo yanayohitaji kupewa rufaa.
Dkt. Naiz ambaye pia
ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema asilimia kubwa ya watu waliowapima walikuwa wanatumia
dawa za shinikizo la damu (BP) lakini baada ya kuona hali zao ziko vizuri
wameacha kutumia dawa kitu ambacho siyo sawa kwani mgonjwa wa shinikizo la damu
akianza kutumia dawa hatakiwi kuziacha katika maisha yake yote.
“Tumewaanzishia dawa wagonjwa tuliowakuta wameacha
kutumia dawa za shinikizo la damu pia tumewaeleza madhara ya kuacha kutumia
dawa hizo hii ikiwa ni pamoja na moyo kutanuka na kushindwa kufanya kazi,
kupofuka kwa macho, figo kuacha kufanya kazi, kiharusi na vifo vya ghafla”,
alisema Dkt. Naiz
Aliwashauri wazazi wanaokwenda kupima afya zao katika
banda hilo kwenda kupima na familia zao wakiwemo watoto kwani tafiti zinaonesha
kuwa kati ya watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai mmoja anatatizo la moyo.
Comments
Post a Comment