Fanyeni kazi kwa uweledi na ufanisi katika kutekeleza majukumu yenu ya kazi
Wafanyakazi
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa uweledi,
ufanisi na kuepuka vitendo vyote vinavyoweza kuwasababishia kushindwa kufikia
hatua ya kustaafu katika utumishi wa umma.
Rai
hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Tatizo Waane wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wastaafu wawili
waliofikia ukomo wa utumishi wa umma hivi karibuni na kuagwa leo katika ukumbi
wa Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo Dkt. Waane amesema kuwa wapo watu wengi ambao wanaanza
utumishi wa umma katika ngazi mbalimbali lakini hawafikii ukomo wa utumishi wao
kutokana na sababu mbalimbali, hivyo ni vyema kwa wastaafu hao kumshukuru Mungu
kwa kuwafikisha salama siku ya leo.
“Mnastahili
pongezi kwa utumishi uliotukuka, Tunafahamu ni kwa namna gani ambavyo mmekuwa
mkifanya kazi, mmekuwa mkitoa huduma bora kwa wagonjwa wetu, kila mstaafu
amekuwa na namna yake ya kufanya kazi, mmetumia utashi mwingi na kujitoa kwa
ajili ya wagonjwa, hongereni sana” alisema Dkt. Waane.
Aidha
Dkt. Waane amewataka wastaafu hao kutokusita kuendelea kutoa maoni yao yatakayoiboresha
JKCI ili kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini pamoja na kujenga
undungu ambao umejengwa baina yao.
Kwa
upande wake mstaafu ambaye alikuwa Afisa Uuguzi Marcelina Granima ameushukuru
uongozi wa JKCI kwa kuwa Taasisi ya umma ya kipekee kabisa katika kutoa huduma
bora za afya lakini pia kuwawekea mazingira salama na wezeshi watumishi wake.
Granima
amesema kuwa safari ya utumishi wake wa umma haikuwa raisi, ilikua ni safari
ndefu yenye mafanikio na matope mengi lakini kwasababu kazi ya uuguzi na
udaktari ni kazi ambayo inahitaji wito hivyo kumfanya kuendelea kujitoa kwa
ajili ya wagonjwa.
“Nawasihi
watumishi wenzangu mnaoendelea na utumishi wa Umma, ni vyema mkawa na hekima
katika kazi, mjue yakuwa hamkuja kazini kutembea, bali angalieni hekima ambayo
Mungu amewapa katika kutekeleza majikumu yenu” alisema Granima
“JKCI
mtaani inapeperuka kama bendera, naenda kuwa mwakilishi wenu mzuri, hili jina
tulilolijenga liendelee kukua na kuheshimika Tanzania na duniani kote” alisema
Granima
Naye
mstaafu aliyekuwa Mhudumu wa Afya Sofi Josiah amewataka wafanyakazi wa JKCI
kuendelea kuwa na ushirikiano unaojenga na kuifanya JKCI kuwa Taasisi bora
zaidi.
“Kustaafu ni matakwa ya kisheria, kikubwa zaidi ni kustaafu na kuacha kumbukumbu katika nafasi uliyokuwa ukiitumikia, niwaombe wote tufanye kazi kwa ushirikiano na tukistaafu tukumbukwe kwa uweledi wetu kazini” alisema Sofi
Mkurugenzi
wa Kurugenzi ya huduma ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Robert Mallya katika picha ya pamoja na wastaafu Afisa Uuguzi wa JKCI Marcelina
Granima (wapili kushoto) na Sofi Josiah (wapili kulia mstari wa chini) pamoja
na baadhi ya wafanyakazi baada ya hafla fupi ya kuwaaga wastaafu hao
iliyofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment