Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuondoa uzembe na vitendo vya rushwa mahali pa kazi
Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kwa dhati kuondoa
uzembe na vitendo vyovyote vya rushwa mahali pa kazi hii ikiwa ni pamoja na
kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua mkutano
wa sita wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo uliofanyika hivi karibuni jijini
Dar es Salaam ambao ulipitia makadirio ya bajeti ya JKCI kwa mwaka wa fedha wa
2022/2023.
Prof. Janabi alisema ni wajibu wa kila mfanyakazi kuhakikisha
anafahamu wajibu wake mahali pa kazi,anafanya kazi kwa bidii, anatekeleza malengo aliyopangiwa katika muda
uliopangwa. Vilevile kwa mfanyakazi anatakiwa kutunza mali na vifaa
alivyokabidhiwa kufanyiwa kazi na kuwahi kazini ili kuiwezesha Hospitali hiyo
kusonga mbele katika kutekeleza malengo ya Serikali pamoja na kutoa huduma a bora
kwa wananchi.
“Mfanyakazi wa JKCI anatakiwa kufahamu ni huduma ya kiwango
gani aitoe kwa wagonjwa na ndugu zao wakati huo huo ni lazima ajue bajeti
iliyotengwa kwa ajili ya shughuli zake ndani ya Taasisi ili afanye kazi kwa
kuzingatia malengo na rasilimali zilizokadiriwa kutumika”,.
“Utaratibu ambao bajeti huandaliwa kulingana na mipango kazi
iliyoainishwa kwenye mpango mkakati wa Taasisi kulingana na vyanzo vya mapato
na rasilimali zilizopo. Mtindo huu wa bajeti huonesha wazi wazi utendaji wa
kila idara hususan kwa mtu mmoja mmoja kulingana na vipimo vya utendaji wake”,
alisema Prof. Janabi.
Akiwasilisha makadirio
ya bajeti ya JKCI kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Mkurugenzi wa Fedha na
Utawala CPA Agnes Kuhenga alisema bajeti hiyo ya shilingi bilioni 44.6 imelenga
zaidi katika ununuzi wa vifaa tiba na vitendanishi, madawa, ujenzi wa jengo la
utawala na vipimo, mafunzo kwa watumishi na mishahara na posho za wafanyakazi.
Aidha CPA Agnes alisema katika kuboresha kipato cha wafanyakazi,
Taasisi hiyo ilianzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) mwaka 2019 ambayo
hadi sasa kina wanachama 91 ambao ni wafanyakazi wa JKCI na tayari kimeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi
milioni 200.
“Kuwepo kwa JKCI SACCOS kumewasaidia kwa kiasi kikubwa
wafanyakazi wetu kuweka akiba na kupata mikopo ambayo wanaitumia katika
shughuli za maendeleo yao binafsi ili kujikwamua kiuchumi. Jambo la kufurahisha ni
kuwa wanachama hawa wanalipa mikopo yao
kwa wakati na hivyo kuiwezesha SACCOS
hii kuwa na mafanikio makubwa zaidi”, alisema CPA Kuhenga.
Kwa upande wake Mwenyekiti mteule wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi
hiyo Prof. William Mahalu aliipongeza managenenti ya JKCI kwa kuwa na maelewano
mazuri baina yao na wafanyakazi, uongozi wa Chama cha Wafanyakazi
wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE)na baraza la wafanyakazi jambo linalosaidia kuwepo na utoaji mzuri wa
huduma kwa wagonjwa na wananchi wanaowahudumia.
Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo
katika Hospitali ya Kanda Bugando aliwapongeza wafanyakazi wa JKCI kwa huduma bora na za kisasa za matibabu ya
moyo wanazozitoa kwa wagonjwa na kuwaomba waendelee na moyo huo huo ili huduma
hizo ziwe endelevu ili wagonjwa waendelee
kutibiwa hapahapa nchini na siyo nje ya nchi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Ninawapongeza kwa
bajeti nzuri mliyoiandaa ambayo imegusa idara zote za Taasisi ikiwepo kutengwa
kwa fedha za kuwasomesha wafanyakazi. Ninawaomba wale ambao mtapata nafasi ya
kwenda kusoma muitumie vizuri nafasi hiyo ili mtakapomaliza mrudi na ujuzi
ambao utaboresha utoaji wa huduma kwa wananchi”, alisema Prof. Mahalu.
Comments
Post a Comment