EAC, SADC wakaribishwa JKCI kutibiwa magonjwa ya moyo
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela akiwaonesha viongozi wa wizara
zinazosimamia vituo vya umahiri (center of excellence) pamoja na viongozi wa
vituo hivyo kutoka nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) jinsi tundu
lililoko kwenye moyo linavyozibwa kwa
kutumia mtambo wa Cathlab wakati viongozi hao walipotembelea JKCI kwa ajili ya
kuangalia huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Prof. Mohamed Janabi akielezea huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na
taasisi hiyo kwa viongozi wa wizara zinazosimamia vituo vya umahiri (center of
excellence) pamoja na viongozi wa vituo hivyo kutoka nchi wanachama wa Jumuia
ya Afrika Mashariki (EAC) na wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini
Zambia walipotembelea Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi wa wizara zinazosimamia vituo vya umahiri
(center of excellence) pamoja na viongozi wa vituo hivyo kutoka nchi wanachama
wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini
Zambia wakifuatilia wasilisho la matibabu ya moyo lililokuwa linatolewa na Prof. Janabi wakati
wa ziara iliyofanywa na viongozi hao ya kuangalia huduma za matibabu ya moyo
zinazotolewa na taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Shirika la Save a Child Heart (SACH) la nchini
Israel Simon Fishers akielezea ushirikiano uliopo kati ya Israel na Tanzania
katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto wakati wa ziara iliyofanywa
na viongozi wa wizara zinazosimamia vituo vya umahiri (center of excellence)
pamoja na viongozi wa vituo hivyo kutoka nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika
Mashariki (EAC) waliyoifanya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Tulizo Shem akiwaelezea huduma zinazotolewa katika wodi ya
watoto wenye magonjwa ya moyo viongozi wa wizara zinazosimamia vituo vya
umahiri (center of excellence) pamoja na viongozi wa vituo hivyo kutoka nchi
wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) wakati wa ziara ya kuangalia
huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Na: JKCI
****************************************************************************************************************************************************************
Nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameombwa kupeleka wagonjwa wao kutibiwa
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwani matibabu yanayotolewa ni ya
umahiri wa hali ya juu hayana tofauti na yanayotolewa nchi za Ulaya na India.
Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wizara ya
Afya ambaye ni Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka wizara hiyo Dkt. Saitore Laizer
wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa ziara ya
viongozi wa wizara zinazosimamia vituo vya umahiri (center of excellence)
pamoja na viongozi wa vituo hivyo kutoka nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika
Mashariki waliotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili yakuona
huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Dkt. Laizer alisema mashine zinazotumika kuchunguza na kutibu
magonjwa ya moyo na mishipa ya damu zilizopo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ni
zilezile zinazotumika Ulaya na nchini India ambazo katika nchi za Afrika ziko
tatu na Afrika Mashariki ziko mbili.
“Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete pako salama na gharama za
matibabu wanaweza kuzimudu ukilinganisha na maeneo mengine ambayo wangeenda kutibiwa nje ya Afrika pia mazingira
ni hayohayo ya kiafrika ambayo wameyazoea na hata stress za kuwa nje
ya nchi wanaweza kuziepuka”, anasema Dkt. Laizer.
Akizungumzia kuhusu ziara hiyo ya ugeni kutoka nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika
Mashariki Dkt. Laizer alisema katika
Afrika Mashariki wametengeneza vituo vya umahiri wa matibabu tofauti kwa kila
nchi kwa upande wa Tanzania ilichaguliwa kuwa kituo cha umahiri wa matibabu ya moyo na
mishipa ya damu.
Alisema ujenzi wa kituo hicho unasimamiwa na wizara ya Elimu kupitia
chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) kwani taasisi hizi mbili zinafanya kazi kwa pamoja
kwa sababu mwananchi anayelengwa ni mmoja.
“Hatuwezi kuzungumzia matibabu ya moyo na mishipa ya damu pasipo
kujumuisha Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI), Taasisi ambayo imeleta
mapinduzi makubwa katika matibabu ya moyo nchini na Afrika ya Mashariki na
Kati. Ujumbe wa nchi za EAC uko hapa
wamepata maelezo na wengine wamekiri hawakuwa wanafahamu kama kuna huduma hizo
hapa nchini ambazo hata kama mtu angeenda kutibiwa mbali na Afrika angezipata”,.
“Ujio wa ugeni huu ni kuona huduma zinazotolewa ambazo
zitashahibiana na kile ambacho wanachama
wa nchi za Afrika Mashariki wamependekeza Tanzania iwe na kituo cha umahiri wa
matibabu ya moyo na mishipa ya damu kwa hiyo wageni wamefurahi sana na wakitoka hapa wataenda Mloganzila
kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho umefikia wapi”, alisema Dkt. Laizer.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa wizara
zinazosimamia vituo vya umahiri (center of excellence) pamoja na viongozi wa
vituo hivyo Dkt. Nicholus Ndongi kutoka nchini Kenya alisema hii ni mara ya
tatu wanakutana na leo hii wako nchini
Tanzania kwa ajili ya kuona hatua ya ujenzi wa kituo cha umahiri cha
magonjwa ya moyo na mishipa ya damu umefikia katika hatua gani na kuangalia
kama kuna matatizo yanayokwamisha ujenzi huo na kama yapo ni kwa ajili gani na
angalia namna ya kuweza kutatua matatizo hayo.
Alizitaja sababu ya kuanzishwa kwa vituo hivyo vya umahiri ni
mawaziri wa Afya wa Afrika Mashariki waliona watu wanapata shida wanapopata
magonjwa ambayo hayawezi kutibiwa katika
nchi hizo na kwenda kutibiwa nje ya nchi. Mawaziri walikaa chini na kuona waanzishe
vituo vya umahiri vya matibabu hayo ambavyo vitakuwa na vitendea kazi vyote ili
wagonjwa wasiende nje kwenda kutibiwa
bali watibiwe katika nchi za Afrika Mashariki.
Kila nchi ilipewa kituo cha umahiri ambapo Tanzania ni kituo
cha umahiri wa matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, Uganda ugonjwa
wa saratani, Rwanda chanjo na ufundi wa vifaa tiba (bio medical engineering) na
Burundi lishe.
“Kabla ya kwenda kuona ujenzi wa kituo cha Mloganzila
tumepita hapa Taasisi ya Moyo na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa,
tumefurahi na hatukuwa tunajua kama JKCI inatoa huduma ya juu sana jambo la
muhimu ni watangaze huduma wanazozitoa zijulikane Afrika Mashariki na Duniani
ili watu wajue kuna kituo ambacho
wanaweza kutibiwa na wasiende mbali na Afrika”,.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Prof. Mohamed Janabi aliwashukuru wajumbe hao kwa kutembelea Taasisi
hiyo na kusema idadi ya wagonjwa wanaowatibu
imekuwa ikiongezeka kila mwaka hiyo ni kutokana na kuwa na wataalamu
wenye uzoefu wa hali ya juu pamoja na
vifaa tiba vya kisasa.
“Katika Taasisi hii
tunapokea wagonjwa kutoka nje ya nchi pia Kenya wameanza kuleta wagonjwa na
wiki iliyopita tumewafanyia upasuaji mkubwa wa moyo watoto wawili kutoka nchini
humo pia tunatarajia kupata wagonjwa
wengi zaidi. Burundi pia wanaleta wagonjwa kuja kutibiwa hapa mwaka huu tumeshawatibu wagonjwa sita kutoka nchini humo”, alisema
Prof. Janabi.
Prof. Janabi alitoa ushauri wakati vituo hivyo vya umahiri
vinajengwa pamoja na kuwasomesha
madaktari bingwa, technician na wauguzi waangalie namna ya kuwasomesha
wataalamu wa vifaa tiba (bio medical engineering) kwani vifaa hivyo ni vya gharama kubwa ni vizuri wawe na mafundi
wao ambao wataijua mitambo na kufanya matengenezo madogo pale itakapoharibika
kuliko kutegemea mafundi kutoka nje au kutoka kwa waliuwauzia mitambo ambao
watawalipa fedha nyingi.
Wakati huohuo Lyidia Irima kutoka nchini Kenya ambaye mtoto
wake amefanyiwa upasuaji wa moyo alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema
kuwa mtoto wake alizaliwa na matatizo ya moyo na walimgondua akiwa na umri wa
mwaka mmoja na miezi mitatu alizunguka katika Hospitali mbalimbali lakini
hakuweza kupona hadi alipofika JKCI.
“Mtoto wangu alikuwa na matunu kwenye moyo na mishipa
inayopeleka damu kwenye moyo ilikuwa na shida hakuwa anaweza kuhema vizuri
lakini baada ya kufanyiwa upasuaji anapumua vizuri ile sauti aliyokuwa anatoa
haiku tena”,.
“Ninawaambia wamama wa Afrika Mashariki ambao watoto wao
wanamatatizo kama ya mwanangu wasife moyo kwani kuna Hospitali zinazoweza
kuwasaidia watoto wao ikiwemo Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wanaweza
kuja hapa wakatibiwa”, alisema Lyidia .
Wakiwa katika Taasisi hiyo viongozi hao walitembelea maeneo
mbalimbali ya Taasisi hiyo ikiwemo mitambo ya Cathlab, wodi za wagonjwa walioko
katika uangalizi maalum (ICU) na wodi ya
watoto.
Comments
Post a Comment