Kateni bima za afya kumudu gharama za matibabu – Prof.Janabi
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimpima shinikizo la damu (BP) mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya vipimo vya magonjwa ya moyo na kisukari wakati wa maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kuhenga akisaini kitabu cha wageni
alipotembelea banda la Taasisi hiyo lililopo katika Maonesho ya 46 ya Biashara
ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayoendelea kwenye viwanja vya
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Mteknolojia wa maabara wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jordan Megabe akimchukuwa kipimo cha damu
mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kumfanyia vipimo vya
kuchunguza figo, ini na kiwango cha mafuta mwilini wakati wa Maonesho ya 46 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayoendelea katika viwanja
vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Mzuma Mzuma akitoa ushauri wa matumizi sahihi ya dawa za moyo
kwa mwananchi aliyefika katika banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma
ya vipimo vya magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 46 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Baadhi ya wananchi
waliotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakipatiwa huduma za vipimo na ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa
ya moyo wakati wa maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es
Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Picha na: Khamis Mussa
****************************************************************************
Wananchi wahimizwa kukata bima za afya kumudu huduma za matibabu kwani magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo hutumia gharama kubwa kuyatibu na mara nyingi hutibiwa kwa kipindi chote cha maisha pale mtu anapogundulika kuwa na magonjwa hayo.
Rai hiyo imetolewa jana na
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi wakati wa maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA)
yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo
barabara ya Kilwa.
“Ni muhimu kila mtanzania akakata
bima ya afya kwani matibabu ya moyo ni gharama, mtu mwenye magonjwa haya
hutibiwa maisha yake yote, na dawa zinazotumika pia gharama hivyo huwezi kuwa
unatoa hela kila siku kwa ajili ya matibabu kwani hata uchumi wako
unaweza kuyumba kwa ajili ya matibabu” alisema Prof. Janabi.
Aidha Prof. Janabi aliwahimiza
wananchi kutembelea katika banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanyiwa
uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari ili kujenga tabia ya kuchunguza afya
zao mara kwa mara
“Uchunguzi huu wa magonjwa ya moyo
kwa wananchi usiishie hapa Sabasaba, tuwe na tabia ya kuchunguza afya zetu mara
kwa mara katika vituo vya afya vilivyo karibu nasi ili pale tutakapogundulika
kuwa na matatizo na kuhitaji huduma za kibingwa zaidi tuweze kupata rufaa
mapema kufika katika hospitali yetu kwa ajili ya matibabu zaidi”, alisema Prof.
Janabi
Prof. Janabi alisema kuwa watu
wanaowafanyia vipimo katika banda la JKCI lililopo Sabasaba na kugundulika kuwa
wanahitaji huduma za kibingwa zaidi hupatiwa fursa ya moja kwa moja kwenda
kwenye Taasisi hiyo kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Niko hapa katika banda letu kwa
ajili ya kutoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na
sukari mwilini. Mwananchi niliyetoka kumhudumia sasa hivi nimekuta anatembea na
presha ya 195 kwa 117 ambapo kidaktari ni hatari kwa sababu ni mtu ambaye
akianguka hapo huwezi kushangaa kutokana na shinikizo lake la damu kuwa juu”,
“Tumemuanzishai dawa za Shinikizo
la juu la damu kwa ajili ya kuweka presha yake sawa, lakini tumemshauri
kufuatilia mwenendo wa presha yake mara kwa mara na pale atakapoona anahitaji
huduma zaidi afike katika Taasisi yetu”, alisema Prof. Janabi.
Kwa upande wake mwananchi
aliyepatiwa huduma katika banda la JKCI Rehema Daniel aliwapongeza wataalam wa
afya wa Taasisi hiyo kwa kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kabla ya kufanyiwa
vipimo kwani kwa kufanya hivyo kumemuwezesha kufahamu sababu, viashiria na
namna ya kuepukana na magonjwa ya moyo.
“Sikuwa na uelewa wa kina kuhusu
magonjwa haya ya moyo, lakini elimu niliyoipata hapa leo inaniwezesha kwenda
kuwa mwalimu katika familia yangu kuhusu magonjwa haya kwa kuhakikisha kuwa
familia yangu inaepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo”,
“Naelewa umuhimu wa kuwa na bima ya
afya ndio maana hata mimi ninayo, rai yangu kwa wananchi wenzangu ni kuwa na
kadi hizi za bima ya afya kwasababu maradhi hutufika wakati wowote bila kuangalia
kama wakati huo tuko vizuri ama vibaya kiuchumi”, alisisitiza Rehema.
Naye Mteknolojia wa Maabara wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Jordan Megabe alisema kuwa mwitikio wa wananchi
kufika katika banda la JKCI kuchunguza magonjwa ya moyo na vipimo vya damu
vinavyofanywa maabara ni mkubwa kutokana na hamasa zinazotolewa katika banda
hilo.
“Tupo hapa Sabasaba kwa ajili ya
kuwahudumia wananchi kutoka pande zote za Tanzania wasisite kufika katika banda
letu, tumejipanga kutoa huduma bora kwa kila mwananchi anayehitaji kufanyiwa
uchunguzi wa magonjwa ya moyo”, alisema Jordan.
Comments
Post a Comment